- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA CONGES MRAMBA, MWANZA
ZAIDI ya vibanda 500 vya mabanzi, vilivyokuwa
vinatumiwa na wafanyabiashara kama maduka na makazi, viliteketezwa kwa
moto, Sengerema mkoani Mwanza.
Vibanda hivyo vilikuwa vimejengwa kwa mabanzi ya
miti, huku vikiwa vimeezekwa kwa karatasi za nailoni na makuti au nyasi, huku
mali za thamani kubwa pia ziliteketea.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,
Ahmed Msangi, alisema, zaidi ya vibanda 300 viliteketea kwa moto Juni 30,
2016 majira ya saa 8:00 mchana katika Kisiwa cha Kabiga, Kata ya Maisome, Tarafa
ya Kahunda.
Kamanda Msangi alisema, vibanda hivyo vilikuwa
vimejengwa kwa mabanzi na miti huku vikiwa vimeezekwa kwa karatasi za nailoni,
huku mali za thamani kubwa zikiwemo ndani, ambazo pia ziliungua na kuwa majivu.
Polisi walisema, moto huo uliwashwa na watu
wasiofahamika.
Wafanyabiashara wengi wa visiwani wana kawaida kununua
mafuta, hususan petroli, wanayotumia katika injini za boti za uvuvi Ziwa
Victoria.
Petroli hiyo huwa inahifadhiwa katika mabanda
haya wanayoyatumia kama nyumba za kuishi, nyumba za kulala wageni na mabanda ya
biashara.
Polisi walisema, siku hiyo ya ajali ya moto, inakisiwa
wezi waliiba mafuta, wakawa wanagawana ndani ya moja ya vibanda hivyo.
Kufuatia vibaka hao kugawana petroli jirani na
vibanda hivyo, moto ukalipuka. Pengine kuna mtu aliwasha sigara jirani na
mahali hapo.
Vibaka hao walitoroka wakawa wanatafutwa na
polisi ili wafikishwe mahakamani kujibu mashitaka.
Aidha, siku hiyo hiyo ya Juni 30, 2016, katika
kisiwa kidogo cha Migongo huko huko Maisome wilayani Sengerema, vibanda vingine
200 viliteketea kwa moto majira ya saa 4:00 usiku na kusababisha mali za
thamani kubwa kuteketea.
Chanzo cha moto huo kilitajwa kuwa ni mshumaa uliounguza
makuti.
Wafanyabiashara hawa wanamiliki fedha nyingi, lakini
wanaishi katika vibanda hivi vya makuti, huku wakiweka bidhaa za thamani na
magudulia yaliyojaa petroli!
HAWAJENGI NYUMBA BORA
Matukio ya moto yamekuwa ya mara kwa mara kutokana
na makazi holela katika visiwa hivyo zaidi ya 100 vya Ziwa Victoria katika
mikoa ya Kagera, Mwanza, Geita na Mara.
Makazi ya visiwani ambako ardhi ni mchanga,
hakuna hata vyoo.
‘Matajiri’ hawa wamekuwa wakienda haja ndogo na
kubwa ufukweni mwa Ziwa Victoria.
Kulingana na wataalam wa magonjwa ya milipuko, kipindupindu
huanzia visiwani humo kila mwaka na kuua maelfu ya watu.
Hata wanapougua kipindupindu, watu hawa husema
kwamba ‘wamerogwa’ na wachawi kwa kutumia uchawi wanaoita, ‘Kadumu’!
Mwaka 2016 walikufa mamia ya wavuvi na
wafanyabiashara hawa visiwani humo.
“Wachawi hujaza sumu ya uchawi wao katika galoni
(kadumu); halafu uchawi huo humwagwa ziwani au mitoni, mtu akinywa maji, tayari
anahara na kutapika!" ndivyo wanavyosema.
Hizo ndizo imani za ‘Matajiri hawa Uchwara’ wa
visiwani…na ndiyo chimbuko la uchawi wa ‘Kadumu’ ambao maofisa wa afya wa mikoa
ya Mara, Kagera na Mwanza wanaamini ni kipindupindu.
