- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA ALOYCE NDELEIO
Mara nyingi watu wanapokuwa wamepiga kinywaji na kikawaingia
kama mpo kwenye mazungumzo jua yote yatakayozungumzwa yatakuwa na ukweli ndani
yake kwa asilimia zote.
Kutokana na hali hiyo upo msemo mmoja wa lugha ya
Kilatini unaosema ‘In vino veritas’ ambao kwa tafsiri rahisi ‘Ndani
ya mvinyo kuna ukweli’ kwa maana kwamba ni vigumu kwa mtu aliyekwishapata
kilevi kusema uongo.
Mara nyingi watu wa rika la kati walipokuwa wanataka kupata
wosia au busara kutoka kwa wazee wenye umri mkubwa wengi walikuwa
wanawanunulia kinywaji na hapo simulizi zilikuwa zinatolewa kwa mtiririko hivyo
kwamba kinywaji ndicho kinakuwa kimemrubuni mkongwe huyo.
Lakini mvinyo hapo unaweza kuwa ni kiashiria na kiwakilishi
cha kitu chochote kile ambacho kinaweza kumfurahisha au kinachoweza kutumika
kumrubuni ili kupata kitu au jambo fulani.
Mfano wajukuu wengi kwenye familia za ki-Afrika ambazo
zimezama kwenye utamaduni na mila (sio familia nyingi za sasa zilizosombwa
utapiamlo wa kiutamaduni kwa kubugia utandawazi) wamekuwa wakizawadiwa mali na
babu zao kutokana na kufurahishwa na zawadi ambazo wamekuwa wakipata
kutoka kwao.
Madaraka au mamlaka yanaweza kuwa kama mvinyo wenye kulevya
na hivyo kuwafanya waliopewa madaraka hayo kulemaa na kutoa kauli ambazo kwao
wanaziona ni sahihi lakini kwa upande mwingine zinaonekana kuwa sivyo.
Lakini baadaye inaweza kubainika kuwa hiyo ndio kweli
aliyoisema na aliisema akiwa amedhamiria.
Inapotokea kwamba mzito anatoa kauli kwamba hakuna Mtanzania
mwenye uwezo wa kuwekeza kwenye uchimbaji wa gesi asilia na kwamba kampuni
zao zina uwezo wa kusindika juisi moja kwa moja anaonesha kulewa mvinyo
wa madaraka ambapo mara nyingi huishia kudharau hata kule walikotoka.
Hali hiyo inamaanisha kuwa ile dhana ambayo inaelezwa na
wataalamu wa sayansi ya siasa kwamba tumekuwa tunajianika uchi kwa kufanya uza
uza ya kila kitu hapa ina mashiko.
Aidha ile dhana kwamba kasi ya uwekezaji ni kwa wawekezaji
wa nje hapa nayo inajidhihirisha. Mazingira ya aina hiyo inaonesha ni
jinsi gani na kwa namna gani jamii itakavyokuwa wasindikizaji kwenye
kuzionja tamu za rasilimali zilizopo nchini.
Kama hali ndio hivyo leo hii hakuna cha kushangaza kuhusu
utajiri wa baadhi ya wazito kwani hayo ni matokeo ya mambo ambayo Mwalimu
Julius Nyerere aliyazuia sana wakati wa uongozi wake (1962 – 1985).
Mwalimu aliita “miujiza” ya aina hiyo ni “ulevi wa madaraka”
na ni matokeo ya Azimio la Zanzibar (1992) lililofuta Miiko ya Uongozi katika
Azimio la Arusha (1967).
Pia ni matokeo halisi ya yale yanayoelezwa na taasisi ya
kimataifa iitwayo Transparency International (TI) kwa Kiingereza kuwa ni “Grand
Corruption” yaani “Rushwa Kabambe” au ufisadi kwa neno maarufu lililokita ndani
ya jamii hivi sasa.
TI imeeleza rushwa kabambe kwa Kiingereza kuwa ni: “Misuse
of entrusted power for private gain”. Tafsiri yake: “Matumizi mabaya ya
madaraka kwa maslahi binafsi”.
Haieleweki ni kwanini watu wanashangaa leo kuhusu taarifa
kwamba kuna watu walioficha fedha nje ya nchi na kuibuka kwa kebehi za kuzitaja
fedha hizo kwamba ni vijisenti.
Haiyumkini kwamba kujishangaa huko kunatokana na kuwapa
madaraka makubwa na badala ya kuitumikia jamii wamekuwa wanajitumia wao wenyewe
kwa maslahi yao.
