Featured Post

WAIRAQW: WANAPATIKANA MANYARA, LAKINI NI JAMII ILIYOTOKA NCHI YA IRAQ

Warembo wa Kiiragw wakati wanawania taji la Miss Mbulu


Na Innocent Nganyagwa
TUNAZUNGUMZIA kabila mojawapo la Kikushi, Wairaqw, watu waliotokea mbali kabla hawajafika mahali walipo sasa.
Barani Afrika tuna takriban mbari (races) kuu tano zinazounda makabila yetu. Mojawapo ya mbari hizo ni Wakushi nyingine ni Wabantu, Wakhoisan, Wahamitiki na Wanailotiki.

Zipo mbari zinazotokana na mchanganyiko wa mbari mbili au zaidi, ndipo unaweza kusikia kuna Wabantu na Wanailotiki wa Kihamitiki. Baadhi ya makabila mengine ya Kikushi ni pamoja na Wanyaturu, Wafyomi na hata Wasi, japo pia si kwa ujumla wake maana wana mchanganyiko wa mbari nyingine ndani yake.
Kwa asili hawa Wairaqw wanatokea nchi anayotokea Saddam Hussein, yaani Iraq.
Mwendo wao hadi kufika huku kwetu si wa miaka michache, tena unaweza kuwa wa karne kadhaa zilizopita mpaka kufika mahali walipo hivi sasa. Kuna njia moja rahisi ya kufahamu uwezekano wa jamii za makabila kutoka maeneo ya mbali, ambayo yamelowea maeneo mengine yaliyo mbali sana na chanzo chao cha asili.
Hapo ndipo umuhimu wa mlinganyo wa kutumia vyanzo mbalimbali vya utafiti unapohitajika, hasa unapokabiliwa na utata wa kufahamu mahali lilipoanzia kabila. Nikumegee kidogo Mjadi baadhi ya vyanzo hivyo, ndipo utakapofahamu si rahisi kutayarisha maandishi haya kama inavyodhaniwa.
Mathalan, unaweza kutumia maandiko kama sehemu ya historia bila kugubikwa na uhafidhina wa kiimani.
Kwenye maandiko kuna simulizi za Nuhu na watoto wake – Sham, Ham na Japhet – naye Ham ana uzao wake wakiwamo watoto wake – Egypt (Misri), Cush (Abyssinia, Ethiopia) na Libya. Hayo ni majina ya nchi zilizopo Afrika, lakini kumbuka kuwa zamani maeneo yalipata majina kutokana na sifa za jamii husika, au jina la mtu wa jamii fulani aliyefanya mambo makuu.
Ni sawa na tutakavyoona hapo baadaye jinsi ‘Wambulu’ walivyotokana na Wairaqw, ni kama jiografia ya Afrika na Mashariki ya Kati ikiwemo Israel wanakotokea Wakurya wa Kinyabhasi inavyojidhihirisha.
Tafuta ‘Atlas’ na uangalie ramani ya Afrika au ya dunia, kisha tazama utangamano wa maeneo hayo mawili. Ili upate taswira halisi futa mipaka ya nchi na maeneo hayo, maana hiyo kwa sehemu kubwa ilitokana na siasa za utawala.
Ndipo nikikuambia kuwa hapo zamani nchi za Ethiopia, Eritrea na zile Somalia tatu, yaani ile yenye mji wake mkuu Mogadishu alikotawala Siad Barre, Punt Land na Somali Land zote zilikuwa nchi moja, utaamini.
Ni kama nchi wanayotokea Wamaasai ambayo zamani ilikuwa moja, yaani Misri na Sudan, huku hao Wamaasai wakitokana na jamii inayoongea lugha yao mama inayoitwa ‘Maa’. Lugha hiyo baadaye ilizaa lugha nyingi za makabila mengi, yaliyokuja maeneo ya kusini kupitia bonde la mto Nile. Jiografia nayo ni moja ya vyanzo muhimu vya kung’amua makabila yalikoanzia. Na inavyoelekea, kadiri miaka inavyokwenda ramani ya dunia inazidi kubadilika, maana hadi miaka ya hivi karibuni taifa changa kabisa kuliko yote lilikuwa East-Timor. Lakini kwa sasa nchi changa zaidi ni Kosovo, usisahau South Sethia, Ingushetia, Chechnya na kwingineko.
Nadhani unakubaliana nami kuwa huu ni mkoroganyo maridhawa unaohitaji uangalivu kuudadavua lakini tusisahau ukweli halisi wa jamii zilizofifia na kupotea.
Mathalan, Wanubi ni miongoni mwa wenyeji wa kwanza wa Misri waliojenga mapiramidi na kuweka msingi mkubwa wa utamaduni wa huko.
Hata ukitazama baadhi ya silabi za muundo wa lugha tanzu za Kiarabu, zimekopa sana kwenye lugha yao. Mnubi akiongea wakati mwingine unaweza kufikiri anaongea Kiarabu kisicho sahihi, hata hivyo tuachane na mambo hayo kwa sasa, maana yana mtiririko wenye kina kirefu sana kihistoria.
