- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
VIONGOZI tisa wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) wanaokabiliwa na mashtaka 13, katika kesi ya jinai
namba 112 ya mwaka huu kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, watasomewa maelezo
ya awali (PH) Septemba 27, mwaka huu akiwemo Freeman Mbowe.
Washtakiwa hao walipaswa kusomewa maelezo hayo
na upande wa mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri lakini
ilishindikana kwa sababu mshtakiwa wa tano, Esther Matiko ambaye mbunge wa Tarime
Mjini hakuwepo mahakamani, mdhamini wake
alisema ana tatizo la kiafya kwenye mfumo wa uzazi.
Hata hivyo, Wakili Peter Kibatala
anayewatetea washtakiwa hao aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa Peter Msigwa
ambaye ni Mbunge wa Iringa mjini alikuwa akitetewa na wakili Jeremiah Mtobesya
ambaye amejitoa.
Baada ya Kibatala kueleza hayo, mchungaji Msigwa
alinyoosha mkono mahakamani hapo na kuieleza mahakama kuwa ana kesi nyingine
katika Mahakama ya Iringa kwani muda mwingi yupo katika Mahakama ya Kisutu
hivyo aliomba mahakama hiyo iiandikie samasi Mahakama ya Iringa.
Pia mchungaji Msigwa aliomba mahakama impatie
muda wa wiki tatu ili aweze kutafuta wakili.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo
ambapo ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar, Salum Mwalimu na Naibu
Katibu Mkuu Bara ambaye pia ni Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime
Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Esther
Bulaya.
Wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Msigwa,
Mbunge wa Tarime Mjini, Matiko na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dkt. Vincent
Mashinji.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na
mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha
hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi, kushawishi utendaji
jinai kati ya Februari Mosi na 16, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Comments
Post a Comment