Featured Post

UMEMUONA BEN SAANANE?


Ujumbe wa Ben Saanane wa kuendeleza mapambano mwaka 2016.

Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
LEO ni siku ya 134, au kwa kufuata Kalenda ni miezi minne na siku 16, tangu Bernard Rabiu Focus Saanane, au Ben Saanane, mwanaharakati chipukizi wa kisiasa, alipotoweka Novemba 18, 2016 katika mazingira ya kutatanisha.
Katika hali ya kushangaza kabisa, suala la Ben Saanane limefunikwa ama kuzikwa kabisa na hakuna yeyote anayejali kupotea kwake.
MaendeleoVijijini inasikitika na kuhuzunika kuona uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) umeendelea kukaa kimya kwa kipindi chote hicho wakati Ben Saanane ni mwanachama wao, kada wao na zaidi ni Katibu Myeka (Personal Assistant) wa Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, ambaye naye mpaka sasa hajishughulishi kwa lolote kuhusu kupotea kwa kijana huyo.
Mbowe, ambaye Watanzania wengi wanaofuatilia siasa wanamjua, asingeweza kukaa kimya hata kwa siku mbili, achilia mbali siku 134 zote, baada ya kutoweka kwa msaidizi wake binafsi, ambaye ndiye mshauri wake wa masuala ya siasa.
Hili linaogopesha na kutisha vijana wengi, hasa wanaharakati wa kweli waliokuwa wakipigania mabadiliko na kwa namna ilivyo, inaonekana hakuna aliye salama.

Ben wa Saanane alijitoa muhanga kukitetea chama na hakuogopa kukosoa au kukosolewa, hata kama mabandiko yake mengi yalionekana wazi 'kutumwa', 'kutumika' ama 'kufanya tu propaganda za kubadili upepo'.
Wakati mwingine alikuwa akitoa tahadhari mapema kabla hajaanzisha 'mapambano yake mitandaoni' kama alivyofanya hapa:
"Familia yangu ya Facebook, marafiki wa karibu na wa mbali kwenye mitandnao na nje ya mitandao, Salaam! Kwa rehema na mapenzi yake Mwenyezi Mungu na kwa dhamira ya kweli, moyo usiotetereka katika hali yoyote kimapambano, Ndani ya saa 72 nitatangaza maamuzi."
Nitawaomba mniunge mkono katika maamuzi hayo. Ni makini na sahihi. Yatakuwa matamu na machungu kwa baadhi ya watu. Nimedhamiria...!
The storm will pass, the spring will come.
Let the nature of patience be an encouragement as you continue to wait.
Aluta Continua, Victory Ascerta...
Ben Saanane."
Ukimya wa viongozi wa Chadema, ambao kwa kawaida ndio waliopaswa kuwa mstari wa mbele kushughulikia kupotea kwake, umeleta tafsiri hasi katika jamii, na hii inaweza kuleta taswira moja tu, kwamba huenda wanajua kilichompata kada wao huyo.
 MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, zile kelele za wanaharakati wa Chadema huko kwenye mtandao wa Facebook nazo zimekoma ghafla hali inayotafsiriwa kwamba, huenda "wana taarifa kuwa Ben hajapotea" kwa sababu ghafla wameitosa kampeni yao ya #BringBackBenAlive, kwa mtindo ule ule kama Mbowe na viongozi enzake walivyozitosa "Operesheni UKUTA Toleo la Kwanza", "Operesheni UKUTA Toleo la Pili" na "Operesheni KATA FUNUA."
Kama unabisha nenda Facebook, fuatilia mabandiko ya "vinara" wa #BringBackBenAlive utamelewa hiki ninachokisema.
Desemba 11, 2016 pale LandMark Hotel wale vijana waliojiita Umoja wa Kizazi cha Kuhoji Tanzania (UTG) wakiongozwa na mwenyekiti wao Malisa Godlisten, walitoa tamko na kuipa Chadema saa 72 kutoa taarifa za kupotea kwa Saanane, lakini muda huo ulikwisha kitambo, Ben hajaonekana na hakuna taarifa sahihi za Chadema zilizotolewa ukiacha lawama kwamba ‘serikali ndiyo inayohusika’. Hawa nao wameziba midomo licha ya kufanya biashara ya kuuza T-Shirt za #BringBackBenAlive.

