- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Mmoja wa abiria akikaguliwa na mashine ya
mkono, iliyoshikwa na Ofisa Afya wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe, Peter
Maseke, ikiwa ni moja ya njia za kudhibiti wagonjwa wa Ebola wasiingie nchini.
Ugonjwa huo umetangazwa hivi karibuni kusambaa nchini Kongo.
Ofisa Afya wa Kiwanja cha Ndege
cha Songwe, Bw. Peter Maseke (katikati) akikagua hati za kusafiria za mmoja wa
abiria aliyekuwa akisafiri kuelekea Dar es Salaam, ambapo (kulia) ni mashine
maalum inayotambua abiria wenye homa kali, ambayo ni moja ya dalili za ugonjwa
wa Ebola.
Abiria wakiwa katika eneo la nje
la kuondoka kwenye Kiwanja cha Ndege cha Songwe
Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa Viwanja vya Ndege vya Songwe na Kigoma,
umejiandaa kwa kushirikiana na maafisa afya, kuhakikisha hakuna mgonjwa mwenye
dalili za Ebola anaingia nchini, akitokea maeneo ya Tunduma na nchini Burundi.
Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe, Pius Kazeze
alimwambia Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),
Bi.Bahati Mollel kwa njia ya simu kuwa, tayari Maafisa wa Afya wameshafunga
mashine maalum (thermo scanners) inayotambua joto la mwili la abiria ambaye
anasafiri kwa kupitia kiwanja hicho, na likizidi 38 anatakiwa kutoa taarifa za
afya yake.
Kazeze amesema Kiwanja cha Songwe ni tofauti kidogo na
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ambapo zaidi
wanakagua abiria wanaoondoka kwa kuwa wengi wanatoka mpakani maeneo ya Tunduma
na kwenda maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
“Tayari maafisa Afya wamefunga mashine ya ukaguzi wa afya
eneo la nje la kuondokea abiria kwani kwetu huku tunapata abiria wengi
wanaotoka nchi jirani wanaopitia mpakani Tunduma, hivyo wengi wao wanatoka nchi
zinazopakana na Kongo, ambayo inasadikika ugonjwa wa Ebola umeibuka kwa kasi
kubwa,” alisema Kazeze.
Hatahivyo, amesema mbali na mashine hiyo kubwa iliyowekwa
sehemu maalum, pia wanamashine mbili ndogo zinazotumiwa kwa kushikwa mkononi na
maafisa Afya, lakini wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa Watumishi wa afya,
ambao tayari wameshaomba kuongezewa mmoja ili kufanikisha kazi hiyo kuwa
rahisi.
Naye Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma, Bw. Theophan
Bileha amesema wapo mbioni kiweka kifaa hicho kwa kuwa wanatarajia abiria
kutoka Burundi watakaowasili kwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL),
itakayoanza safari zake kuanzia Agosti 30, 2018.
“Tumeshafanya kikao na wenzetu wa Afya, na wameahidi kuleta
mashine mojawapo, tunatarajia abiria wanaotoka Bujumbura, kwani tumeambiwa ATCL
itaanza kwenda huko kuanzia tarehe 30, na hawa wapo watakaoshuka hapa na
wengine wanakwenda kwenye viwanja vingine kulingana na ratiba ya ndege hii,”
alisema Bw. Bileha.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kigoma, Dk. Peter
Nsanya amesema mashine hiyo itawekwa kiwanjani hapo kwa kipindi, ambacho ndege
zinatua na baada ya ratiba za ndege kumalizika, wanahamishia eneo la Bandarini
kwa kuwa pia kuna abiria wanaotoka maeneo mbalimbali.
“Sisi tumejipanga kukabiliana na maradhi haya ikiwa na
kuhakikisha hatutaruhusu uingie nchini, na ndio maana tunaratiba za ndege,
ambapo tutakuwa tunakwenda kutoa huduma, na baadaye kuhamia bandarini,”
amesema.
Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, Mohamed Maulid
amesema wamejiandaa kwa kushirikiana na Maafisa Afya wamekuwa wakitumia mashine
ya mkono kwa ukaguzi wa abiria wanaotoka nchi za Uganda, Nairobi na Kongo.
Ugonjwa wa Ebola unaosambazwa kwa virusi vya Ebola,
husababisha homa kali inayoweza kuambatana na kutokwa damu mdomoni, puani,
masikioni, machoni na sehemu nyingine za wazi na unaenea kwa haraka. Hivi
karibuni umetangazwa kutokea nchini
Kongo na kusababisha vifo.
Dalili za Ebola ni pamoja na homa kali, maumivu ya kichwa na
misuli, mwili kulegea, kutapika, kuharisha, vipele na kutokwa damu.
Juzi Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNIA) kilitangaza kuchukua hatua kali za kuweka zuio kwa abiria wanaongia
nchini kupitia Kiwanja hicho, ambapo kumefungwa vifaa ambavyo vinabaini joto la
abiria na endapo litazidi nyuzi joto 38, atatakiwa kutoa maelezo zaidi ya
maisha yake.
Pia abiria wote wanaowasili kwa ndege zinazotoka nchi jirani
na Kongo wanatakiwa kupitia eneo maalum ambalo hutakiwa kunawa mikono yao kwa
dawa maalum ili kuua vijidudu mbalimbali.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO CHA
MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA (TAA)



Comments
Post a Comment