Vifo vya magonjwa ya kuambukiza yatokanayo na
ngono zembe (Sexually Transmitted Diseases) kama Ukimwi, ni ya
kawaida sana katika visiwa hivi.
Na mtu akiugua hawezi kutambua kwamba
ameambukizwa kutokana na uzembe au kukosa elimu. Atasingizia uchawi na wachawi.
‘Matajiri’ hawa wa visiwani wana imani potofu, ndiyo
maana wana fedha lakini hawaachani na mila na desturi za kale zinazorutubisha ushirikina.
Wengine wamepiga ramli na kukatazwa kuishi
katika nyumba bora, wengine hawalalii vitanda, na wengine hawavai viatu. Wanaita,
‘ndagu’.
Ndagu hizi hutafutwa kwa njia haramu hata kuua
albino na kunyofoa viungo. Hawa ndiyo wenye imani kwamba, sangara akiona nywele
za albino katika nyavu, hata akiwa Kisumu nchini Kenya, anakuja kwa kasi na
kunasa mtegoni!
UKEREWE
Mfanyabiashara na mkazi wa kitongoji cha Bukini, Kijiji
cha Chifule huko Bukungu, Tarafa ya Ukara, Ukerewe alipoteza maisha kufuatia
moto mkali kulipuka na kuunguza nyumba nzima, wakati yeye na mwenzake aitwaye
Dotto wakimimina mafuta aina ya petroli.
Zephania Bitta (42) alikumbwa na mkasa wa kulipukiwa petroli
Julai 30, 2016, saa 4:30 asubuhi.
Kamanda wa Msangi, alisema kwamba, marehemu akiwa na
mwenzake Dotto, walikuwa wakimimina petroli hiyo kwenye madumu katika chumba
cha kulala.
Naam, petroli katika chumba cha kulala!
Ghafla nje akaja mtu aliyekuwa akivuta sigara, moto huo wa
sigara ukalipua petroli, ukaunguza nyumba hiyo na kusababisha watu
hao kuungua vibaya!
Kufuatia kuungua kwa nyumba hiyo, thamani ya mali
iliyoteketea haikujulikana.
Kufuatia hali hiyo, Kamanda Msangi alitoa rai kwa wakazi wa
Ukerewe kuwa macho na kutunza petroli katika nyumba zao za kulala, huku sigara
zao zikiwa hazibanduki midomoni, wakipuliza moshi angani mithili ya treni!
Wilaya ya Ukerewe peke yake ina jumla ya visiwa 38.
Mkoa wa Mwanza una visiwa 79. Mikoa ya Mara, Kagera, Simiyu
na Geita, hufanya visiwa takriban 100 ambako wanakaa wavuvi hawa wenye imani za
kijima.
MATAMBIKO
Hata mitumbwi yao na nyavu hufanywiwa matambiko ili iweze
kunasa samaki kwa wingi na kuleta utajiri mkubwa.
Kandoni mwa makazi ya watu hawa, unaweza kukuta
vibanda vidogo vya mviringo (tembe) vilivyokandikwa kwa udongo na kuezekwa kwa
nyasi.
Humo ndani, ni mahali pa kutambikia mizimu, wao
huita “Bhinyasamba”, wanaamini mizimu yao huishi humo, kwa hiyo kila siku
wanawaletea mizimu hao kilo nyingi za nyama, ili bahati au baraka isije
ikawaacha!
Nataka kusema kwamba, katika visiwa vingi vya Ziwa
Victoria ni mahali pa kutambikia mizimu.
Nahodha wa Meli ya Samar II ya jijini Mwanza (jina
linahifadhiwa) aliwahi kuniambia kwamba, kina cha maji ya ziwa hili hupungua
sana nyakati za kiangazi.
Kufuatia kupungua kwa kina cha maji, basi miamba
mingi huzuka ziwani na kuhatarisha meli au boti zinazoweza kukwaa miamba hii na
kutoboka.
Mahali pengine meli hizi hushindwa kutembea
baada ya nyavu za wavuvi kukusanywa na ‘propellers’ za injini, hivyo meli
kulazimika kuzima majini.
