- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA
ALOYCE NDELEIO
Miongoni
mwa nchi zinazoendelea zimeshajengeka fikra kwamba bila misaada haziwezi kupiga
hatua na hilo kushabikiwa na walio wengi imekuwa ni jambo la kusikitisha.
Inasikitisha
kwa sababu hali hiyo ni kujikana na hata kujilemaza na kuwa tegemezi ilhali
zinaweza kujinasua katika mkondo huo.
Wanaoona
kujinasua wamekuwa wakidhihakiwa kwamba si rahisi kwao kujitegemea kwa kuwa
ubavu wa kufanya hivyo hawana, lakini hali ni tofauti kwani ubavu wa kufanya
hivyo upo.
Walio
katika mkondo huo hususani miongoni mwa nchi za Afrika wanatambua kuwa zipo
rasilimali nyingi ambazo zinaweza kutumika badala ya kutegemea misaada.
Kilichojitokeza
katika mkondo huo ni kwamba nchi zilizoendelea na ambacho zinategemewa
kwa misaada zinatambua kuwa misaada zinayotoa haisaidii kuzinyanyua nchi
zinazoendelea, lakini haziweki hilo wazi.
Hilo
linawekwa wazi na baadhi ya watu kutoka katika nchi hizo hizo zilizoendelea
ambao wanasikitishwa na matendo au unafiki uliomo katika utoaji wa misaada.
Uthibitisho
huo umo katika Kitabu kilichoandikwa na William Easterly, na kuchapishwa
na kampuni ya Penguin Press mwaka 2006 katika ukurasa wa nne,
ambacho kwa Kiingereza kinafahamika, “The White Man’s Burden; Why the
West’s Efforts to Aid the Rest have Done So Much Ill and so Little Good.”
Kwa
tafsiri isiyo rasmi; “Mzigo wa watu weupe; Kwanini juhudi za msaada za
Magharibi Mingi Imeleta Maumivu Makubwa na Neema Kidogo Sana.”
Anasema,
“Janga linalowakabili maskini linatokana na kwamba nchi za Magharibi
zimeshatumia dola trilioni 2.3 kwa ajili ya misaada inayotoa nje katika kipindi
cha miaka miongo mitano na hata hivyo hazijaweza kutoa senti 12 za dawa
kwa ajili ya watoto ili kuwaokoa nusu yao na vifo vinavyotokana na malaria.
“Nchi
hizo zimetumia dola trilioni 2.3 lakini zimeshindwa kutoa dola nne kwa ajili ya
vyandarua kwa familia maskini.
“Zimeshatumia
dola trilioni 2.3 na bado zimeshindwa kutumia dola tatu kwa ajili ya mama
anayejifungua kwa mara ya kwanza ili kuzuia vifo milioni tano vya watoto.
“…Inavunja
moyo kwamba jamii duniani zimeibua njia zenye ufanisi wa hali ya juu kwa ajili
ya kutoa burudani kwa matajiri, watoto na watu wazima, wakati haiwezi kutoa
senti 12 kutibu watoto maskini wanaofariki.”
Nukuu
hiyo haina ubishi wa aina yoyote kwamba aliyoyaelezea mwandishi huyo ni ukweli
kuwa kile wanachokitoa nchi tajiri ni sawa na tone la maji kutoka baharini na
kwamba hiyo haiwezi kuwa ni misaada bali ni sawa na makapi tu.
Kauli
hiyo haijatoa kwa mwandishi huyo katika kitabu chake tu, bali pia watu maarufu
kutoka nchi zilizoendelea nao wamekuwa na mawazo yanayoonesha kuwa upo unafiki
mkubwa katika utoaji huo wa misaada.
Rais
wa 39 wa Marekani, Jimmy Earl Carter katika nukuu yake moja alisema kuwa
wakati Marekani inatoa kiwango kikubwa cha misaada ya kivita kwa nchi
inazoziona kimkakati kuwa ni muhimu, inashika nafasi ya chini miongoni mwa nchi
zilizoendelea katika kiwango cha misaada ya kibinadamu inayotoa kwa nchi
maskini; na kuongeza, “Tumekuwa wang’ataji kushinda mataifa yote.”
Kauli
ya Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter aliitoa hivi karibuni katika
Chuo cha Principia kilichopo Elsah, katika jimbo la Illinois.
Kwa
mtazamo huo ndipo zinapoibuka kauli kwamba itakuwa inashangaza sana kuwaona
watu na akili zao timamu kushangilia kupata msaada.