Mwanahalisi lilimaliza kazi
 Gazeti la MwanaHALISI ambalo linamilikiwa na kada wa Chadema inaonekana kama lilimaliza kila kitu kuhusu utata wa kutoweka kwa Ben Saanane.
Kwanza Desemba 26, 2016 liliandika kuhusu “Mbowe ategwa”, kwamba kutoweka kwa mwanasiasa huyo chipukizi na msaidizi wake, huenda ulikuwa ni mpango madhubuti wa kumdhoofisha mwenyekiti huyo.
Hata hivyo, likashindwa kueleza ukweli ni kwa nini Mbowe na viongozi wengine wa ngazi za juju Chadema walikuwa wamepuuzia suala la kupotea kwa Ben.
 Lakini MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, habari inayoonekana kuzima kelele hata za wanaharakati wa Chadema mitandaoni, licha ya baadhi yao kulichoma moto gazeti hilo, ni ile iliyosema “Msaidizi wa Mbowe kuibuka” ambayo ilichapishwa Januari 2, 2017 huku wakieleza kwamba Ben amekuwa akionekana kwa marafiki zake mitaani na kwenye vijiwe vya kahawa huku Mjumbe mmoja wa Kamati Kuu (CC) ya Chadema akisema, “Nina wasiwasi kama siyo mkakati binafsi wa kisiasa. Kijana Saanane amekuwa akionyesha kutaka kukwea madarakani haraka hata nje ya taratibu. Tafuteni tu mtaona.”
Lakini tunazidi kufahamishwa kwamba, gazeti hilo lilipata ‘andishi la mkono’ lililopenyezwa kwenye mlango wa ofisi Jumapili, Desemba 25, 2016 ikieleza kuwa wanajisumbua bure kwa sababu ‘mtoto huyo yupo’.
"Ninyi jisumbueni tu. Huyu mtoto yupo na akitokea mtashangaa. Hamumfahamu Saanane. Sisi tunajua alipo. Wala hatuoni anayetishia maisha yake. Kuna wanaodai kauawa. Ni waongo. Anapumua. Kuna kitu wanaandaa. Kaa chonjo.” Sehemu ya andishi hilo inanukuliwa na Mwanahalisi.

Habari hiyo kubwa kwenye gazeti hilo ilizua maswali mengi ambayo yanahitaji majibu muafaka, kwa sababu ilivyoonekana ni kama njia ya kumsafisha Mwenyekiti Mbowe na sakata hilo.
Kwamba sasa Ben anatuhumiwa ‘kujiteka’ mwenyewe kwa sababu anataka kukwea madaraka nje ya taratibu? Na huo mtego kwa Mbowe ni wa aina gani ambao Ben ameutega?
Kuhusu andishi linalosemwa, ni kwa nini itokee tu likapenyezwe kwenye ofisi za Mwanahalisi wakati kuna magazeti mengi hapa Dar es Salaam? Kwa nini lisipenyezwe kwenye ofisi za Raia Mwema ambao ni jirani zao pale Kinondoni? Kwa nini lisipenyezwe kwenye ofisi za Mtanzania, Mwananchi au hata Uhuru?
Kilicho wazi ni kwamba, Chadema wamejitekenya, na sasa wameamua kucheka kabisa. Kama walikuwa wanataka kutumia kutoweka kwa Ben kama sehemu ya mkakati wao wa Operesheni Kata Funua, basi wameanza vibaya na operesheni hiyo haiwezi kufanikiwa, labda kwa huku kuandikwa mara kwa mara tu.
Kama kuna hila yoyote imefanyika na sasa wanaona mambo yamekaa vibaya hivyo kuamua kutunga habari na kuanza kusafishana, ni wazi Watanzania siyo wajinga kiasi hicho, wanaweza kubaini pumba na mchele.
Mtu mmoja ambaye anaitwa Deo Meck, aliandika kwenye mtandao wa JamiiForums akisema: “Nimekuwa mtumishi wa Makao Makuu ya Chadema, kama Msaidizi wa Mwenyekiti wa Tiafa. Watumishi wote wako chini ya ofisi ya Katibu Mkuu, chini ya Kurugenzi ya Fedha na Utawala, ambaye Mkurugenzi wake, ni Mh. Anthony Komu (MB). Kila asubuhi lazima mtumishi afike ofisni kabla au saa mbili kamili asubuhi na anasaini kitabu cha wafanyakazi getini kwa mlinzi kabla ya kuingia ndani. Hivyo ikitokea mtumishi hajaonekana kazini, siku hiyo hiyo ofisi ya Katibu Mkuu inachukua hatua ya kujua kwa nini hujaonekana.
“Na pia kwa nafasi yake kama Katibu Myeka wa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba kila siku lazima uwasiliane na mkuu wako wa kazi, akupangie majukumu au umpe taarifa ya majukumu uliyotekeleza na kadhalika, kutoweka kwa mtu wa namna hiyo hadi wiki tatu hujatoa taarifa, si polisi tu bali hata kwa wazazi kunazua shaka ya uhusika wako katika sakata hilo.
“Kwa mujibu wa gazeti moja la siku, siku ya tatu ya Ben kutoonekana nyumbani, mmiliki wa nyumba anayoishi alienda makao makuu ya Chadema na kuulizia kama wanajua alipo maana hajamuona siku tatu na simu zake hazipatikani, wao wakamjibu hawajui na inavyodhihirika hawakuchukua hatua yoyote.
“Kwa msingi wa mazingira haya kuna ishara kubwa sana kuwa kutoweka kwa Ben Saanane ni kazi ya ndani ya chama na haswa hao viongozi wakuu na walitaka kulitumia hilo tukio kwa manufaa yao ya kisiasa.”