Wakati mwingine pia meli au mitumbwi na boti
hunasa kwenye tope zito katikati ya ziwa, hasa mpakani mwa nchi tatu za Kenya, Uganda
na Tanzania.
Ikitokea meli ikanaswa au ikazima injini, watu
hawa huamini ‘imeshikwa na mizimu’, hivyo hulazimika kutambika kwa kujikata
vidole ili damu imwagwe ziwani!
MAANA
YA MWANZA
Jina la Mwanza limetokana na neno, “Ngwahnzah’au
‘Mwah-n-zah’, maana yake ni majaruba ya mpunga!
Ni jiji lililojengwa kandoni mwa fukwe za Ziwa Nyanza.
Ziwa Nyanza (Nyanza mana yake Maji Mengi), liliitwa
Victoria kwa heshima ya Malkia Victoria wa Uingereza, binti wa Mfalme Edward
aliyekuwa mtoto wa nne wa Mfalme George III.
Alitawala kuanzia 1837-1901 aliporithiwa na
mwanaye mkubwa, Edward VII.
Aliyeliita ziwa hili kwa jina hili ni John
Hanning Speke (miaka ya 1850) alipokuwa akitafuta chimbuko la Mto Nile, ule
unaotiririka kuanzia Mto Luvironza, Burundi hapa Afrika Mashariki hadi Bahari
ya Mediterranean, umbali zaidi ya kilomita 6,656 kama maili 4,160.
Hivyo, ziwa hili ni kivutio kikubwa cha utalii (tourist
site) ambacho kinaweza kuiingizia nchi fedha nyingi za kigeni.
Ziwa hili linaumbwa na maji yanayotiririshwa na
mito mikubwa kama Kagera na Nzoia, hususan nyakati za mvua kubwa za vuli
na masika kutoka misitu mbalimbali hapa Afrika Mashariki na Kati.
Hii misitu inayoleta mvua na kujaza ziwa hili
sasa inafyekwa kwa kasi ya kutisha.
Ziwa hili huletewa maji na mito mingi midogo
kama Simiyu, Duma, Mara na kadhalika kutoka nyanda za juu za miinuko na milima
yenye misitu minene.
Ni ziwa la pili kwa kuwa na maji baridi hapa
duniani, nyuma ya Superior huko Marekani.
Lina ukubwa wa kilomita 68,000; kama
maili 26,828 na humilikiwa na nchi tatu za Afrika Mashariki ambazo ni
Kenya (asilimia 6), Uganda(43%) na Tanzania (51%).
Kina chake ni futi 270, ni kina kifupi
sana. Ziwa Tanganyika lina kina cha futi 4,823.
Kuna mnara ambao unaonesha maandishi
yanayoeomeka kwamba, mwaka 1858,John Hanning Speke alikuwa Mzungu wa kwanza
kuliona Ziwa Victoria akiwa kilima cha Isamilo.
Dk. Speke alikuwa akipeleleza chanzo cha Mto
Nile, na aliyaita maji haya ya Ziwa Nyanza maana yake Maji 'Inyanja' kwa
Wakerewe na Wajita, na 'Lweru' kwa Wahaya, kwa heshima ya Malkia wa Uingereza,
Victoria.
Jiji la Mwanza linatambulishwa na mawe haya
yaliyobebana yanayoitwa, Bismarck ama Bismarck Rock, yaliyoko katika fukwe za Ziwa
Victoria.
Mawe haya yamepewa jina la aliyekuwa Chancellor
wa Ujerumani, Chancellor Bismarck miaka ya 1880.
Mahali pengine mawe haya huabudiwa. Kuna mawe
Ukara wanasema yanacheza dansi (The Dancing Rock), na mengine yapo visiwa vya
Irugwa.
Mamilioni ya watu katika nchi hizi hulitegemea ziwa
hilo kwa maji ya kunywa, chakula, usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria -
nazungumzia mchango wa Ziwa Victoria katika uchumi wa wakazi wanaolizunguka na
uchumi wa taifa kwa ujumla.
Uchumi wa wakazi wa ufuo wa ziwa hili hutegemea
uvuvi wa samaki ili kujipatia chakula chao (samaki ni chanzo cha protini
nyingi) na mahitaji mengine muhimu ya kiuchumi.