Kwa sasa tuwaangalie kwa ukaribu hawa Wairaqw, wanaopatikana kwa wingi huko Manyara na Arusha katika wilaya za Mbulu, Babati, Hanang na Karatu.
Lakini usishangae nikikuambia kuwa wapo hata mahali tulipokuwa mara ya mwisho, yaani Kondoa, hiyo ni kutokana na kupita mahali hapo wakati wanaelekea kwenye makazi yao ya sasa. Makabila haya tunayoyatembelea sasa kwenye eneo hili, yanapatikana kimafungu katika uwanda unaotokea kaskazini mashariki hadi magharibi mwa nchi yetu. Wairaqw wanatokea huko Iraq ambako zamani kulifahamika zaidi kama Messopatamia, mahali ambapo jamii zao zilizofika huku zilitoka tangu karne za mwanzoni kabisa.
Kutoka huko walivuka bahari ya Sham na kulowea Ethiopia, mahali walipokumbwa na vita vya mara kwa mara. Kutokana na hali hiyo wakaondoka kuelekea upande wa kusini magharibi, wakipitia Bonde la Ufa kando mwa Ziwa Victoria.
Wakaja hadi maeneo ya Iramba mkoani Singida, kisha wakaelekea ulipo mpaka wa mikoa ya Dodoma na Iringa. Wakahofia kwenda kusini zaidi kutokana na mapambano yaliyokuwa yamepamba moto baina ya Wahehe na Wangoni, wakageuza na kwenda Guse Tulaway, Kondoa.
Hapo walitulia na kuanza kulima na kufuga, lakini vita iliwaandama tena na safari hii walisigana na Wabarbaig.
Wakaamua kuondoka na kwenda Mlima Hanang’, lakini wengine walienda Gallapo au kwa jina lingine panaitwa ‘Tsea Daaw’ hawa ndiyo walizalisha kundi la jamii ya kabila la Wagorowa.
Kundi jingine lilienda Dabil na Gangaru na kuamua kulowea maeneo hayo, kutoka hapo wakiongozwa na Haymu Now Haytipe walielekea eneo la Mama Isara na kuishi mahali hapo.
Itabidi uyavumilie na kuyazoea matamshi ya kijadi ya Kiiraqw, maana hata majina yao ni kama unavyoyaona, ndiyo mambo ya lugha zao za Kimesopotamia!
Tukirejea kwenye ule msafara wao ulioongozwa na kiongozi wao Haymu, walipofika hapo Mama Isara waliishi milimani maana eneo lote hilo hapo zamani lilikuwa ziwa. Huyo kiongozi wao alitumia ujuzi wake wa uganga wa jadi, kuongeza ukubwa wa ardhi waliyoihitaji kwa kilimo.
Alimuagiza mtumishi wake aitwaye Moya kutupa mshale ili uchome katikati ya ziwa, mtumishi huyo alipofanya hivyo lile ziwa lilihama. Ziwa lile lilihama na yule mtumishi na kusogea hadi usawa wa bonde la ufa, hilo ndilo lile ziwa ambalo kwa sasa linaitwa ziwa Manyara lakini kwa lugha yao wao huliita ‘Tlawta Moya’. Eneo lilipoongezeka baada ya ziwa kuhama waliendelea na maisha yao kama kawaida. Baadaye wakatawanyika maeneo ya Muray, Kuta, Amoa, Kainam, Suum, Datlaa, Tsaayo na Mbulu.
Baadaye kabisa wengine wakatawanyikia maeneo ya Karatu, Babati na Hanang’, mahali wanakopatikana kwa wingi hata sasa. Ndugu zetu hawa ambao baadhi ya mambo yao yanafanana kwa karibu mno na Wayahudi, awali walipendelea zaidi kula nyama zilizotokana na wanyama waliowawinda na mifugo yao.
Hawa Wairaqw ni jamii ya watu wa siku nyingi mno, kwa hiyo wamepitia zama za mawe hadi chuma. Mathalan, zamani kabisa walichuna ngozi za wanyama kwa kutumia mawe yaliyochongoka. Kisha walichoma nyama hizo kwa moto uliowashwa kwa kutumia kibiriti chao cha asili ‘bui na daha’ yaani kupikicha vijiti. Vyakula vyao vilivyotokana na mazao waliyoyagundua kama vile mtama, ulezi na uwele, walivisaga kwa kutumia mawe ya kusagia. Unga wa nafaka hizo ulipikwa ugali laini ambao wenyewe huuita ‘xwante’ unaoweza kuulinganisha na uji usio wa moto.
Labda ugali huu naweza kuufananisha na uji maarufu wa kwetu Iringa, unaopikwa kwa maziwa na unga wa mahindi unaoitwa ubaga. Nafaka hizo walizozigundua, zilitumika pia kupikia pombe iliyonywewa kwenye sherehe zao za kimila.
Kesho tutaendelea kuwatazama wa undani ndugu zetu hawa Wairaqw.


Makala haya yamehaririwa na yalichapishwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Tanzania Daima Aprili 4, 2009.

Comments