Featured Post

MIKAKATI SHIRIKISHI NYENZO YA KUPAMBANA NA UJANGILI



NA ALOYCE NDELEIO
Mafanikio ya kuwalinda tembo dhidi ya ujangili yametokana na  mikakati kadhaa ya msingi ambayo imewezesha wanyama hao kuongezeka ikiwemo ushirikishwaji wa jamii, kuongeza askari, matumizi ya teknolojia kupambana na majangili na ushirikishwaji wa jumuia ya kimataifa.
Aidha mikakati mingine ni kusitisha biashara ya meno ya tembo, ushirikiano miongoni mwa nchi za Afrika, mikataba baina ya nchi jirani, uratibu wa utekelezaji wa sheria, mchango wa mashirika ya wanyama pori na tafiti mbalimbali duniani.

Hizi ndizo nyenzo ambazo zimewezesha kuleta matumaini kwenye maisha ya mnyama huyo, na hata hivyo ushirikishwaji wa jumuia na watu hususan katika muundo wa  Maeneo ya Uhifadhi ya  Wanyama pori (WMA) imewezesha  jumuia kwenye maeneo yanayozunguka  hifadhi  kujihusisha  kwenye  kuhifadhi  na matumizi endelevu ya bidhaa  zinazotokana na wanyama pori
Awali maeneo hayo yalikuwa yakisaidiwa na serikali  ya Tanzania na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na WMA nyingine kama Ikoma  zimekuwa na mafanikio kwenye kupata fedha na hali kadhalika kwenye kuhifadhi.
Jumuia kwenye maeneo haya zimekuwa zinafanya upelelezi ambao umekuwa unasaidia juhudi za serikali katika kupambana na ujangili kwenye maeneo hayo.
Kwa upande wa matumizi ya askari wanyama pori inafahamika kuwa iwe iwavyo  hakuna kinachoweza kuchukua nafasi ya askari hao kutokana na kujituma kwao kulinda wanyama pori nchini Tanzania.
Kipindi cha hivi karibuni idadi ya askari wanyama pori iliongezwa mara mbili  zaidi ili kukabiliana na changamoto zilizopo  kwenye mfumo wa ikolojia wa Ruaha-Ruangwa ambao umekuwa unaonekana kama kitovu cha uhalifu wa ujangili Tanzania  na hivyo kuwa ndio lengo kuu katika kuchukua hatua.
Matumizi ya teknolojia katika kupambana na ujangili  ni jambo ambalo limekuwa likifanyika  kuanzia kwenye majaribio hadi kufanikiwa kutumia ndege zisizo na rubani (drone), matumizi ya  kidijitali ya mawasiliano ya Very High frequency (VHF) na matumizi ya kompyuta  zilizo na GPS miongoni mwa askari wanyama pori mambo ambayo yameifanya Tanzania kuwa  mstari wa mbele katika mstari wa kupambana na majangili.
Ongezeko la matumizi ya ndege maalum, helikopta na hali kadhalika aina mbalimbali za magari kwenye uwanja wa mapambano  kumekuwa kunabadilisha mwenendo wa vita dhidi ya  ujangili.
Serikali ilishabainisha kuwa kwenye ushirikiano wa kimataifa kwamba tangu kuridhiwa kwa mkakati wa kupambana na ujangili, serikali  imefanya kazi kwa ukaribu na washirika wake wa maendeleo katika kukabiliana na tatizo hilo kwa pamoja.
Hali hiyo ilisababisha kunaamini kwenye uwazi na ufumbuzi katika kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwenye vita dhidi ya ujangili.
Programu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP), Ujerumani, Uingereza, Marekani, China na Benki ya Dunia  ndio wamekuwa washirika wanaoongoza katika kushirikiana na Tanzania kwenye juhudi zake za kupambana na ujangili.
“Tanzania pia imejiunga na  Mkakati wa Kulinda Tembo Afrika (AEPI) pamoja na nchi za Botswana, Gabon, Chad na Ethiopia  chini ya uongozi wa Uingereza  kuratibu juhudi za Afrika  kwenye mataifa yaliyo mstari wa mbele katika vita dhidi ya ujangili.
“Mbali na maazimio ya mkutano mbalimbali Tanzania imejikita kufanya kazi na serikali ya Uingereza kupitia makubaliano na shirika la Stop Ivory  ambalo ni shirika la hisani la Uingereza na imeshuhudiwa  ikifanya kazi na wataalamu  wakiwemo kutoka CITIES katika kukusanya shehena kubwa ya pembe za ndovu nchini.
Kuhusu ushirikiano miongoni mwa nchi za Afrika  Novemba 2014 Tanzania  ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa kikanda uliozikutanisha nchi 11  kwa ajili ya kujadiliana  na kufikia maamuzi ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa  kudhibiti na kuzuia uhalifu dhidi ya wanyama pori.
