- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA MWANDISHI WETU
Mkataba wa Cartagena uliandaliwa mahsusi ukilenga kuhifadhi
mazingira kwa kuzingatia usafirishaji na matumizi ya viumbe watokanao na
bioteknolojia za kisasa ambazo zinaweza kuathiri afya ya binadamu.
Mkataba huo ulianza kutumika duniani tangu Septemba 11,
2003, baada ya kuridhiwa na nchi zipatazo 50 duniani kote na hadi kufikia
Novemba 2006, jumla ya nchi 116 zilikuwa zimeridhia itifaki hiyo.
Kwa ufupi ni kwamba Ibara ya 2 ya itifaki hiyo inasisitiza
haja ya nchi zilizoridhia kuandaa sheria, miongozo ya usimamizi wa usalama wa
mazingira dhidi ya athari za baiotekinolojia ya kisasa.
Aidha uandaaji wa mwongozo kuhusu usimamizi wa bidhaa ambazo
zimefanyiwa mabadiliko ya vinasaba, ikizingatia usalama wa afya za binadamu,
mazingira pamoja na bioanuai ni jambo jingine linalotiliwa mkazo na ibara hiyo.
Katika mazingira hayo kampeni za uhusiano wa mashirika ya
kimataifa ni za kijani na kampuni kubwa, kuanzia zile zinazozalisha vinywaji
hadi magari, zinawashawishi wanaharakati kuwa zinafanya jitihada za kulinda
mazingira kutokana na kuongezeka kwa joto duniani na kupotea kwa bioanuai.
Lakini kampuni hizi zinachokifanya ni suala jingine na tofauti.
Suala hilo lilibainika katika mkutano wa tano wa pande
zinazohusika katika Itifaki ya Usalama wa Bioanuai uliofanyika Bonn miaka ya
hivi karibuni.
Kampuni nyingi zinazotengeneza kemikali aidha zinajaribu
kugomea taratibu kali za kimataifa za kudhibiti viumbe waliozalishwa katika
maabara, au wanapuuzia sheria za hati miliki ili kufaidika na maarifa ya jadi
katika nchi zinazoendelea.
Mmea wa Umckaloabo (Pelargonium sidoides) au unaojulikana
kwa jina la Geranium nchini Afrika Kusini ndiyo unaochukuliwa mfano mkubwa.
Serikali ya Afrika Kusini, Kituo cha Afrika cha Kusimamia
Bioanuai (ACB) na Azimio la Berne, asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Uswisi,
wote wanasema kuwa mmea huo umekuwa ukitumiwa katika dawa za jadi kwa karne
dhidi ya magonjwa ya mapafu.
Lakini katika miaka ya hivi karibuni, mmea huo umekuwa wa
kibiashara katika kampuni ya dawa ya Kijerumani ya Spitzner, kwa kudai kuwa
matumizi ya Umckaloabo yamejulikana barani Ulaya tangu mwaka 1935.
Spitzner pia inauza dawa za Ukimwi zinazotokana na
Umckaloabo. Waafrika wanasema dawa hizo za Kijerumani siyo halali kwa sababu
zinatokana na asili ya kinasaba na maarifa asilia kutoka kusini mwa Afrika.
Lakini kwa upande wa Tanzania zipo sababu mbalimbali
zilizoisukuma kuridhia makubaliano hayo ya Cartagena Machi 2003.
Mojawapo ya sababu hizo ni kuwa na uwezo wa kuchukua hatua
madhubuti na za haraka katika kudhibiti athari zitokanazo na matumizi ya viumbe
na bidhaa zinazozalishwa kwa bioteknolojia ya kisasa na hivyo kuepusha Tanzania
kuwa jalala la bidhaa zilizokataliwa katika nchi zingine.
Vilevile kuiwezesha nchi kuharakisha upashanaji habari juu
ya kudhibiti matumizi holela ya mazao yatokanayo na bioteknolojia pamoja na
kukuza ushirikiano na nchi nyingine ili kuweka mfumo wa kudhibiti athari
zitokanazo na hali hiyo.
