- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA ALOYCE NDELEIO
WATAALAM mbalimbali wa masuala ya afya mara kwa mara
wanashauri watu wawe wanafanya mazoezi ikiwa ni njia ya kuweka afya zao sawa,
pia hushauri kuwa mazoezi ni tiba kwa baadhi ya dosari zinazotokeza mwilini.
Hata hivyo fikra
nyingine ni kuwa mazoezi husaidia kunyoosha viungo na kutoa jasho pamoja na
kupunguza uzito lakini wataalamu wanabainisha kuwa mazoezi ni lishe kwa ubongo
kwani huuongezea kumbukumbu.
Mara nyingi baadhi ya watu hufikiria jinsi ubongo wa
mwanadamu utakavyokuwa pindi atakapofikia uzeeni katika dhana kuwa atasahau
baadhi ya mambo na hususani yale ambayo yatakuwa hakuyaandika kwenye vitabu vya
kumbukumbu za kila siku ili aweze kuyarejea.
Hali hiyo inatokana na ukweli kuwa uwezo wa ubongo wa
binadamu unapungua kadri mtu mwenyewe anavyozeeka na hivyo kupoteza kumbukumbu
au kuwa msahaulifu.
Hali hiyo inasababisha ashindwe kufanya maamuzi sahihi na
mara nyingi hufikia hatua ya kushindwa kuzungumza na baadhi huzungumza kwa
kurudia rudia baadhi ya maneno.
Hali ya aina hiyo imekuwa inawaogopesha baadhi ya watu na
hivyo kuwafanya wawe wanakuwa makini kwa
kuchukua tahadhari za mara kwa mara.
Hilo linawezekana kwa kuandika kumbukumbu zao kwenye
vitabu vya kumbukumbu, jambo ambalo ni zuri, na linaweza kuwanufaisha watu
walio karibu nao iwapo kwa bahati mbaya watakuwa hawawezi kuzungumza au
kutambua baadhi ya mambo.
Mara nyingine hutumika kama ushahidi wa kuondoa utata
unaoweza kutokeza miongoni mwa ndugu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni iliyochapishwa
kwenye gazeti la Washington Post nchini Marekani inadokezwa kuwa zipo njia
ambazo mtu anaweza kutumia ili aweze kulinda uwezo wa ubongo wake, hali
kadhalika kuulinda dhidi ya magonjwa.
Gazeti hilo linaarifu kuwa njia pekee itakayowezesha hali
hiyo kuwepo ni kutoa changamoto kwa ubongo kwa kufanya mazoezi mara kwa mara.
Kwa mujibu wa utafiti mkubwa ulioendeshwa kwa mwezi mmoja
kupitia takwimu za kisayansi zilizochapishwa kwenye mtandao zilibainisha kuwa
kufanya mazoezi kwa wingi kunapunguza hatari ya kukabiliwa na magonjwa ya moyo,
pia ni miongoni mwa njia maridhawa za kuuweka ubongo katika hali nzuri ya
kiafya.
Aidha, kwa mujibu wa utafiti
wa Taasisi ya Taifa ya Afya ya Marekani inabainishwa kuwa shughuli nyingi
zinazotumia ubongo katika maisha ya mtu huufanya ubongo ushindwe kuhifadhi
uwezo wake wa kumbukumbu.
Kutokana na utafiti huo mwandishi wa Uingereza, Margaret
McCartney ambaye anauunga mkono anadokeza hali ya aina hiyo kufuatana na
utafiti uliofanywa na Profesa Ian Robertson wa Idara ya Saikolojia katika Chuo
cha Trinity mjini Dublin.
Akihadhiri katika tamasha la sayansi la Chama cha
Maendeleo ya Sayansi nchini Uingereza, Profesa Robertson alisema kuwa hali hiyo
sio tu kwamba mazoezi yanaboresha umri wa ubongo lakini mlo anaotumia mtu,
mazoezi, chemsha bongo na majaribio ya
kuushughulisha ni miongoni mwa vigezo vinavyochangia.
Hali hiyo inawezesha kutambua kuwa ubongo unaweza ukawa
na afya nzuri na hivyo kumwezesha mtu kufurahia maisha katika ngwe inayoanzia
miaka 50 hadi 80.
McCathney anasema kuwa watafiti wapo kwenye harakati za
utafiti unaohusu tiba ya kuzeeka, lakini habari nzuri ni kuwa kama mtu
amebahatika kupata elimu, na anafanya kazi zinazomfanya awajibike kwa kutumia
ubongo zaidi katika kufikiria masuala ya kazi, basi anakuwa kwenye nafasi nzuri
ya kurefusha uwezo wa ubongo wake katika kuhifadhi kumbukumbu.
Anasema kuwa kwa mujibu wa utafiti wa Profesa Robertson
upo uthibitisho wa kuwepo uhusiano kati ya kiwango cha elimu na kushuka kwa
uwezo wa ubongo katika kuhifadhi kumbukumbu.
Kiwango cha elimu kina uhusiano na kuongezeka kwa
muunganiko wa mawasiliano katika seli za ubongo.