Kwenye kumbukumbu za Bunge kuhusu hoja ya rasilimali
Mbunge wa Bariadi Magharibi Februari 12, 2004 akiwa Dodoma alisema,
“Niseme tu hapa Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ina utajiri mkubwa sana wa
madini. Kwa taarifa tu za utafiti uliofanywa, mkienda hapa Ofisi yetu ya Madini
hapa, ukiomba wakuonyeshe ‘geological data’ iliyopo kwa nchi nzima, utasema
kweli tunachofanya sasa hivi ni kidogo mno.
“Lakini narudia kwamba Watanzania hatuwezi kuendelea kila
siku tunasema, tuna potential nzuri sana. Hatuwezi kuishi kwa kula potential.
Madini haya lazima tuyatafute kokote yalipo, tuyapate, tuyachimbue,
tuyasafishe, tuya-process na kisha tuweze kuyauza na tutumie mafao yanayotokana
na mauzo hayo kwa faida ya maendeleo ya nchi yetu na watu wake....
“Lakini madini yaliyopo siyo madini ya dhahabu peke yake au
almasi au vito, yapo madini mengi sana, madini ya vyuma, mkaa wa mawe na odium,
unaweza kusema uranium na mengine yote mpaka kule maeneo ambayo yana madini
mengi tunayafahamu lakini kwa leo mimi nasema tunaboresha maeneo haya...”
Kwa nukuu hiyo ni dhahiri kwamba rasilimali zilizopo nchini
thamani yake inapanda kila siku kutokana na kugundulika kuwepo kwa kiwango
kikubwa. Kimsingi madini hayo hayaozi.
Ardhi nayo haionekani kuwa nzuri kwa kilimo kama ambavyo
ingetarajiwa lakini kwa kuwa wageni wanaona utajiri wa rasilimali hiyo kwenye
uzalishaji wa mazao na hususani kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji na kwamba
mazao yanaweza kuzalishwa mwaka mzima wapanga sera nao wamekuwa wanadanganyika
kwa kuwapa maeneo makubwa kwa ajili ya uwekezaji.
Katika mazingira hayo ni wazi kuwa haitashangaza kuona kuwa
hata huduma na bidhaa ambazo zitakuwa zinazalishwa kutokana na uwekezaji huo
hapo baadaye na hata zitakazokuwa zinabakia ndani kwamba zitaangukia mikononi
mwa watu wasio wazawa au mikononi mwa tabaka la walioonja pepo.
Ukweli unabakia kuwa ili kuelewa hali halisi ya uchumi wa
nchi hii ni vyema kufahamu ni kwanini tuna uelewa duni wa utambuzi kuhusu
umuhimu wa rasilimali za asili na pia inatakiwa kufahamu ni kwanini
sehemu kubwa ya utajiri huo unaangukia kwenye mikono wageni ambao kwa
ujumla wanaishi nje ughaibuni.
Katika kurejea kwenye historia ni kwamba tangu zamani ndani
ya jamii walikuwepo wanajeolojia ambao walikuwa wanafahamu miamba
iliyokuwa na dhahabu pamoja na shaba.
Wakati wazungu wanafika kwenye karne ya 19 waligundua kuwa
miamba yote iliyokuwa shaba au dhahabu ilikuwa imeshachimbwa na wajamii japo
sio kwa kiwango kikubwa kama ambavyo wazungu walifanya kwa kutumia zana zao za
kisasa.
Katika mazingira hayo kinachojitokeza hivi sasa ni kuona
kuwa wazawa kwamba hawana uwezo ni hatua ya marudio ya kihistoria kwamba
wawekezaji wa nje ndio wanaoweza tu.
Aidha hali hiyo tayari inaonesha ni jinsi gani wapanga sera
wetu jinsi ambavyo fikra zao zimeshatekwa au kuuzwa ughaibuni.
Haiyumkini kwamba ni vyema kuchukulia kauli za wataalamu wa
masuala ya maendeleo na uchumi kwamba bara la Afrika ndilo litakalokuja
kuchipukia na kuongoza kwa maendeleo kwa kuwa rasilimali zake nyingi
hazijaguswa.
Kauli hiyo inamaanisha rasilimali hizo ziondoe umaskini wa
watu wake ndipo maendeleo hayo yatapatikana. Lakini kwa upande mwingine
hao wawekezaji kutoka nje nao walishaliona hilo na ndio maana kila mahali
zinapoibuliwa rasilimali huanza kupigana kumbo kwenda kuwekeza na wanapoingia
na kuwakuta watu wake wamejilegeza basi huutumiwa mwanya huo vizuri kupoka
rasilimali hizo.
Lakini ni vyema ikiwa wapanga sera watabaini kuwa mamlaka
yao wameyatumia vibaya wakaja baadae na msemo huu wa kilatini “mea culpa, mea culpa, mea
maxima culpa” kwamba “nimekosa
mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana”.
CHANZO: FAHARI YETU

Comments
Post a Comment