Biotekinolojia ya kisasa inawezesha uhamishaji wa viini tete
vya uhai kutoka kiumbe kimoja kwenda kingine, ambapo viini vya samaki vinaweza
kuhamishiwa hata kwenye mimea na wanyama.
Ili kukidhi haja mbalimbali kama vile kuimarisha ubora,
kudhibiti magonjwa, kuhimili ukame na kukuza uzalishaji, matumizi ya
biotekinolojia yamekuwepo duniani takribani kwa kipindi cha miaka 30 iliyopita
bila utaratibu wa kimataifa wa kutathimini athari zinazoweza kusababishwa na
matumizi au uendelezaji wake.
Mfano, mojawapo ya bioteknolojia ya kisasa ambayo ina
uwezekano wa kushamiri kwa kasi ulimwenguni, ni ‘Terminator Technology’, aina
ya teknolojia inayohusisha uzalishaji za mbegu zenye vinasaba vitokanavyo na
mabadiliko ya kisayansi.
Hii ni teknolojia iliyojaa ukiritimba kwani inafanya mkulima
kuwa tegemezi wa maghala ya mbegu za wazalishaji wenye teknolojia hiyo, hali
kadhalika inaua mfumo wa asili wa upatikanaji wa mbegu.
Aidha inashawishika kuamini kuwa wataalamu wa mazingira
anuai wanaihofia teknolojia hii kuwa inaweza kusababisha hata upungufu wa
chakula, na hivyo uchumi wa nchi kuyumba hususani katika sekta ya kilimo.
Aidha inaeleweka wazi kuwa bioteknolojia ni moja ya vitu
vyenye uwezo wa kuchangia katika maendeleo ya nchi, hususani katika sekta ya
kilimo, uzalishaji viwandani na hifadhi ya mazingira iwapo itatumika vizuri,
ikiwa na maana ya kuwepo na udhibiti wa kitaalamu.
Kwa kuzingatia athari zinazotokana na bioteknolojia ya
kisasa, sheria ya usimamizi wa mazingira namba 20 ya mwaka 2004 ambayo pamoja
na mambo mengine ina kifungu kinachoruhusu usalama wa mazingira dhidi ya athari
zitokanazo na aina hiyo ya teknolojia.
Tayari Umoja wa Ulaya una sheria kali dhidi ya bidhaa
zitokanazo na mabadiliko ya kinasaba (GMOs), jambo ambalo limefanya bidhaa
chache sana ndizo zikubalike kibiashara ndani ya umoja huo.
Kutokana na hali hiyo, hakuna kampuni inayoruhusiwa kufanya
biashara ya aina hiyo mpaka itoe uhakika wa usalama wake dhidi ya afya ya
binadamu, mazingira na bioanuai.
Nchi za India, Asia na China ni moja ya wazalishaji wa pamba
iliyofanyiwa mabadiliko ya vinasaba, lakini pamoja na hayo nchi hizo zimeweka
sheria, miongozo na mifumo inayosimamiwa na wataalamu waliobobea katika fani
hii pamoja na vifaa vya kutosha.
Kutokana na hali hiyo nchi hizo zinaweza kuokoka dhidi ya
hatari zinazotokana na teknolojia hiyo na hivyo kufanya mzigo kuzielemea ambazo
hazijabobea katika teknolojia hiyo ya kisasa ulimwenguni.
Hata hivyo, hatari iliyopo kwa nchi kama Tanzania ni
upungufu wa elimu juu ya bioteknolojia sambamba na wataalamu waliobobea katika
taaluma hiyo.
Kutokana na utafiti uliofanywa mwaka 2004 (Kenti 2004)
umeonesha hali hiyo wazi kuwa nchi 48 kati ya 53 ndani ya Afrika, Tanzania
ikiwemo, hazina sheria hizo maalumu kama zilivyozitaja hapo awali.
Changamoto iliyopo mbele ya wataalamu wetu ni kuhakikisha
inawekwa sheria na mifumo mizuri ya kukabiliana na hali hiyo, kama ambavyo
baadhi ya nchi jirani zimekwishafanya katika kukabiliana na bioteknolojia ya
kisasa.
