Featured Post

KUHABARISHWA KUTAWEZESHA KILIMO KUUNGANISHA MIJI, VIJIJI



NA ALOYCE NDELEIO
Jamii kuhabarishwa kuhusu kilimo ni jambo la msingi  katika kupata maendeleo yanayohitajika katika sekta hiyo inayotegemewa  kwa ajili ya chakula pamoja na malighafi inayotumika viwandani.
Lakini ni dhahiri kuwa vyombo vya habari mara nyingine vimekuwa  vinajikita kwenye masuala yanayohusu kilimo na ukweli unabakia kuwa  waandishi wa habari wana jukumu gumu la kuwa kiunganishi  katika  jamii za mijini na vijijini.

Uhaba wa chakula, mabadiliko ya hali ya hewa, utandawazi, bioteknolojia, utabiri kuhusu kupungua kwa kiwango cha maji ni baadhi ya mada nyingi ambazo moja kwa moja zinabeba  maisha ya kila mtu  iwe mijini au vijijini.
Miongoni mwa nchi nyingi zinazoendelea  kilimo kimekuwa mioyoni mwa mada hizo lakini ili kuelewa kwa uwazi ni namna  gani  maisha yalivyo katika ulimwengu wa vijijini ni muhimu kuboresha maisha ya   jamii katika maeneo hayo.
Wawekezaji, wafanya biashara, wapanga sera, wote wale  ambao makazi ya ni mjini wamekuwa wakijihusisha na mahitaji ya wakulima kuhabarishwa.
Hata hivyo uhabarishwaji  kuhusu sekta hii muhimu umebakia kuwa hautoshi, mara nyingine kuwa ni uhabarishaji wa nusunusu  usiokamilika na mara nyingine kutounganishwa na sekta yenyewe.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Mfuko wa  Kimataifa wa Habari wa Wanawake (IWMF) ulibainisha kuwepo kwa tofauti kubwa kati ya umuhimu wa kilimo katika uchumi miongoni mwa nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kilimo katika eneo hilo kinachangia asilimia 34 ya pato la ndani kwa nchi, asilimia 40 ya mauzo ya nje na asilimia 70 ya  ajira lakini kwa kulinganisha na nafasi inayopata katika vyombo vya habari ni kwamba inakejeliwa.
Katika nchi za Mali, Uganda  na Zambia  vyombo vya habari vilijikita katika kuhabarisha kuhusu kilimo kwa kiwango cha asilimia 4.0 ya kurasa au muda wa kurushwa kipindi.
Hata hivyo kilichojitokeza ni kwamba mchango unatolewa  na wanawake katika sekta ya kilimo ilikuwa ni nadra kupewa nafasi au kutolewa katika vyombo hivyo.
Asilimia 70 ya matukio kwenye redio, televisheni na  magazeti yaliyo mengi yalijikita kwenye mada zake kwa kuandika mada ambazo  zilitokana na mazungumzo na wataalamu.
Aidha vyombo hiyo ilibainika kuwa viliripoti hotuba  zilizotolewa ambapo asilimia 20 ya mada zilitokana na kuonana  na kuhojiana  na wakulima na wakazi wa vijijini ambao wana uzoefu wa moja kwa moja wa masuala hali halisi ya kilimo.
Mada nyingi zilizoandikwa  na kutanganzwa  kuhusu kilimo  zilionekana kuwa zinaegemea upande mmoja tu na kuusahau uapnde wa pili.
Kwa mfano  baadhi ya mada  zilikuwa zinahusu 'Wakati rais ametembelea au kama mtu amefariki kutokana na kukosa chakula au tukio la kutolewa misaada kwa ajili ya wahanga wa njaa.”
Mbali na matukio hayo ambayo  yaliwalazimisha  wahariri wa vyombo vya habari  wawapeleke waandishi wao kwenye  matukio hayo ni mara  chahche waaandishi wamekuwa wakitoka  mijini.
Aidha ilibainishwa kuwa kuandika kuhusu sherehe za kufunguliwa na kufungwa kwa semina ambako wanakuwa wamealikwa na kulipwa  kuliripotiwa kwa kiwango kikubwa.
Katika mazingira ya aina  hivyo utafiti huo unadai kuwa waandishi kwa kiwango fulani walikuwa ni maofisa uhusiano ambao walitakiwa kuhabarisha kuhusu mambo ambayo yameshafanywa na mamlaka  husika, asasi zisizo za serikali na vyama au mashirika ya kimataifa.
Ukweli na takwimu zilizohusishwa  zilitoka upande mmoja  ambao ulikuwa macho  kulinda  taswira yake.
Uandishi  wa kweli unajumuisha uchambuzi wa takwimu zilizotolewa  na kulinganisha na hali halisi katika mshamba ikiwa ni njia halisi ya  kuhakikisha na kuona kama miradi au ubunifu ni kweli unafanikiwa na  ni sahihi kwa maendeleo ya kilimo ya nchi.