Ilikuwa janja ya Chadema?
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, akionyesha ujumbe unaodaiwa kuwa wa vitisho kwenda kwa Ben Saanane, wakati alipokutana na wanahabari Desemba 14, 2016.
Ukisoma kwenye mitandao ya jamii mabandiko yaliyotolewa wakati huo, na hata katikati ya mistari ya gazeti la MwanaHALISI utagundua kwamba, viongozi hao wakuu wa Chadema “walikubaliana na Ben kuwa ajifiche na wafanyie tukio hilo siasa” hasa ikikumbukwa kwamba ni katika kipindi hicho Mbowe, John Mrema na wengine walikwenda ziara Ulaya na malalamiko yao yalikuwa ya kukandamizwa na kutekwa, huku nyuma Ben ‘akatoweka’.
Inaonekana hawakujua kwamba mkakati huo ungeweza kuwageuka na ndipo katika kuogopa jumba bovu lisiwadondokee, wakaamua kuandaa mkakati mwingine unaoonyesha kwamba Ben kajificha mwenyewe kwa manufaa ya kisiasa, kwa sababu ana tamaa ya vyeo na yuko tayari kufanya lolote kupanda cheo.
Kwa jinsi mwanasiasa huyo chipukizi alivyo mahiri wa ‘kucheza’ na mitandao ya kijamii, kwa vyovyote vile mpaka angekuwa amejibu mwenyewe kwamba yuko wapi – awe mapumzikoni au kazini – kwa sababu siku zote amekuwa mahiri wa ‘kushinda’ kama siyo ‘kukesha’ kwenye mitandao ya kijamii akianzisha hoja mbalimbali.
Baada ya kushindwa kwa Operesheni Ukuta, Chadema ikaandaa Opereshenii Kata Funua ambayo tunaambiwa ni Ben Saanane ndiye aliyeiandaa kabla ya kupewa ‘likizo’ na Mbowe kwa ‘kazi nzuri’ aliyoifanya.
Ama tafsiri iliyopo ni kwamba, huenda Chadema, au viongozi wa Chadema, walitaka kutumia kutoweka kwa Ben Saanane kama ‘kick’ yao ya kuianzisha Operesheni Kata Funua kwa kusingizia kwamba kupotea kwake ni hujuma za Serikali ya Chama cha Mapinduzi – CCM ambayo wanaiita ya ‘kidikteta’, wakati siyo kweli.
Pengine walitaka kutumia hiyo kama njia ya kutafuta huruma ya Watanzania ili wawaunge mkono watakapoanzisha operesheni yao baada ya ‘ukuta wao kubomoka’. Hakuna anayejua.
Kwa kuwa hakuna anayejua kilichomo katika mkakati wa Operesheni Kata Funua zaidi ya Ben Saanane mwenyewe na viongozi wa juu wa Chadema, basi ni vigumu kueleza kama hata kutoweka kwake ilikuwa sehemu ya kufanikisha mkakati huo ama ndio ufunguo wa kuanzisha operesheni hiyo. Hakuna ajuaye.
Yanasemwa mengi kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari. Lakini mdau mmoja alitoa maoni kupitia JamiiForums, ambayo yanamtaja moja kwa moja Mbowe, kwamba anahusika na ndiye aliyefanikisha ‘mapumziko’ ya Ben Saanane huko Afrika Kusini.
Soma mwenyewe, halafu pima, tafakari na utapata jibu halisi;
Wadau, amani iwe kwenu.
Nawapa pole ndugu wa Ben Saanane hususan Baba yake mpendwa, Focus Saanane na mdogo wake Erasto Saanane ambao kwa zaidi ya wiki sasa wanahangaika kumtafuta mpendwa wao Bernard Rabiu Saanane au Ben Saanane kama tulivyozoea kumuita ambaye amepotea katika mazingira ya kutatanisha. Ninasema ni mazingira ya kutatanisha kwa sababu mpaka leo hakuna anayejua ni lini BEN alipotea na katika mazingira yepi. Pia haijajulikana kama Ben amepotea ama yupo busy na majukumu ya kikazi.
Kutokana na kupotea kwa Ben Saanane, baadhi ya wafuasi wa CHADEMA wanaunyooshea vidole vya lawama uongozi wa CHADEMA hususan Mwenyekiti Freeman Mbowe. Kupitia mijadala mbalimbali wanayoanzisha hasa kwenye kurasa zao za facebook, kwa hakika nimebaini mambo yafuatayo;
1. Julai 2016, Freeman Mbowe alimteua Ben Saanane kuwa Msaidizi wake akimpa cheo cha ‘Executive Assistant’ wa Ofisi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa au kama Malisa Godlisten anavyoita Personal Assistant. Wakati huo huo, Ben Saanane alikuwa na Wadhifa wa Mkuu wa Sera na Utafiti wa CHADEMA kama Gazeti la Tanzania Daima la Desemba 10, 2016 lilivyobainisha. Kupitia nyadhifa zake hizo, Ben Saanane ameratibu na kusimamia mikakati na Operesheni kadhaa za chama ambazo ni pamoja na Mkakati wa Siri juu ya Zitto Kabwe wa mwaka 2013, Operesheni UKUTA ya Septemba 2016 na Operesheni Kata Funua ambayo utekelezaji wake haujafanyika. Kwa ujumla, Ben Saanane ni mmoja wa maafisa waandamizi wa CHADEMA ambaye amebahatika kuwa na Siri Kuu za chama. Ni katika siri hizi ndizo zilizoweka rehani maisha ya Ben Saanane.
