Featured Post

KUHABARISHWA KATIKA UTANDAWAZI KUTAWANASUA WAKULIMA WADOGO



NA ALOYCE NDELEIO
UTANDAWAZI unalenga kuiweka dunia kwa ukaribu na kuifanya kama kijiji na hata hivyo hali hiyo haijaleta ufanisi kwa jumuia za wakulima wadogo na hususan kwa nchi zinzoendelea kutokana na kukabiliwa na vikwazo kadhaa.
Miongoni mwa vikwazo hivyo ni pamoja na kukosekana au kushindwa kupatikana kwa habari iwe za kuchapishwa au kutangazwa, umaskini ambao unakuwa hauruhusu kuwa na uwezo wa kununua vyombo vya kisasa kama vile televisheni, redio, kompyuta n.k ambavyo vitawawezesha kunufaika na utandawazi.

Aidha, kukosekana kwa miundombinu ya msingi kama vile kuwepo kwa umeme wa uhakika na njia nyingine za mawasiliano nako kunawaathiri wakulima.
Vikwazo wanavyokabiliwa navyo jamii ya wakulima pia vinawanafanya washindwe kufikia ugunduzi au ubunifu wa mbinu mbalimbali za kilimo.
Utandawazi unatafsiriwa kuwa ni kuongezeka kuunganika kwa dunia, kufungamana na kutegemeana katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, kijamii, kiteknolojia, kiutamaduni, kisiasa na kiikolojia.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia faida zinazotokana na utandawazi zinajumuisha kukua kwa uchumi, kuboresha viwango vya maisha, kupunguza umaskini, kuongeza kiwango cha kuishi na kukua kwa uhuru wa kidemokrasia.
Kutokana na mtazamo huo ni wazi kuwa utandawazi unajumuisha nyanja tofauti za shughuli za binadamu na mojawapo ni suala la uhakika au usalama wa chakula duniani.
Kwa mujibu wa Kamati ya Uhakika wa Chakula ya Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) inabainishwa, “Uhakika wa chakula unamaanisha chakula kinakuwepo muda wote hivyo kwamba watu wote wanakipata au kukifikia kikiwa na virutubisho vya kutosha katika nyanja ya ubora, wingi na aina tofauti na kwamba kinapatikana katika utamaduni unaokubalika.
“Aidha ni wakati ambapo hali zote hizo zinapokuwepo ndipo idadi ya watu inaweza kuelezwa kuwa ina usalama wa chakula. Lengo ni kujitegemea katika ngazi ya kitaifa na kaya. Katika kufanikisha huko mikakati ni lazima iwe kwenye misingi ya kanuni za kiuchumi, usawa, ushiriki kwa upana na matumizi endelevu ya maliasili.”
Hata hivyo kumekuwepo tishio dhidi ya uhakika wa chakula duniani kutokana na kushuka kwa uzalishaji wa chakula. Uhakika wa chakula ni mtazamo mkubwa wa utandawazi.
Ili kuwa na tija kwenye utoaji wa ongezeko la chakula, utandawazi umekuwa unakuza na kuhimiza biashara huria ambayo itahakikisha kuongezeka kwa ufanisi na kuboresha mazingira ya kiuchumi ya wakulima.
Inatarajiwa kuwa biashara huria inaweza kutoa fursa za kuongezeka kwa bei za mazao ya kilimo, kukuza hali ya kiuchumi ya wakulima, na kuboresha nyanja za utumiaji wa chakula.
Tanzania kwa upande wake ndani ya mazingira hayo Agosti 2009, Serikali ilisema, “... lipo suala zima la kuimarisha masoko ya mazao ili mkulima apate soko la uhakika na bei zenye tija kulingana na jasho lake.
“Kipimo cha mafanikio yetu kama taifa katika kufuta umaskini nchini kinategemea kilimo cha kisasa na cha kibiashara na sekta ya viwanda inayohudumia kilimo na kukuza ushindani wa Tanzania katika soko la dunia la utandawazi.”
Upatikanaji wa habari na ubunifu au ugunduzi unaohusiana na utendaji wa kilimo kwa wakulima wengi ni mdogo. Wakulima hutegemea maofisa ugani ambao wanakutana nao uso kwa uso ili kupata habari zinazohusiana na kilimo.
Kwa bahati mbaya idadi ya maofisa ugani ni ndogo hivyo inakuwa vigumu kwa wakulima kupata habari mpya kwani uwiano kati ya maofisa ugani na wakulima upo chini.

