Featured Post

WATAFITI WABAINI MAKASHA YA RISASI ZA MJERUMANI KILOLO



HISTORIA kuhusu Chifu Mkwawa kuandikwa upya baada ya watafiti wa mambo ya kale kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuvumbua ushahidi wa makasha ya risasi eneo la Lugalo wilayani Kilolo mkoani Iringa.
Mtafiti wa mambo ya kale, Dkt. Frank Masele, amesema katika utafiti wao wamegundua makasha ya risasi kwenye Kijiji cha Lugalo kwenye maadhimisho ya miaka 127 ya Vita ya Mkwawa dhidi ya Wajerumani.

Katika vita hiyo iliyopiganwa Agosti 17, 1891 Mkwawa alifanikiwa kuwaua askari wapatao 300 pamoja na kiongozi wao Emil Von Zelewisky ambapo baada ya kushindwa vita hiyo Wajerumani walikwenda kujipanga upya namna ya kumkabili Mkwawa.
Dkt. Masele amesema kuwapo kwa mabaki mengi ya maganda ya risasi katika eneo hilo la Lugalo kunaonesha kulikuwa na mapambano makali ya kivita ambapo licha ya majeshi kutumia silaha za jadi kama mikuki bado waliwashinda Wajerumani ambao walikuwa wakitumia silaha kali za kivita.
Hili ndilo Kaburi maarufu la Nyundo walikozikwa makamanda wote wa Kijerumani waliouawa na Mkwawa mwaka 1891 Lugalo

 “Leo tupo hapa kuendelea na utafiti wetu eneo la Lugalo, tumekuja kutafuta ushahidi, na kwa bahati nzuri tumepata maganda ya risasi zilizotumiwa na Mjerumani na huu ndio ushahidi pekee, Mkwawa alitumia mkuki na Mjerumani alitumia silaha hizi kali na katika harakati za kuikomboa nchi yetu hatuwezi kukwepa kijiji hiki cha Lugalo na ndio maana nimekuja na wanafunzi wangu 49 ili wajifunze kwa vitendo zaidi,” alisema Dkt. Masele.
Naye Fatuma Mkwawa ambaye ni dada wa Chifu Mkwawa aliiomba serikali kuweka kumbukumbu nzuri kwa kujenga mnara au sanamu ya Mkwawa mwenyewe jambo ambalo familia itapendezwa zaidi kumuenzi kuliko hayo makaburi ambayo yanaonesha bado wanaendelea kuwatukuza Wajerumani.
Awali akizungumza, Mzee Alfred Mnyagala ambaye alizaliwa mwaka 1910 kijijini hapo na kupigana Vita ya Pili ya Dunia, alisema duniani hakuna sehemu Wajerumani walikopigwa kama Iringa na walivyorudi kwa mara ya pili kwa lengo la kuteketeza ngome ya Mkwawa walipitia Kata ya Lulanga, Nguluhe, Tosamaganga hadi Kalenga na walimkuta Mkwawa ameshajimaliza mwenye kabla ya kukamatwa na Wajerumani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah, na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, kwa pamoja wamesema wamepokea maombi yaliyotolewa na mwanafamilia huyo kuhusu kuendeleza eneo hilo kwa kuwa Mkoa wa Iringa uliteuliwa kuwa kitovu cha utalii.
Abdallah alisema kuwa katika kukuza utalii wa Kusini mwa Tanzania ni lazima kuviibua na kuvitangaza vivutio vyote vya kiutamaduni pamoja na hifadhi za taifa ili viweze kutangazwa kwa lengo la kuwanufaisha wananchi, kuingizia taifa fedha za kigeni, kuongeza ajira kwa vijana pamoja na kuwafundisha watoto historia ya vivutio hivyo kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadaye.
Katika maadhimisho hayo ambayo yamefanyika kwa mara ya kwanza serikali za wilaya zote mbili zimepokea matokeo ya awali ya watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Ikiolojia na Taaluma za Urithi wa Utamaduni na pia Abdallah alisisitiza dhamira ya serikali kuboresha kaburi hilo linalofahamika kama Kaburi la Nyundo ili kuwavutia watalii wengi zaidi na kuongeza pato la Mkoa wa Iringa.


Comments