2. Agosti Mosi 2016, Ben Saanane alipewa jukumu maalum la kumuandama Rais Magufuli kwenye mitandao ya kijamii. Lengo la jukumu hili ni kuuandaa umma uamini kuwa lolote litakalomtokea Ben, watu wataamini kuwa ni kutokana na maandiko yake kwenye mitandao ya kijamii.
3. Wiki ya pili ya Mwezi Novemba 2016, Freeman Mbowe alimuandalia Ben Saanane safari ya kwenda Nchini Afrika ya Kusini ambapo kwa mujibu wa mtu wa karibu na Ben Saanane aitwaye HILDA NEWTON, Safari hiyo ilipaswa kufanyika Novemba 19. Kabla ya safari hiyo, Ben alipewa na bosi wake (Mbowe) mapumziko ya wiki moja ili akamilishe andiko la Operesheni Kata Funua ambalo lilikuwa katika hatua ya mwisho kukamilika. Pia Mbowe alimpa maelekezo maalum Ben ya kutowasiliana na watu wengine ili apate muda wa kutosha wa kukamilisha andiko hilo. Aidha, Mbowe alimlipa Ben gharama zote za safari ambapo haikubainishwa ni kiasi gani na haijulikani alipaswa kuwa Afrika ya Kusini kwa siku ngapi na kwa majukumu yepi. Ni katika kipindi hicho ndipo ukimya wa Ben Saanane ulipoanza kuripotiwa.
4. Wakati Ben anaandaliwa kwenda Afrika ya Kusini, Mbowe na baadhi ya viongozi akiwemo John Mrema wakaandaa safari ya kwenda Uingereza. Ni ajabu kwa Mbowe kwenda Uingereza bila ya msaidizi wake wa karibu.
5. Novemba 26, 2016, Hilda Newton alijitokeza kuwajibu wale wote waliokuwa wanamtumia ujumbe kumuuliza alipo Ben Saanane. Katika ujumbe huo ambao aliandika kwenye ukurasa wake wa facebook, Hilda Newton alisema kuwa Ben Saanane yupo Afrika ya kusini na kwamba atarejea siku chache zijazo. Bado haijafahamika nani alimtuma Hilda kutoa taarifa hiyo ijapokuwa habari za chini ya kapeti zinasema kuwa ni maelekezo kutoka ngazi za juu za CHADEMA. Baadhi ya wafuasi wa CHADEMA walihoji sana andiko hilo. Familia ya Ben Saanane nayo ilishtushwa na andiko hilo kwani haiingii akilini Ben asafiri bila ya kutoa taarifa kwa familia yake.
6. Familia ya Ben imefanyamawasiliano ya mara kwa mara kwa uongozi wa CHADEMA kupitia Katibu Mkuu Vincent Mashinji. Hata hivyo, walijibiwa kuwa Ben yupo salama na anatekeleza majukumu ya kikazi. Hata hivyo, kadri ziku zilivyosonga, wasiwasi uliwajaa na ndipo Jumanne Desemba 6, 2016 walipoamua kwenda kituo cha Polisi Tabata kutoa taarifa za kupotea kwa Ben. Hadi wakati huo, chama kiliendelea kuwa na msimamo kuwa Ben yupo salama na kwamba wasiwe na wasiwasi.
7. Hadi hivi sasa, hakuna kiongozi yeyote wa CHADEMA aliyetoa taarifa rasmi kwa vyombo vya Habari juu ya ukimya wa Ben Saanane. Je ni kweli kwamba amepotea au yupo kikazi Afrika ya Kusini kama baadhi ya viongozi wa chama hicho walivyonukuliwa?
8. Mwenyekiti wa CHADEMA ambaye Ben ndiye Bosi wake Mkuu mpaka sasa hajatoa tamko lolote. Hii inatia shaka kwani inaeleweka kuwa kwa taratibu za kiofisi, mtu akikosekana kwa muda wa siku saba mfululizo bila ya taarifa zozote lazima aandikiwe barua ya kutaka kujieleza kwa nini asichukuliwe hatua. Mbowe hajafanya hivyo na hii inatujengea imani kuwa anajua nini kinaendelea. Aidha, licha ya kupata taarifa kuwa msaidizi wake amepotea, Mbowe anaendelea na ziara zake nchini Uingereza kana kwamba hakuna kilichotokea. Hajashtushwa kabisa na kupotea kwa Ben. Anajua dhahiri nini kinaendelea.
9. Jitihada za kumtafuta Ben Saanane zinafanywa na ndugu zake tu pamoja na marafiki zake wa karibu. Hii inazua mashaka mengine juu ya mfumo wa uendeshaji wa CHADEMA.
10.Gazeti la Tanzania Daima kwa mara ya kwanza limeandika taarifa juu ya kupotea kwa Ben Saanane Desemba 10, 2016. Hili ni gazeti linalomilikiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA. Ukimya wa gazeti hilo kwa hakika unazua mjadala mwingine.

