- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA DANIEL MBEGA
SHIRIKA la Ndege Tanzania (ATCL)
limerudi katika enzi zile za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye ndoto
zake zilikuwa kuona Tanzania inajiimarisha katika usafiri wa anga kwa ajili ya
kukuza uchumi na kuimarisha usalama wake.
Tangu Serikali ya Awamu ya Tano
chini ya Rais Dkt. John Magufuli iingie madarakani Novemba 5, 2015, jitihada
kubwa zimeonekana katika kulifufua shirika hilo lililokuwa likikabiliwa na
madeni mengi huku likiwa halina hata ndege moja.
Wapiga dili waliligeuza
kitegauchumi chao, ambapo ilifikia mahali hata sare za wahudumu zilishoneshwa
ng'ambo kwa mamilioni ya shilingi, fedha halali za walipa kodi na wavuja jasho
wa Tanzania.
Tayari mpaka sasa ATCL inazo ndege
nne - tatu ni Bombardier DHC-8-Q400 NG na moja ni Boeing 787-800
Dreamliner 5H-TCG - ambazo tayari zinafanya safari sehemu mbalimbali katika
miji ya Bukoba, Dodoma, Kigoma, Kilimanjaro, Mbeya, Mwanza, Tabora, Zanzibar,
Mtwara, Songea, Dar es Salaam na Moroni visiwani Comoro wakati ambapo safari za
kwenda Mumbai, India na Guangzhou, China zinatarajiwa kuanza mwezi Septemba
mwaka huu 2018.
Ndege hizi ni sehemu ya ndege
sita ambazo Serikali imepanga kununua kwa fedha taslimu, ambapo ndege mbili
zaidi zinatarajiwa kuwasili nchini Novemba 2018.
Ujio wa ndege hizi umerejesha
heshima ya Tanzania katika usafiri wa anga tofauti na ilivyokuwa nyuma ambapo
siyo tu serikali ilikuwa ikikosa mapato kwa kushindwa kusafirisha abiria,
lakini hata kiusalama haikuwa vizuri kwa kuwa ndege zilizokuwa zikifanya safari
ni za binafsi.
Leo hii Watanzania wanafurahia
safari za ndani zenye uhakika, tena kwa gharama nafuu kulinganisha na mashirika
ya binafsi, hatua ambayo imewafanya wawe na imani kubwa na serikali ya sasa.
Kelele za wapinzani
Licha ya
jitihada hizo zinazofanywa na serikali, lakini wapinzani wanaendelea kubeza
kila kinachofanyika, huku wakisahau kwamba ni ATCL hiyo hiyo ambayo ilikuwa
ikiingizia Serikali hasara kubwa kwa kukodi ndege kuu kuu na Tanzania kushindwa
kuwa na ndege zake yenyewe ambayo ni alama ya utaifa na uzalendo.
Wapinzani
wanasema kwamba, ATCL inabebwa kwa nguvu kwa sababu ya mtazamo alionao Rais
Magufuli, lakini halibebeki.
Wanakejeli
kwamba, kuongezeka kwa ndege hizo maana yake ni kuwa gharama za kuendesha shirika
nazo zinaendelea kuongezeka hata kama ni kwa kulibeba.
Wengine
wanasema eti hizi ndege zilizopo zinaweza zisitosheleze iwapo kweli tunanuia
kuruka kimataifa hivyo huenda huko baadae tukalazimika kuongeza ndege zingine
na hii itakuwa ni gharama nyingine.
Kweli hali
itakaporuhusu itabidi kuongeza ndege nyingine kwa sababu huo ndio uhakika wa
kujiimarisha kimataifa na kuwa na uhakika wa kuingiza wageni wengi, wakiwemo
watalii na wawekezaji.
Wapo
wanaosema ni bora kuuza ndege zote na kujiimarisha kwenye usafiri wa reli,
lakini unawashangaa watu kama hao vichwa vyao vikoje kwa sababu hatuna treni
inayoweza kwenda nje ya nchi, ikiwemo Ulaya.
Binafsi
ninawaunga mkono wanaosema suala siyo ndege, bali ni uendeshaji wa shirika, na
hilo ndilo ambalo Serikali ya Magufuli inalifanyia kazi.
Tunapaswa
kujiuliza pia kama kweli shirika letu halikuwa linahujumiwa, life ili watu
wengine waingize midege yao na kuchukua ukanda katika usafiri wa anga.
Twende
ndani tukachunguze na kuona ni akina nani wanamiliki mashirika yaliyofumuka
tangu mwaka 1997, huku ATCL ikifilisika na kukodishwa kabla ya kuchungulia
kaburi.
Haitashangaza
hata mara moja kukuta kwamba wapo vigogo waliopata kuwa na nyadhifa za juu za
maamuzi serikalini, ambapo hata mashirika hayo ya binafsi yalianzishwa wao
wakiwa madarakani.
