- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii,
jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu akisisitiza jambo wakati wa uwasilishwaji
wa taarifa ya uendeshaji wa hospitali za rufaa za mikoa mbele ya kamati ya
kudumu ya bunge ya huduma na maendeleo ya jamii jijini Dodoma.
Naibu waziri wa Afya, maendeleo ya jamii,
jinsia, wazee na watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiwasilisha ripoti ya
uendeshaji wa Hospitali za rufaa za mikoa mbele ya wajumbe wa kamati ya kudumu
ya bunge huduma na maendeleo ya jamii jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge
ya huduma na maendeleo ya jamii Mhe.
Peter Selukamba akitoa neno wakati wa kuwasilisha kwa taarifa za
uendeshaji wa hospitali za rufaa za mikoa kutoka wizara ya afya, maendeleo ya
jamii, jinsia, wazee na watoto jijini Dodoma.
Wajumbe wakifuatilia mjadala uliokua
unaendelea katika kikao cha mawasilisho ya taarifa za uendeshaji wa Hospitali
za rufaa za mikoa kutoka wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na
watoto katika kamati ya kudumu ya Huduma na maendeleo ya jamii jijini Dodoma.
Na WAMJW-Dodoma
SERIKALI imetenga shilingi bilioni 30 kwa ajili ya
kujenga na kukarabati miundombinu ya
hospitali zaRufaa za Mikoa kila
mkoa ili kuweza kuwawezesha wananchi
kupata huduma za rufaa za kibingwa karibu na wanapoishi na hivyo kupunguza adha
ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati akiwasilisha taarifa za uendeshaji wa hospitali za rufaa
za Mkoa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii jijini
Dodoma.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa
fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha hospitali za Rufaa za
Mikoa ya Geita, Katavi, Simiyu, Njombe na Songwe ambapo zipo katika hatua za
ujenzi wa hospitali hizo hivyo itafanya
idadi ya hospitali hizo kuwa 28 pindi zitakapokamilika.
“Serikali ilifanya mabadiliko ya kuzihamishia hospitali za
Rufaa za Mikoa Wizarani ili kuboresha
huduma za kibingwa ikiwemo kutoa fursa
nzuri ya udhibiti ,usimamizi na mgawanyo
wenye tija zaidi wa rasilimali chache zilizopo,” alisema Dkt. Ndugulile.
Alisema kuwa baada ya Wizara kukabidhiwa hospitali hizo
ilifanya tathimini ya awali ya hali
halisi na kubaini changamoto mbalimbali zilizoathiri utoaji wa huduma za
afya katika maeneo yote ambayo ni nguzo ya msingi katika kuwezesha upatikanaji wa huduma bora.
“Hospitali za Rufaa za Mikoa zinapaswa kutoa huduma za
kibingwa ambazo hazitolewi katika hospitali ngazi ya Halmashauri, Huduma za
kibingwa ambazo ni lazima kupatikana katika
hospitali za Rufaa,” alisema Naibu Waziri Dkt. Ndugulile.
Alitaja huduma za kibingwa ambazo zinatakiwa kutolewa katika
hospitali hizo za Rufaa za Mikoa ni pamoja na upasuaji wa jumla, magonjwa ya
uzazi na yanayoathiri wanawake, magonjwa ya watoto, magonjwa ya ndani, magonjwa
ya kinywa na meno na Radiolojia.
Kwa upande wa ubora wa huduma zinazotolewa Naibu Waziri huyo
alisema Wizara ilifanya kaguzi za kuzitambua hali halisi ya ubora wa huduma za
afya zinazotolewa katika hospitali hizo na jumla ya hospitali za rufaa ishirini
na moja zilifanyiwa tathmini na kupewa nyota kutokana na vigezo vilivyowekwa na
kupewa mpango kazi wa kuboresha huduma.
“Ni hospitali 9 zilipata nyota mbili, hospitali kumi na moja
zilipata nyota moja na hospitali moja ilipata nyota sifuri, hivyo hakuna
hospitali yeyote iliyopata nyota 3 hapa
nchini," alimalizia Dkt. Ndugulile.




Comments
Post a Comment