Kwa mujibu wa gazeti la Washington Post, Chama cha
Wataalamu wa Masuala ya Ubongo cha Marekani kinadai kuwa watu ambao mara kwa
mara huwa wanafanya shughuli zinazohusisha kufikiri kama vile kusoma magazeti
kila siku, au kutembelea sehemu za makumbusho, pamoja na sehemu nyingine ambazo
ni tofauti na mazingira yake ambayo yanakuwa yamemjengea mtu taswira mgando
kwenye ubongo huchangamka kimawazo.
Kutokana na hali hiyo ni kwamba kubadilisha mazingira au
kusoma mambo au matukio mapya katika magazeti huingiza jambo jipya katika
ubongo na hivyo kulazimika kufikiri au kutambua hali ambayo humfanya mtu awe na
afya njema.
Gazeti hilo linaripoti kuwa hali hiyo imekuwepo baada ya
utafiti wa Profesa Robertson kuendeshwa
au kufanyika miongoni mwa watu 1700 kwa kipindi cha miaka sita.
Hali kadhalika watafiti walibaini kuwa watu wanaofanya
mazoezi angalau mara tatu kwa wiki ni mara chache sana wanaweza kukumbwa na
tatizo la kiharusi.
Katika nadharia moja ambayo ililenga utafiti wa wanyama
uliweza kuleta matokeo yaliyobainisha kuwa mazoezi ya mwili yanaboresha
mtiririko wa damu mwilini na kiwango cha hewa ya oksijeni kinachopokelewa
kwenye ubongo.
Hali kadhalika mazoezi hayo yanaweza kuuongezea ubongo
uwezo mwingine wa ziada ambao ni kuboresha kukua kwa tishu na chembe chembe za
damu katika sehemu ya ubongo inayohusika na kuhifadhi kumbukumbu.
Kuhusu changamoto ambayo inatolewa kwa ubongo kwa mtu
ambaye anafanya mazoezi, kwa mujibu wa majaribio yaliyofanywa nchini Marekani
katika Chuo Kikuu cha John Hopkins cha Baltmore unaonesha kuwa hali hiyo
inaweza kuboresha maisha ya watu walio na umri mkubwa na hususani wastaafu.
Watafiti hao ambao walilifanyia majaribio kundi moja
la wazee ambao mara nyingi huwa
wanaonekana kama watu waliotengwa kijamii hususani kwa utamaduni wa nchi za
magharibi ambako familia hazina mshikamano kama zilivyo familia za nchi maskini
hasa Afrika.
Waliwafanyia mazoezi katika suala zima la kusoma ili
kuushughulisha ubongo ambapo baadaye walizinduka na kuwa wasaidizi wa kujitolea
kwa kufanya shughuli mbalimbali za kujitolea katika mashule.
Aidha, watafiti
walipofuatilia ili kuangalia maendeleo yao baada ya kipindi cha miezi sita
walibaini kuwa si tu kwamba uwezo wao wa kufikiri ulikuwa umeongezeka bali pia
walikuwa wanaweza kutembea kwa haraka, na walikuwa tayari wameshapanua
mawasiliano na jamii iliyokuwa inawazunguka.
Kutokana na hali hiyo inakuwa ni vigumu kupingana na
wataalamu ambao kwa kiasi kikubwa wameweza kubaini kuwa sayansi si suluhisho la
mwisho bali ni sehemu ya chachu ya kupanua uwanja wa kuelewa.
Hivyo ni muhimu na ni wazo mwafaka kufanya mazoezi ambayo
kwa upande mmoja yanaboresha afya ya mwili na kwa upande mwingine yanakuwa ni
lishe ya ubongo, hivyo kuboresha au kuufanya uwezo wa kuhifadhi kumbukumbu kuwa
mkubwa.
Katika mazingira ya jamii kama Tanzania wapo wanaoamini
au wanaochukulia kuwa wanaofanya mazoezi ama ya mbio nyepesi au yoyote yale
ambayo hayako kwenye orodha ya mashindano kuwa wanapoteza muda.
Hali kadhalika imejengeka dhana kuwa kutembelea maeneo
mbalimbali tofauti na mazingira waliyozoea kama vile kutalii hilo linaonekana
kuwa ni kwa ajili ya watalii kutoka nje.
Dhana potovu hiyo kwa kuwa yanayoonekana kwa kufanya
utalii huo wa ndani huondoa mgando wa uelewa na kupata taswira mpya ndani ya
ubongo.
Hata hivyo, ukweli unabakia kuwa kufanya hivyo ni kuutafutia ubongo
lishe ambayo itauwezesha kukuza uwezo wake wa kumbukumbu.
Hali hiyo pia hupunguza kwa kiwango kikubwa utegemezi na
upweke ambao unaweza kumkumba mtu anapofikia kwenye umri mkubwa na ndio maana
inashauriwa na kuwepo kauli mbiu mara kwa mara ya ‘Fanya Mazoezi kwa Afya’.
CHANZO: TANZANIA
Comments
Post a Comment