- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William
Lukuvi akizungumza na Wakazi wa Kikwajuni Vijibweni wilaya ya Kigamboni
alipokwenda kutatua mgogoro kati ya Mwekezaji Registered Trustees Korea Church
Mission jijini Dar es Salaam jana.
Na Munir
Shemweta
Waziri wa
Adhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William lukuvi amewaonya wenyeviti wa
Serikali za Mitaa kutojihusisha na masuala ya uuzaji ardhi katika maeneo
mbalimbali kwa kuwa hapaswi kisheria kufanya kazi hiyo.
Lukuvi
alitoa onyo hilo jana wakati alipokwenda kusuluhisha mgogoro wa ardhi kati ya
wananchi wa Kikwajuni Vijibweni maarufu kama kwa Mkorea wilayani Kigamboni mkoa
wa Dar es Salaam na Mwekezaji ‘Registered Trustee of Korea Church
Mission’ katika eneo hilo la ukubwa wa ekari 305.
Lukuvi
alisema sheria ya ardhi haisemi kama wenyeviti wa mitaa wanaruhusiwa kusimamia
uuzaji ardhi na kusisitiza kuwa wenyeviti hao hawana mamlaka ya kufanya hivyo
na mwenye jukumu la kusimamia masuala ya ardhi katika miji ni halmashauri za
mji au Manispaa.
Waziri wa
Ardhi alisema mtu yeyote atakayeuziwa ardhi kupitia wenyeviti hao wa mitaa au
mtu mwingine asiyetambuliwa kisheria basi atakuwa ameuziwa ‘bomu’ na kuwataka
wananchi kuwa makini na suala hilo na kuwashauri kabla ya kununua eneo lolote
ni vyema wakaiuliza mamlaka husika iwapo eneo husika limepangwa kwa matumizi ya
aina gani ili kuepuka kubomolewa.
‘’Ukitaka
kununua kiwanja kwanza kaulize Manispaa maana unaweza kununua eneo kumbe ni la
kuzikia kwani manispaa ndiyo inayojua kama eneo hilo ni salama’’ alisema Lukuvi
Katika
hatua nyingine, Waziri Lukuvi ametoa siku
kumi kwa halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam kufanya
uhakiki kwa wananchi wote wanaoishi eneo lenye mgogoro na Mwekezaji la Kikwajuni
Vijibweni Kigamboni maarufu kwa Mkorea ili kupata taarifa sahihi za wananchi
hao.
Aidha,
amemtaka Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Dar es Salaam Methew Mhonge kupata
nakala ya hukumu ya kesi ya wananchi hao dhidi ya Mwekezaji ‘Registered
Trustees Korea Church Mission’ inayoonesha kuwa wananchi wa eneo hilo
wameshindwa kesi na wanatakiwa kuondoka.
Maagizo
hayo ya Lukuvi yanafuatia kuelezwa na wananchi 22 wa Kikwajuni kupitia
mwakilishi wao Meja Mstaafu Peter Ismail kuwa haki haikutendeka wakati wa zoezi
la ulipaji fidia kwa wananchi wa eneo hilo jambo lililosababisha kukataa
kuchukua fidia na wengine 6 kudai nyongeza ya fidia huku wananchi 95
wakilalamika.
Meja
Mstaafu Ismail alisema, wao walichukua uamuzi wa kutokubaliana na mwekezaji
aliyetaka kuwafidia laki nne kwa ekari moja wakati wao walitaka kulipwa
shilingi milioni moja kwa ekari moja na kufafanua kuwa kilichowashangaza ni
Mwekezaji kulipa fidia mwaka 2015 wakati zoezi hilo lilitakiwa kufanyika miezi
sita baada ya Agosti 2004.
Kwa upande
wa wananchi sita wanaotaka kuongezewa fidia wananchi hao kupitia mwakilishi wao
Hamza Rashid walidai kesi yao iliamuliwa kupatiwa taarifa halisi ya uthamni na
siyo nakala kama walivyofanyiwa jambo walilolieleza kuwa halikufanyika.
Kufuatia
hali hiyo, Waziri Lukuvi aliagiza taarifa zote muhimu zipatikane kipindi cha
siku kumi ikiwemo Mwekezaji kuwasilisha mpango wa jinsi atakavyolitumia eneo
hilo la ekari 305 sambamba na chanzo cha mtaji wa uwekezaji huo.
Eneo la
Kikwajuni Vijibweni maarufu kwa Mkorea kwa muda mrefu tangu mwaka 2004 limekuwa
na mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa eneo hilo na Mwekezaji ‘Registered
Trustees Korea Church Mission’ anayetaka kujenga chuo Kikuu.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William
Lukuvi akitembea kuelekea eneo lenye mgogoro kati ya Wananchi wa Mkwajuni
Vijibweni wilaya ya Kigamboni maarufu kama kwa Mkorea na Mwekezaji wakati
alipokwenda kutatua mgogoro katika eneo hilo jana.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William
Lukuvi akimsikiliza mwananchi wa Mkwajuni Vijibweni Mariam Kange
alipokwenda kuatatua mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa eneo hilo maarufu
kwa Mkorea na Mwekezaji Registered Trustees Korea Church Mission (PICHA NA
WIZARA YA ARDHI)
Comments
Post a Comment