Featured Post

MAHAKAMA YASEMA ABDUL NONDO 'ALIYEJITEKA' ANA KESI YA KUJIBU



NA MWANDISHI WETU, IRINGA
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Iringa, imemkuta na kesi ya kujibu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Omary Nondo.

Akisoma hukumu ndogo jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi Liad Chamshama, alisema baada ya kupitia maelezo ya pande zote, mahakama imemuona Nondo anakesi ya kujibu kulingana na kielelezo namba sita.
Kielelezo hicho ni nyaraka kutoka Jeshi la Polisi aliyoandikishwa Nondo Mjini Mafinga akidai ametekwa na watu wasiojulikana, kuachiwa karibu na Kiwanda cha Pareto (PCT) kilichopo Mjini Mafinga.
Chamshama alisema, Nondo alitoa taarifa za uongo mbele ya shahidi namba moja ambaye ni Ofisa wa Jeshi la Polisi au Serikali mwenye namba E.2328, Coplo Salum wa Kituo cha Polisi Mafinga.
Alisema mshtakiwa ana kesi ya kujibu kwa mujibu wa kifungu namba 231 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambapo mshtakiwa anayo haki ya kujitetea.
Kesi hiyo iliyotolewa hukumu ndogo kwa muda wa dakika 13, ambapo Nondo aliongozana na Wakili msomi, Chance Luwoga ambaye alisema mteja wake atajitetea.
Machi 21, mwaka huu mshtakiwa hiyo alifikishwa katika mahakama hiyo kwa kosa la jinai namba 13 ya mwaka 2018 akidaiwa kuchapisha taarifa za uongo kwa njia ya kompyuta akitumia simu ya mkononi kinyume na sharia ya makosa ya mtandao namba 16 ya mwaka 2016 na kusambaza taarifa hiyo kwa njia ya Whatsapp.
Machi 7, mwaka huu, mshtakiwa akiwa katika eneo la Ubungo, Dar es Salaam alidaiwa kusambaza ujumbe kwa kwa njia ya mtandao wa Whatsapp akitumia simu namba 0659-366125 uliosomeka (Im at risk) akibainisha yupo  hatarini, baadaye taarifa hiyo ilisambaa kuwa ametekwa na watu wasiojulikana hali iliyoleta hamaki katika jamii.

Comments