Mazao na shehena nyingine hutegemea ziwa hilo
kusafirishwa kwenda viwandani, ng’ambo au kutoka sokoni.
Rwanda, Kenya, Tanzania, Uganda na kadhalika
hutegemea ziwa hili kusafirishia shehena ya mazao au bidhaa nyingine.
TOPE
Mito kama Simiyu na Duma imegeuka kuwa kitisho
kwa uhai wa Ziwa Victoria.
Mito hii huingiza ziwani asilimia 40 ya kiasi
cha tope zote zinazoingizwa nyakati za mvua.
Tope zinapojazwa ziwani kutoka nchi kavu
husababisha kina cha ziwa kupungua kila mwaka.
Tope zikijaa ziwani wenyeji wakiona mitumbwi
imenaswa, wanasema wameshikiliwa na mizimu.
Kina cha ziwa kinapopungua huleta athari nyingi
ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mazalia ya samaki, kuongezeka kwa gugu maji (water
hyacinth) linaloondoa oksijen kwa viumbe wa majini.
Adui wa kwanza wa Ziwa Victoria ni kilimo ndani
ya mita 60 kutoka mito inayomwaga maji yake ziwa hili, kinacholeta mmomonyoko
wa udongo baada ya misitu kufyekwa kwa ajili ya upanuzi wa mashamba.
Adui namba moja wa Ziwa Victoria ni wananchi
wanaoendesha kilimo ndani ya eneo la mita 60 kutoka ziwa lenyewe kama barabara
ya Makongoro jijini Mwanza, na kando ya mito mikubwa kama Simiyu, Duma, Kagera,
Nzoiya na kadhalika.
Inadaiwa, ziwa hili liliwahi kukauka miaka
mamilioni yaliyopita, ingawa Biblia inasisitiza dunia ina umri wa miaka zaidi
kidogo ya 6,000 tu tangu kuumbwa na Yehovah.
Kwa kipindi cha kati ya mwaka 1998 na 2006, maji
ya Ziwa Victoria yalipungua kutoka mita 1,141.24 juu ya usawa wa bahari hadi
mita 1,139.20.
Upungufu huu ulikuwa wa wastani wa mita 2.04.
Kufuatia hali hiyo, hata meli zimekuwa
zikishindwa kutia nanga bandarini hususan huko Nansio, Ukerewe, na meli
zinakuwa hatarini kuparamia miamba na kupasuka kufuatia kuzuka kwa miamba.
Hali hii ni hatari kwa maisha ya abiria na
mizigo yenye thamani ya mamilioni ya fedha.
JIJI LA MWANZA
Kilomita za eneo 425
ndizo nchi kavu na eneo lililobaki ni maji ya Ziwa Victoria.
Hali ya hewa hapa ni
joto; nyuzi joto kati ya 25 C hadi 30.2 nyakati za hari.
Wakati wa baridi hali ya
hewa huwa nyuzi joto 15.4 hadi 18.6 C, na wastani wa mvua kwa mwaka ni 700-1,000
mm hasa mvua za vuli hunyesha hapa kati ya Oktoba na Desemba na masika ni
Aprili hadi Mei.
MINYOO NA KICHOCHO
Kulingana na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa
(WHO) asilimia 25 ya watu wanaoathiriwa na sumu hapa duniani ni wale waliokula
sumu hizo kupitia maji ya kunywa.
Hata wana minyoo na kichocho. Wakivimba matumbo,
utasikia wanasema, “Wachawi wamewatega uchawi kwenye viti vya kienyeji!”
Kwa lugha za wenyeji, ukiwa na kitambi cha
minyoo, wanasema ‘Bhamamulisya!” yaani amelishwa uganga, uchawi, mabhugota!
Asilimia takriban 80 ya wakazi wa Mwanza
na maeneo haya ya visiwa, wana kichocho, minyoo, safura na wanahara na
kutapika (kipindupindu) kufuatia uchafu na hujuma wanayolifanyia ziwa hili
muhimu kwa maisha yao.
CHANZO: FAHARI YETU





Comments
Post a Comment