Featured Post

MKURUGENZI TIC AWAONYA MA-RC, DC WANAOTOA ADHABU KWA WAWEKEZAJI



MKURUGENZI Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geofrey Mwambe, amewataka Wakuu wa Wilaya na Mikoa nchini, kuacha mara moja kutoa adhabu, matamko mbalimbali kwa wawekezaji waliopo nchini bali waziachie mamlaka husika kufanya kazi hiyo.

Mwambe aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa akielezea mafanikio ya ziara yao ya kutafuta wawekezaji, waliyoifanya katika nchi za Korea na China, mwezi huu.
''Utakuta DC au RC anaenda kwenye ziara sehemu, anaanza kutoa maagizo ya kukamatwa mwekezaji au alipe kodi kiasi fulani,  hiyo siyo kazi yao, kuna mamlaka husika ambazo zinatakiwa kufanya kazi hiyo,” alisema.
Aliwataka viongozi hao kufuata sheria na kanuni kwani wao hawahusiki na mwekezaji au mfanyabiashara ambaye halipi kodi bali hiyo ni kazi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Wajibu wa viongozi ni kutoa taarifa kwa mamlaka husika juu ya wawekezaji wasiolipa kodi,  wanataarifa kuna mtu halipi kodi, wanatakiwa kupeleka taarifa hiyo ofisi husika na siyo kutoa matamko na vitisho.
Mkurugenzi huyo alisema, kuna viongozi wengine wanadiriki kutoa amri kiwanda fulani kifungwe au wanatoa siku kadhaa kiwe kimelipa kodi wakati hiyo si kazi yao.
“Kama mwekezaji ana tatizo wanatakiwa kutoa taarifa TIC au kwa mamlaka husika iliwe kufuatilia, kodi  inakusanywa na TRA, viongozi, tuache kila taasisi ifanye kazi yake.
“Tusiingilie majukumu ya watu wengine, kila mmoja ana lengo la kumsaidia Raisi Dkt. John Magufuli, lakini tunatakiwa kufuata utaratibu,” alisisitiza.
Alitoa wito kwa viongozi wenzake, kufuata sheria na taratibu na washirikiane  kukuza uchumi kwani Rais Dkt. Magufuli anatamani kuona Tanzania ifikapo 2025 inakuwa katika uchumi wa kati.
Katika hatua nyingine, alisema anatarakjia kumuandikia barua Kamishna Mkuu wa TRA, kwani kuna wawekezaji wamekaa miaka 7 nchini bila kulipishwa kodi badala yake wanakuja wageni wanadaiwa walipe kodi.
“Hii siyo sawa, wawekezaji hao wamekaa miaka 7 nchini, hakuna mtu wa forodha aliyeenda kudai kodi, wameondoka wamekuja wapya, wanadaiwa kodi  ya miaka saba ilioyopita,” alisema.

Comments