Kauli tata za viongozi
Kauli za viongozi wa chama hicho – Mwanasheria Tundu Lissu na Mwenyekiti Mbowe – zinaonekana kuwa na nyufa mahali fulani na kuzidisha mashaka.
MaendeleoVijijini ina kumbukumbu kuwa, Lissu akizungumza na wanahabari Jumatano, Desemba 14, 2016 alisema kwamba mara ya mwisho kwa Ben Saanane kuwasiliana na bosi wake Mbowe ilikuwa Novemba 14, 2016.
Lakini kuna taarifa nyingine zinazoelezea kwamba, Jumanne, Novemba 15, 2016, Ben alitambulishwa Bungeni kama mgeni wa Mwenyekiti wa Chadema Taifa. Kwa maana nyingine alikuwepo ama alitakiwa kuwepo Bungeni siku hiyo.
Hii maana yake ni kwamba, Mbowe alikuwa na Ben siku hiyo huko Dodoma na inatengua kauli ya Lissu kwamba wawili hao waliwasiliana mara ya mwisho Novemba 14.

Tundu Lissu anasema:
Alhamisi Desemba 22, 2016 wakati wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa uliofanyika jijini Mbeya, hatimaye Mbowe naye akavunja ukimya, ikiwa ni siku 45 tangu Ben alipotoweka.
Mbowe alikaririwa akisema: “Mambo mengine yanapokuwa katika masuala ya kiuchunguzi siyo kila jambo litasemwa hadharani wakati wote, na tunatambua jambo hili lina hatari, linahusu maisha ya mtu, sasa siyo kila wakati kusema kuyarahisisha.