Kilimo, utandawazi na kuhabarishwa
Inatarajiwa kuwa utandawazi utapunguza uhaba wa chakula Afrika hivyo kujenga uhakika wa chakula kwa misingi ya faida linganifu.
Hali kadhalika inatarajiwa kuwa taifa linatakiwa kuzalisha mazao ambayo kwayo yana faida linganifu na itaagiza kutoka nje mazao ambayo haliwezi kuyazalisha kwa ufanisi kutoka kwenye nchi ambako mazao hayo yanaweza kuzalishwa kwa bei rahisi.
Utandawazi pia unaboresha kuunganishwa kwa mashamba madogo ya kilimo kwenye mashamba makubwa yanayotumika kilimo cha mashine. Dhana nyingine ni biashara huria na kuondoa ruzuku kwenye pembejeo kama vile mbolea za chumvi chumvi.
Ili kunufaika na utandawazi nchi nyingi zinazoendelea zimejiunga na Makubaliano ya Pamoja ya Biashara na Ushuru (GATT) na Shirika la Biashara Duniani (WTO). Katika mazingira hayo nchi nyingi za Afrika zimeshahurisha biashara ili kuweza kuuza bidhaa nyingi za kilimo.
Matokeo ya hali hiyo wakulima wengi wameacha kilimo cha mazao ya chakula na kuingia kwenye mazao ya biashara ambayo yatawawezesha kupata fedha nyingi kutoka kwenye soko la dunia. Hali hiyo ni tishio kwa uhakika wa chakula.
Kufungamanishwa kwa mashamba madogo ya kilimo kwenye kilimo cha mashine cha mashamba makubwa hakujawa na ufanisi kutokana na umiliki wa kina na wenye nguvu wa ardhi kwa wakazi wa Afrika.
Mtazamo huo unawezekana kuwa unatokana na kutoelewa faida zinazoweza kupatikana ambazo zitatoka kwenye kufungamana kwa sekta ya mashamba madogo na mashamba makubwa yanayoendeshwa kwa kilimo cha kutumia mashine.
Jambo jingine linalochangia ni uwezo mdogo wa kifedha miongoni mwa wakulima wengi wa Afrika wa kununua pembejeo za kilimo ambazo zingewawezesha kuongeza kasi ya uzalishaji wa chakula, hivyo serikali kuondoa ruzuku kwenye pembejeo za kilimo kumesababisha wakulima wengi kuachana na kilimo.
Sababu zote hizo kwa pamoja zinafanya uzalishaji kwenye kilimo kupungua. Hali kadhalika utandawazi unatarajiwa kutoa ufanisi na habari za papo hapo kwa shughuli yoyote.
Kutokana na hali hiyo inatarajiwa kuwa wakulima wadogo wataweza kupata ubunifu wa karibuni kuhusu shughuli za kilimo. Mchango wa Vituo vya Habari kwa wakulima  vinatakiwa kutoa habari za mara kwa mara kwa wakulima ili kuwajenga ufahamu mpana kwa kuzingatia kuwepo kwa kiwango kikubwa cha kutojua kusoma, tofauti za kiutamaduni na kukosekana kwa teknolojia.
Kwa mujibu wa Griffith na Smith kwenye mada iliyochapishwa kwenye Jarida la Academic Librarianship kuhusu Sera ya habari wanaelezea suala la habari duniani kuwa ni miundombinu ya simu ambayo inaunganisha kaya, shughuli za biashara, mashule, hospitali, maktaba vikiunganishwa pamoja na vyanzo kadhaa vya habari vya elektroniki.
Katika mazingira hayo miundo mbinu ya simu inajumuisha sehemu muhimu ya habari duniani.
Kwa mujibu wa Takwimu za Intaneti Duniani za mwaka 2006 Afrika ilikuwa na watumiaji wa simu milioni 33 ikilinganishwa na Ulaya ambako kulikuwa na watumiaji milioni 315 wakati Amerika ya Kaskazini ilikuwa na watumiaji milioni 233 na Asia ikiwa na watumiaji milioni 399.
Wakati Afrika ikiwa na asilimia 14.2 ya idadi ya watu duniani ina asilimia 3.0 ya watumaiji wa intaneti na hata hivyo kiwango chake cha kukua kwa matumizi hayo kati ya mwaka 2000 na 2007 kilikuwa ni kwa asilimia 638.4.
Kutokana na hali hiyo inatarajiwa kuwa matumizi ya intaneti yanaweza kupanuliwa hadi maeneo ya vijijini ambako ndiko makazi ya wakulima.
Hakuna shaka kwamba kuna pengo kubwa la teknolojia kati ya maeneo ya vijijini na mijini barani, lakini kusogezwa kwa mawasiliano ya simu kwenye maeneo hayo kunawezekana kama juhudi zitafanyika kuendeleza miundombinu ya mawasiliano vijijini.
Wakulima watanufaika kutokana na habari za dunia kama vituo vya habari vitakuwa vipo maeneo ya vijijini vikiwa na vifaa vyote vya habari na mawasiliano. Vifaa hivyo ni pamoja na kompyuta zilizounganishwa na intaneti, mitandao ya karibu na mipana, redio na televisheni, simu, mashine za nukushi, video na mashine za kurekodia.
Vituo kama hivyo vitatoa habari au vitahabarisha wakulima na inatarajiwa kuwa vituo hivyo vitatoa mafunzo kwa watalaamu wa masuala la maktaba na sayansi ya habari ambao watakuwa na jukumu la kukusanya habari sahihi kutoka kwenye intaneti, wizara husika za kilimo na mashirika yanayojihusisha na kilimo.
Aidha habari hizo zinatakiwa kurahisishwa na kuwa katika mazingira ambayo yanaweza kufikiwa na wakulima wasiojua kusoma. Vituo hivyo vinaweza pia kuwa na filamu au CD, kanda za kaseti zote zikilenga kuonesha uendeshaji wa kilimo cha kisasa kwenye maeneo mengine.
Pindi wanapoona vipindi vya aina hiyo wanaweza kutafsiri kile wanachojifunza kwa kuona na kukitekeleza kwa vitendo kwenye maeneo yao.
Licha ya kwamba kumekuwepo ukosoaji kuhusu utandawazi kwa upande mmoja kwamba hauna faida au haunufaishi Afrika lakini kwa upande mwingine kuna mambo yanayoweza kuwanufaisha wakulima wa Afrika kama kila mdau atatoa mchango wake.
CHANZO: FAHARI YETU

Comments