Kuwepo ushiriki hai wa Benki ya Dunia (WB), Umoja wa Ulaya (EU), Marekani, Uingereza, Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), China, Ufaransa, Ujerumani na nchi 11 za Afrika ambazo ni  Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini, Malawi, Zambia, Msumbiji, Afrika Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), zilikubaliana kuhusu hatua za ziada zinazotakiwa kuchukuliwa kwa pamoja katika  kusitisha mauaji ya wanyama pori.
Hata hivyo kuhusu makubaliano na nchi jirani yapo makubaliano ya Selous-Niassa  kati ya Tanzania na Msumbiji  ambayo ni matokeo ya mkutano uliofanyika  Arusha hivi karibuni.
Kwenye makubaliano hayo juhudi za kimataifa  ziliwekwa pamoja  katika kuisaidia Tanzania na Msumbiji  kuyaweka kwenye utendaji makubaliano ya kuulinda mfumo mkubwa wa ikolojia ya wanyama pori ambao unahusisha eneo la ardhi ya kilomita za mraba 110,00.
Makubaliano hayo hatimaye yalisainiwa Mei 2015 na ni moja ya mafanikio makubwa ya uhifadhi ndani ya  mwongo huu, kwani yatahakikisha tembo wanaishi katika  kipindi cha miaka ijayo na hata kuvuka mipaka.
Aidha kwa upande mwingine  Tanzania na Kenya zinashirikiana mfumo wa ikolojia wa Serengeti-Mara. Kwa kuzingatia utafiti wa tembo uliofanywa mwaka 2014  mfumo huo wa ikolojia  umefanikisha kuongezeka kwa idadi ya tembo kwa asilimia 98 kutoka mwaka 2009 hadi 2014.
Juhudi za pamoja zikiwemo za kushirikiana kiintelijensia kati ya Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Huduma ya Wanyama pori ya Kenya (KWS) kumeonesha mafanikio katika ushirikiano wa kuhifadhi kwenye eneo la mpakani.
Tembo hawajui mipaka na uhamaji wa wanyama wa Serengeti-Mara ni dhihirisho la aina yake duniani la uhamaji wa wanyama kwa msimu kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Hata hivyo  umekuwepo uratibu kwenye utekelezaji wa sheria ambapo mashirika ya ndani pamoja na ya kimataifa yamezidisha kasi ya kufanya kazi pamoja katika kushughulikia na kufuatilia bidhaa haramu za wanyama pori pamoja na dawa za kulevya.
Polisi wa kimataifa, Kikosi kazi cha makubaliano ya Lusaka pamoja na mashirika mengine makubwa duniani yamekuwa yakitafuta njia za kufanya kazi pamoja katika kushughulikia suala la usafirishaji  lakini pia kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wote wanaohusika na ujangili.
Mchango wa mashirika ya utafiti na wanyama pori  duniani nao umewezesha kudhibiti shughuli za ujangili ambapo  makundi kama  Jumuia ya Kuhifadhi  Wanyama pori ya Chuo Kikuu cha Cambridge yametoa mchango maalum katika kuhifadhi flora na fauna za Afrika kwa ajili ya kizazi cha leo na kizazi kijacho.
Tafiti zisizoisha  zikiangalia tabia za wanyama, magonjwa yanayoambukiza miongoni  mwa wanyama wanaofugwa na wanyama pori kumewezesha watafiti kusaidia kuhabarisha maamuzi kuhusu uhifadhi endelevu.
Jambo lililo wazi ni kwamba kuhifadhi wanyama pori kunachangia upatikanaji wa maendeleo na aina ya  uhifadhi wa mafanikio na endelevu utaweza kushughulikia changamoto zinazohusu masuala ya maendeleo ya watu katika dhana nzima ya kuwalinda wanyama pori kwa ajili ya utalii na matumizi mengine au uvunaji wa wanyama pori.
Aidha ni muhimu kwamba watafiti wanaendelea kuangalia namna nzuri ya utendaji  ambao jumuia zinaweza  kuangalia faida za uhifadhi kwenye maeneo yao ili dunia iweze kufanikiwa kwenye kuhifadhi urithi wa wanyama pori.
Tofauti na nchi nyingine barani Afrika, Tanzania imetenga asilimia 30 ya ardhi yake kwa ajili  ya hifadhi ya wanyama pori  na amana hizi zimekuwa zinasimamiwa  kupitia mfumo rasmi wa utawala wa taasisi mbalimbali.
CHANZO: TANZANITE


Comments