Mchango mwingine wa waandishi ni kukusanya habari kutoka maeneo ya vijijini na hivyo kuziunganisha na wapanga sera na wanajamii wengine jambo ambalo limekuwa halitokei.
Kutokana na kukosekana kwa vyanzo, mashirika ya habari ni mara chache hupeleka waandishi wake vijijini. Usafiri na malazi  huwa ni wa gharama kwa ajili ya kutafuta mada  ambayo kipaumbele chake ni cha chini kwenye vyumba  vya habari.
Matokeo yake waandishi huishia kutegemea mashirika  ambayo yanaweza kuwalipia gharama za usafiri na hivyo kuwa mateka wa wadhamini wao ambao huwaonesha  ni kitu gani wanataka waaandike.
Maendeleo vijijini  yamekuwa yanapewa kipaumbele kidogo katika vyombo vya  habari. Wahariri wengi wa habari wanayachukulia  masuala haya kama yana mvuto kidogo kwa wasomaji na hivyo katika kuzipangia kurasa huziweka kwenye kurasa za ndani.
Hata hivyo ni mara chache pia zimekuwepo chambuzi au vipindi vilivyojikita kwenye kilimo. Mara nyingi suala la kilimo limekuwa likishughulikiwa  na  kurasa zinazohusika na masuala ya fedha au  biashara katika magazeti ya kila siku.
Inabainishwa kuwa  hata katika mitandao ya intaneti  ambayo inachapisha habari kutoka nchi mbalimbali imebainika ni mara chache  kumekuwepo kichwa kinachohusu 'kilimo' ambacho kinahusisha 'chakula, kilimo na  masuala ya vijijini’.
Hali kadhalika ilibainishw akuwa ni waandishi wachache waliojikita katika kilimo na mara nyingi huwa ni wachache katika vyombo vya habari.
Hata hivyo wale wanaoshughulisha na habari za kilimo wanakabiliwa na ugumu katika kutoa maelezo yaliyo wazi kwa wasomaji wake au wasikilizaji hususan katika masuala  magumu  kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, bioteknolojia au katika kuwahoji watafiti na wataalamu  kuhusu masuala  yanayohusu kilimo.
Hawa  huishia kutumia misamiati migumu  ya kisayansi na ni mara  chache hufanya juhudi za kujieleza wenyewe katika lugha ambayo inaweza kuwa rahisi kueleweka kwa wanaowahoji.
Kinadharia ni kwamba waandishi wanaweza kupata habari kupitia mtandao wa  intaneti lakini wanatakiwa kuwa na fursa inayowawezesha  kufikia na kufahamu  jinsi ya kutafuta  na kuchambua matokeo  yao kufuatana  na kiwango kikubwa cha takwimu kinachokuwepo.
Tatizo kwa kiasi fulani huonesha kukosekana kwa vifaa vya mafunzo kwa ajili ya uandishi wa habari za kilimo ikiwa ni pamoja na kukusanya  na kutawanya aina za habari zinazotakiwa
Tatizo hilo husababisha kukosekana kwa  uzoefu na  aina mbalimbali za stadi, ueledi wa kilimo, uchumi, lishe  na mazingira yanatakiwa kueleweka kwa waandishi wanaotaka kuelewa  masuala ya kilimo.
Tofauti na sekta nyingine kama vile afya ya binadamu, hakuna  kabisa  programu  ya uandishi wa  habari za kilimo miongoni mwa baadhi ya nchi  zinazoendelea, ambayo matokeo yake ni kwamba  kubobea kunafanywa  kutokana na uendelevu wa kuifanya kazi.
Waandishi wanaalikwa kwenye semina  kuhusu masuala ambayo ni magumu  na hushindwa kutumia  faida ya fursa hiyo kutokana na kutokuwa na  mwanzo mzuri wa  masuala ya sayansi au ufundi.
Lakini ufumbuzi wa hali kama hiyo unaweza kufanywa na taasisi kupitia semina mahsusi kwa vyombo vya habari ambazo mara nyingi hubebwa na wahariri wa vyombo na ambao huw ana nafasi ndogo  kujipa kazi ya kushughulikia masuala ya kilimo.
Hata hivyo tasisi zinaweza kuwa na vyombo vyake ya kujikita kwa kina katika kilimo kama ambavyo ilikuwa kwa Wizara ya Kilimo Tanzania ikiwa na gazeti la Mkulima wa Kisasa, kama bado lipo hakuna anayejua.
Kadhalika vilikuwepo vipindi vya redio  na mojawapo kikiwa na jina hilo pia kikirushwa na Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo sasa ni Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Hata hivyo mchango wa vyombo vya habari ni muhimu katika kuikuza sekta hiyo ikiwepo mikakati inayoviwezesha kufanya hivyo n kinachogomb hapo ni kujumuishwa katika hatua mbalimbali zinazoihusu.

Comments