Kumiliki
ndege ni gharama, hilo halina ubishi na hasa suala la matengenezo, lakini
hatuwezi kukwepa kununua ndege eti kwa sababu ya gharama, vinginevyo hatuna
haja hata ya kufanya kazi au kuweka akiba kwa sababu sote ipo siku tutakufa!
Tukitaka
ATCL iimarike na itengeneze faida baadaye, lazima kuja na mkakati wa kupambana
na ushindani katika bei badala ya kuweka nauli za juu, kwa sababu hiyo ndiyo
itakuwa silaha kubwa ya kujiendesha, achilia mbali silaha ya msingi - Uzalendo!
Ndoto ya Mwalimu
Anachokifanya
Rais Magufuli ni kufufua ndoto ya Mwalimu Nyerere aliyelianzisha shirika hilo
miaka 41 iliyopita, na kamwe hakukosea.
Ilikuwa
Ijumaa, Machi
11, 1977 wakati Shirika la Ndege Tanzania (ATC) linaanzishwa, Rais wa wakati
huo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alikuwa na ndoto za kuona Tanzania
inajiimarisha katika usafiri wa anga.
Usafiri wa anga wakati huo ulikuwa
umesimama kwa muda baada ya kuvunjika kwa Shirika la Ndege la Afrika Mashariki
(EAA) kufuatia kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka huo, kwani EAA
ilimilikiwa kwa pamoja na Kenya, Tanzania ya Uganda.
Itakumbukwa kwamba, baada ya
kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, usafiri wa anga kwa kiasi kikubwa
ulikuwa mikononi mwa Kenya, wakati Tanzania yenyewe ilibaki na usafiri wa reli.
Kwa maana nyingine, Kenya, ambayo
ilikuwa imeanzisha Shirika lake la Ndege (Kenya Airways), ndiyo iliyokuwa
ikitawala usafiri wa anga wakati huo.
Jambo hili lilimfanya Mwalimu
Nyerere aone umuhimu wa kuanzisha haraka Shirika la Ndege Tanzania na mara tu
ATC ilipoanzishwa, serikali ikakodi ndege yake ya kwanza aina ya Douglas DC-9-32, 5Y-ALR (ambayo ilikuwa miongoni mwa zilizokuwa ndege za
EAA) kutoka Kenya Airways.
Mwaka huo huo zikapatikana ndege
nyingine ndogo mbili, DC-9-32 5Y-ALR na Fokker F27-600, PH-EXC c/n
10566 iliyotoka Schiphol, Uholanzi.
Baadaye zikapatikana ndege
nyingine aina ya DeHavilland Canada DHC6 Twinn Otter 300 5H-MRB c/n 579 mwaka
1978 na Boeing 720-022 N62215 ilikodishwa mwaka 1979 kutoka Caledonian
Airlines INC, lakini ATC ililazimika kuvunja mkataba huo miezi mitatu baadaye
kutokana na mkodishaji kupunguza idadi ya abiria waliopaswa kusafirisha, ni
abiria 28 tu.
Katika miaka hiyo Enzi za Mwalimu hasa mwaka 1980-1981, ndege za ATC zilifanya safari nyingi za kitaifa na kimataifa kwa kutumia ndege zake za Boeing 707 na 737 na Fokker kutoka Dar es Salaam hadi Athens - Ugiriki (707), Antanarivo - Madagascar (737), Bombay - India (707) Bujumbura - Burundi (737), Cairo - Misri (707), Frankfurt - Ujerumani (707), Kigali - Rwanda (737), London Gatwick - Uingereza (707), Mahe - Shelisheli (737), Maputo - Msumbiji (737), Mauritius (737), Moroni - Comoro (FKF), Muscat - Oman (737) na Rome - Italia (707).
Katika miaka hiyo Enzi za Mwalimu hasa mwaka 1980-1981, ndege za ATC zilifanya safari nyingi za kitaifa na kimataifa kwa kutumia ndege zake za Boeing 707 na 737 na Fokker kutoka Dar es Salaam hadi Athens - Ugiriki (707), Antanarivo - Madagascar (737), Bombay - India (707) Bujumbura - Burundi (737), Cairo - Misri (707), Frankfurt - Ujerumani (707), Kigali - Rwanda (737), London Gatwick - Uingereza (707), Mahe - Shelisheli (737), Maputo - Msumbiji (737), Mauritius (737), Moroni - Comoro (FKF), Muscat - Oman (737) na Rome - Italia (707).
Kuanzia kiangazi cha mwaka 1981,
safari zilifanywa kwa kutumia ndege ya Boeing 707-320 (N762TW c/n 17675
"Ngorongoro Crater") kwenda Misri-Ulaya, Dubai-Pakistan-India ingawa
safari hizo zilivunjwa baada ya ndege hiyo kupata ajali kwenye uwanja wa ndege
Dar es Salaam.