Katika Afrika Mashariki, Kenya na Uganda tayari zinaendesha
majaribio ya bidhaa ambazo vinasaba vyake vimefanyiwa mabadiliko ya vinasaba.
Kenya yenyewe inatafiti zaidi katika zao la mahindi, pamba
na viazi wakati Uganda ikiendesha utafiti wa ndizi na hali kadhalika Tanzania.
Hofu iliyopo inatokana na kuwepo kwa mianya katika mipaka ya
nchi wakati wa kupitisha bidhaa, kuwa
aina hiyo ya bidhaa zitokanazo na bioteknolojia zinaweza kuingia nchini kupitia
bandarini kwenda nchi jirani kama msaada.
Haya yote yakiwa yanaendelea, mwaka 2001/02 Tanzania
iliendesha utafiti wa tumbaku ambayo imefanyiwa mabadiliko ya kinasaba mkoani
Kilimanjaro kupitia Taasisi ya Utafiti ya TPRI, kwa niaba ya Wizara ya Kilimo
na Chakula.
Jambo la kusikitisha, majaribio hayo yalisitishwa kutokana
na ukweli kwamba kulikuwa hakuna sheria, mwongozo wala mfumo na kanuni kuhusu
usimamizi wa usalama wa mazingira dhidi ya athari zinazotokana na
biotekinolojia ya kisasa.
Aidha, utafiti uliofanywa hivi karibuni na Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, umeonesha kuwepo kwa mbegu za mahindi kutoka aina ya
Monsanto-MON 810- Yieldgard Maize iliyofanyiwa mabadiliko ya kijenetiki.
Swali ni je, Tanzania itaokokaje na tatizo hili kama tayari
imepokea mfumo wa utandawazi na hivyo kulazimika kukubali uingizwaji na
upitishwaji bandarini mazao mbalimbali ya biotekinolojia ya kisasa kwenda nchi
jirani?
Ukwepaji wa athari hizo hauepukiki, kwani tayari Kenya,
Uganda, Zimbabwe na Zambia zimeingiza mifumo hii nchini mwao ambapo itakumbukwa
kuwa hivi karibuni Zimbabwe na Zambia ziliingiza nchini mwao mahindi
yaliyozalishwa kwa teknolojia hiyo kama msaada wa chakula kutoka Marekani.
Ni kutokana na hilo, ipo haja kwa serikali kuendesha
majaribio ya bidhaa zinazoweza kuzalishwa na mifumo ya teknolojia hii jambo
ambalo ni hatari kwa ustawi wa Tanzania isiyo na mawaa.
Mfumo wa usimamizi wa usalama wa mazingira dhidi ya athari
za biotekinolojia ya kisasa unahusisha baadhi ya vyombo na idara muhimu za
serikali, ambazo bila shaka wapo wanamazingira mbalimbali ndani yake.
Idara hizo ni Ofisi ya Uratibu ambayo ina dhamana ya
mazingira ndani ya ofisi ya Makamu wa Rais, pamoja na mamlaka lengwa ambazo ni
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
Zingine ni pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, Fedha
(TRA), Ardhi, Nyumba na Makazi, Maji, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Viwanda,
Biashara na Masoko, Afya na Ustawi wa Jamii, Maliasili na Utalii, Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Sheria na Katiba, Ujenzi na Uchukuzi.
Ikumbukwe kuwa kuwepo kwa miongozo na mifumo maalumu juu ya
suala hili, itasaidia masuala mengi ikiwa ni pamoja na kuongeza weledi na
wataalamu bobezi katika taaluma ya biotekinolojia ya kisasa.
Ni kutokana na Itifaki ya Cartagena na umakini wa Tanzania,
unaweza kuziepuka athari kama vile saratani, usugu wa dawa kwa matibabu ya
magonjwa, athari mbalimbali za kiafya na kujitokeza kwa magugu na spishu ngeni
vamizi.




Comments
Post a Comment