- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip
Mpango (Mb) kushoto, akiwa pamoja na Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la
Japani-JICA, Bw. Hiroshi Kato, walipokutana na kufanya mazungumzo kwenye Ofisi
za ubalozi wa Tanzania mjini Washington DC-Marekani, kando ya Mikutano ya
Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la KImataifa-IMF
Na Benny Mwaipaja, WFM
Washington D.C
Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la
Kimataifa-JICA inakusudia kuipatia Tanzania mkopo nafuu pamoja na ruzuku wenye
thamani ya zaidi ya dola milioni 345 za Marekani, sawa na takriban shilingi
bilioni 794, kwa ajili ya kutekeleza miradi mitatu ya maendeleo ikiwemo
ukarabati wa barabara ya Arusha hadi Holili, ukarabati wa Bandari ya Kigoma na
Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Visiwani Zanzibar.
Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Shirika la
Maendeleo la JICA anayesimamia Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara Bw.
Hiroshi Kato, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango,
Dkt. Philip Mpango, Mjini Washington D.C nchini Marekani.
Ameitaja miradi hiyo iliyoko mezani kwao inayosubiri
kupatiwa fedha wakati wowote kuanzia sasa kuwa ni mradi wa ukarabati wa
barabara ya Arusha-Holili utakaopatiwa mkopo wa dola milioni 221, Mradi wa maji
safi na usafi wa mazingira Zanzibar utakaopatiwa fedha kupitia mkopo wa dola
milioni 99 na mradi wa upanuzi wa Bandari ya Kigoma ambao Japan itatoa ruzuku
ya dola za Marekani milioni 25.
Bw. Kato amesema kuwa Japan inajivunia ushrikiano wa muda
mrefu kati yake na Tanzania na kwamba iko tayari kusaidia juhudi za Serikali ya
Awamu ya Tano za kuwaletea wananchi wake maendeleo na kuitaka Serikali
kuwasilisha miradi yake ya kimkakati ambayo Japan itafadhili kupitia mikopo
yenye riba nafuu pamoja na ruzuku.
Akizungumza na Mwakilishi huyo wa Japan katika Ubalozi wa
Tanzania nchini Marekani, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameishukuru
Japan kwa uhusiano wake mzuri na Tanzania na namna inavyo isaidia nchi
kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo akitaja mmoja wa miradi hiyo kuwa ni
barabara ya juu ya kwanza nchini Tanzania
katika makutano ya Tazara Jijini Dar es Salaam, maarufu kama Daraja la
Mfugale.
Dkt. Mpango ameiomba Japan kupitia Shirika lake la JICA
kutoa ruzuku na mikopo nafuu ili kutekeleza miradi ya kimkakati ya ujenzi wa
reli ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa - SGR, Mradi wa kufua umeme wa Rufiji,
Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato mkoani Dodoma, ujenzi wa barabara za
mzunguko jijini Dodoma, ujenzi wa mtandao wa barabara, upanuzi wa bandari na
miradi mingine ya kijamii.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango anaongoza
ujumbe wa Tanzania katika mikutano ya kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la
Fedha la Kimataifa-IMF, inayofanyika mjini Washington DC nchini Marekani,
ambapo ametumia fursa hiyo kukutana na wadau wa maendeleo kupenyeza ajenda za
maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Philip Mpango (Mb) kushoto, akiwa pamoja na Makamu wa Rais wa Shirika la
Maendeleo la Japani-JICA, Bw. Hiroshi Kato, walipokutana na kufanya mazungumzo
kwenye Ofisi za ubalozi wa Tanzania mjini Washington DC-Marekani, kando ya
Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF,
ambapo JICA imeahidi kutoa ruzuku na mikopo yenye masharti nafuu ili kutekeleza
miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania
(Picha na Benny Mwaipaja, WFM-Washington
DC)
Comments
Post a Comment