- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Katibu Mkuu Kiongozi nchini, Balozi
Mhandisi John Kijazi akitoa maelekezo kwa jopo la Madaktari Bingwa na Uongozi wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili pamoja na Taasisi ya Mifupa ya MOI ambao wanamtibu
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (Aliyeketi) alipomtembelea mapema leo Agosti
28,2018, Wodi ya Kitengo cha Mifupa MOI.
Katibu Mkuu Kiongozi nchini, Balozi Mhandisi John Kijazi
akishuhudia picha ya X ray inayoonesha eneo la mkono wa kushoto wa
Waziri Dkt. Hamisi Kigwangalla anayepatiwa tiba MOI namna unavyoendelea.
Aliyeshika Xray ni Mkurugenzi Mtendaji
wa MOI Dkt Respicious Boniface, wengine
ni Mkurugenzi mtendaji wa
Muhimbili, Profesa Laurence
Museru na Mkurugenzi wa Tiba MOI Dkt. Samuel Swai. Mapema leo Agosti 28,2018,
Wakati alipomtembelea Wodi ya Kitengo cha Mifupa MOI.
Katibu Mkuu Kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Balozi Mhandisi John Kijazi leo tarehe
28/08/2018 amemtembelea na kumjulia hali Dkt Hamisi Kigwangalla ambaye anapata
matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI akiuguza majeraha ya mkono aliyopata
katika ajali iliyotokea Agosti 4, mwaka huu Mkoani Manyara.
Balozi Kijazi amempa pole Mh Dkt. Kigwangalla na kumtakia
heri na apone haraka ili aweze kurejea kwenye majukumu yake ya kila siku kwani Taifa linauhitaji mchango wake.
“Pole sana. Mungu
atajalia utapona na utarejea nyumbani mapema, na kwa kuwa wewe ni daktari
ukiona hali si nzuri utawafahamisha wenzio mapema ili mjadiliane namna ya
kuikabili hali itakayojitokeza” Alisema Balozi Kijazi wakati wa kumjulia pole
Hospitalini hapo.
Aidha, Balozi Kijazi amemueleza Mkurugenzi Mtendaji wa MOI,
Dkt. Respicious Boniface kwamba kwa sasa wananchi wanaridhishwa na huduma
zinazotolewa na MOI na Muhimbili kwa ujumla na hii ni faraja kubwa kwa Serikali
na hivyo kuelekeza ari hiyo iendelezwe.
“Pamoja na Jitihada kubwa za Mh Rais Dkt John Pombe Magufuli
za kuboresha huduma za Afya hapa nchini, nanyi pia kwa upande wenu mnajitahidi
sana na wananchi wanaridhishwa na huduma mnazotoa. Nafahamu kuna changamoto
chache lakini bado mmeendelea kufanya kazi nzuri” Alisema Balozi Kijazi.
Kwa upande wake, Dkt. Hamis Kigwangalla amemshukuru Balozi
Kijazi kwa kumtembelea na kumjulia hali na amemueleza kwamba afya yake
imeendelea kuimarika na anaamini katika kipindi kifupi kijacho madaktari
watakapojiridhisha wanaweza kumpa ruhusa ya kutoka hospitalini.
“Ninaendelea vizuri, afya yangu inaimarika siku hadi siku,
na pia naendelea na mazoezi na kila siku najiona imara zaidi na hii ni ishara
tosha kwamba ninaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani,” alisema Dkt. Kigwangalla.
Dkt. Kigwangalla alihamishiwa katika Taasisi ya Tiba ya
Mifupa MOI tarehe 12/08/2018 baada ya kupata matibabu ya awali katika hospitali
ya Taifa ya Muhimbili na kwa sasa bado anaendelea na tiba kuuguza mkono wake wa
kushoto.


Comments
Post a Comment