Mbowe ajitetea kuhusu kutoweka kwa Ben Saanane:

“Unaweza ukasema kumbe kwa kusema sana unawaruhusu na watesi wake pengine waweze kumtoa roho. Kwa hiyo kuna mambo mengine ni sensitive (nyeti), siyo mambo ya kuzungumza rahisi sana. Tunafanya kazi kwa njia mbalimbali kama chama cha siasa na tunakuwa waangalifu sana kuhusiana na tuseme nini kwa wakati gani na kwa taratibu gani lakini kwamba chama kinafuatilia suala hili, kinawasiliana na vyombo mbalimbali. Chama kina vyombo vyake vingine vya ndani ambavyo vinafanya jambo hili lichunguzwe kwa makini.
“Tuko hivyo na tunawahakikishia wote kwamba muda muafaka ukifika tutaweza kutoa taarifa za kina tumekwamia wapi na nini kifanyike cha ziada,” alisema Mbowe.
Hii siyo kawaida ya kiongozi huyo ambaye anafahamika kwa kuyasemea mambo mengi kila yanapotokea, hata kama yanaihusu serikali na chama tawala, CCM.
Hakuna anayejua kama Ben ametekwa, ametoweka tu, kapotea ama ‘kajiteka’ mwenyewe kwa maana ya kujificha, lakini Mbowe alithubutu kutamka kwamba, kama jambo hilo litazungumzwa sana ‘watesaji wanaweza kumdhuru’ huko aliko!
Pamoja na hayo, hakuna aliyekanusha wala kuthibitisha taarifa zilizoenea mitandaoni kwamba Ben Saanane alilipiwa nauli na gharama za matumizi ili akapumzike Afrika Kusini. Hakuna.
Tunatambua suala hilo liko kwenye uchunguzi wa vyombo vya dola, lakini kwa namna linavyoshughulikiwa na viongozi wa Chadema, ambao wanafahamika vyema kwa kauli tata za mashambulizi dhidi ya serikali, linaleta mashaka makubwa kama siyo mpango mahsusi wa kuhakikisha harakati za chama hicho zinarejea tena.

Yaliyompata Ben, yanaweza kukupata wewe
Suala la kutoweka ama kupotea kwa Ben Saanane halihitaji itikadi ya chama, dini, kabila au rangi. Hapa tunazungumzia uhai wa mtu na inaweza kuwa mimi au wewe.
Serikali kwa upande wake inawajibika kulinda usalama wa raia na mali zao kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama, lakini hakuna mtu anayeweza kuja nyumbani kuomboleza msiba kama uliyefiwa unashangilia!
Chadema hawaonyeshi kushtuka kwa kutoweka kwa Ben ambaye akiwa msaidizi wa Mbowe ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuwasiliana na kiongozi huyo kabla hajakutana na viongozi wenzake ama kutekeleza majukumu mengine ya kitaifa.
Leo hii Mbowe na Chadema wote wamekaa kimya, halafu utasemaje serikali ndiyo ina wajibu?
Ikumbukwe kwamba, si Mbowe wala Chadema waliojisumbua hata kwenda kutoa taarifa polisi kwa tukio hilo, bali walikuwa na ndugu wa Ben ambao siku 17 tangu kutoweka kwake, yaani Desemba 5, 2016, walilazimika kwenda kufungua kesi ya ‘kupotea’ kwa ndugu yao katika Kituo cha Polisi Tabata jijini Dar es Salaam Desemba 5, 2016 na kupewa RB namba TBT/RB/8150/2016, baada ya kushindwa kupata majibu mubashara kutoka kwa viongozi wa Chadema.
Nataka niwaulize viongozi wa Chadema: Kwani Ben alikuwa hatakiwi kwenye makao makuu ya Chama? Kama msaidizi wa Mwenyekiti, ndiye aliyekuwa mwandaaji wa karibu kila hotuba za Mbowe.
Kama wameshindwa kutanzua suala la kutoweka kwa Ben, nina mashaka kama Chadema wanaweza kuwa na ujasiri wa kushika dola katika miaka ya karibuni.
Pengine waseme kwamba, kutoweka kwa Ben Saanane ilikuwa ni mbinu yao nyingine ya kutafuta ‘kick ya kisiasa’ na wanajua mpango mzima.
Vinginevyo, ni hatari sana kucheza na maisha ya mtu kwa sababu ya kutimiza utashi wa kisiasa.

Comments