Mshangao
huo unaibua hoja kwamba wanatusaidia kwa sababu gani? Wana mapenzi
na nchi maskini kwa sababu ipi? Ni wajomba, wazazi na wana uchungu na
nchi maskini? Kuna ule msemo kwa lugha ya Kiingereza "there is no free
lunch", tafsiri yake hakuna mlo wa mchana wa bure.
Jambo
la msingi ni kwamba nchi zinazoendelea hususani Tanzania na kwa kulingana na
kauli ambayo iliwahi kutolewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwamba nchi hii
si ya kuomba kwa mtu yeyote kwani ina kila kitu.
Aidha
jambo linalotakiwa ni kuwa na uhuru kamili juu ya rasimali zetu kwa kuzitumia
kwa ufanisi, kuziongezea thamani, na kushiriki kupanga bei ya kuuza bidhaa
zinazotokana na rasilimali zetu bila ya kupangiwa bei kwa maufaa yetu na si
kuegemea katika huo uhuru wa bendera ulipo.
Japo
lililo dhahiri ni kwamba uwezo huo upo kwa jamii kuacha kuwa makuwadi na
badala yake kipaumbele kiwe ni kuiweka Tanzania mbele badala ya kuweka
ubinafsi, wizi, udanganyifu, ubadhirifu, ufisadi na aina yoyote ile ya uchafu
wenye taswira ya kuipeleka nchi kombo.
Hali
hiyo inamaanisha kile alichokisema Rais kuwa badala ya wao kuwa watoa msaada
sisi ndiyo tunatakiwa kuwapa msaada kwani wao wanatuhitaji sisi kuliko
tunavyowahitaji.
Tafakari
inayoweza kuweka jambo hilo kwa uwazi ni ya kujiuliza ni bara gani duniani
lenye rasimali nyingi zaidi hapa duniani kwa wakati huu ambazo bado
hazijatumiwa? Kwa nini kila mataifa makubwa yako kiguu na njia kuja Tanzania,
Congo DRC na Afrika ya Kusini na nchi nyingine za Afrika?
Sharon
LaFraniere, mwandishi wa gazeti la New York Times, Julai 2005
aliandika kuwa kiasi kikubwa cha fedha za msaada zaidi ya dola
milioni 300 zilizotolewa kwa Afrika kuanzia mwaka 1980 ziliishia kwenye
mashimo ya utapeli, ubadhirifu na kupotea katika mazingira yasiyoeleweka.
Hata
hivyo mchumi mwandamizi Paul Collier yeye aliandika kwenye Jarida la Uchumi la
Afrika Mei 2006 kwenye makala yake, “Nini tunatarajia kutoka kwenye
msaada kwa Afrika?… ukweli uko wazi na kinyume na imani hiyo.
Misaada haijapotea bure; bali imeuweka uchumi wa Afrika kuelea na kupita
kwenye kipindi kigumu.”
Kwa
mujibu wa Benki ya Dunia kwenye mada inayohusu misaada kwa nchi za
Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na mustakabali wa dola bilioni 650 inatuhumu
kuwa misaada imekuwa inatiririkia mikononi mwa madikteta na tawala za
rushwa ambazo hazina nia za dhati na maendeleo ya taifa.
Hali
kadhalika kwa mujibu wa Kituo cha Utafiti wa Maendeleo Kimataifa cha
Ufaransa, kufungamana na nchi zilizokuwa zinazitawala wakati wa ukoloni nako
kumekuwa ni kigezo cha kihistoria cha kutolewa kwa misaada.
Hata
hivyo Chuo Kikuu cha Maryland katika kupima watendaji wanavyoshikilia
madaraka kwa kutumia mfumo unaofahamika kama ‘Polity IV’
kinabainisha kuwa takribani nusu ya misaada yote kuanzia
mwaka 1960-90 ilienda kwa nchi ambazo zilikuwa na ‘mamlaka ya utendaji isiyo na
mipaka’ na asilimia 10 tu ilienda kwa nchi zilizokuwa na demokrasia yenye
‘mipaka ya utendaji’.
Ipo
nahau moja inayosema, ‘Kula mtu kivuli’ inayomaanisha kumfanyia mtu mambo
ya kumdhuru na kumwendea kinyume na hali mbele ya macho yake unamwonesha kuwa
mwema kwake.
Hivyo
ndicho nchi zilizoendelea zinazifanyia nchi zinazoendelea.
- Get link
- X
- Other Apps




Comments
Post a Comment