Kulikuwa na safari nyingi za
ndani kutoka Dar es Salam hadi Bukoba (DHT), Dodoma (DHT/FKF), Iringa (DHT),
Kigoma (737), Kilimanjaro (707/737/DHT/FKF), Kilwa (DHT/FKF), Lindi (FKF), Mafia
(DHT), Masasi (DHT), Mbeya (DHT), Mtwara (737/DHT/FKF), Musoma FKF), Mwanza
(737/FKF), Nachingwea (FKF), Njombe
(DHT), Pemba (DHT/FKF),Songea (FKF), Tabora (FKF), Zanzibar (DHT/FKF).
Safari nyingi za ndani
ziliongezeka kwa kutumia ndege za Boeing 737-2R8C (Adv) 5H-ATC c/n 21710
"Kilimanjaro" na Fokker F27-600RF Friendship 5H-MPU c/n 10569 na
Serikali ikaongeza ndege ya De-Havilland Canada DHC-6 Twin Otter 5H-MRC kwa
ajili ya safari za ndani kutoka Kilimanjaro.
Na tunakumbuka jinsi ndege yetu
ya 5H-ATC Boeing 737-2R8C ilivyotekwa mara mbili - mara ya kwanza
Februari 26, 1982 kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza wakati ikiruka kwenda Dar es
Salaam ambapo akina Mussa Membar na wenzake waliiteka kwa kutumia bastola
bandia na kuipeleka London, Uingereza.
Mara ya pili ilikuwa Februari 13,
1988 wakati watekaji wawili walipoiteka kwenye Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam
ikijiandaa kwenda Nairobi wakitaka ndege hiyo iwapeleke Stanstead, Uingereza.
Tukio hilo lilidumu kwa siku mbili na watekaji walikamatwa baada ya ndege
kuzingirwa.
Baada ya Mwalimu
Tangu Mwalimu Nyerere alipoondoka
madarakani na hasa baada ya ndege kadhaa za ATC kuharibika kutokana na ajali na
uchakavu, shirika hilo likaanza kuyumba na kupoteza kabisa mwelekeo.
Kwanza, kati ya mwaka 1991 na
1992 Serikali ikakodisha ndege ya Boeing 767-200 ET-AIZ kutoka Shirika
la Ndege la Ethiopia lakini ndege hiyo ilionekana kuwa kubwa zaidi na haikuwa
na maslahi, hivyo ikabidi irudishwe kwa wenyewe.
Mnamo Desemba 12, 1993, ndege ya 5H-MPT
Fokker F27 ilianguka wakati ikitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Dar es Salaam. Ndege hiyo ikaondolewa kwenye orodha na ikatumika kwa vipuri tu.
Mnamo mwezi Mei 1994, kampuni ya
Shannon Aerospace ya Ireland ilikodishwa kuzitengeneza ndege mbili za
Boeing 737-200C, ndege tatu za De Havilland DHC-6 Twin Otter 300 na
ndege tatu za Fokker F27-600.
Lengo la ATC lilikuwa kufufua
ndege hizo ili zichukue nafasi ya ndege kongwe ya Boeing 737 kwa kutumia
model mpya ya Fokker F27 na mbili za Fokker 50.
Wakati huo safari za kimataifa
zilikuwa Bujumbura, Djibouti, Entebbe, Gaborone, Harare, Johannesburg, Kigali,
Lilongwe, London, Lusaka na Muscat. Safari za Johannesburg zilifanywa na Air Malawi
kwa niaba ya ATC.
Ni katika kipindi hiki ambapo ATC
iliingia katika mazungumzo ya kuwa na hisa asilimia 10 kwenye Ushirikiano wa
Pamoja na Shirika la Alliance Air (baadaye ikajulikana kama SA Alliance),
shirika la ndege ambalo lilikuwa na makao yake kwenye Uwanja wa Ndege wa
Entebbe, Uganda.
Makubaliano hayo yakafikiwa mwaka
1994 kati ya ATC, Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) na Shirika la Ndege
la Uganda kwa lengo la kushindana na mashirika ya ndege ya kimataifa. Ushirika
huo ulikuwa na ndege moja aina ya Boeing 747SP-44, ZS-SPA cn 211321/280 iliyokodishwa
kutoka Shirika la Ndege la Afrika Kusini ambapo ilifanya safari zake kati ya
Afrika Mashariki na Ulaya.
Ubia huo ulikoma Oktoba 2000,
baada ya kuingia hasara ya Dola za Marekani milioni 50.
ATC ilibinafsishwa mwishoni mwa
mwaka 1998 na mipango ya kuiunganisha moja kwa moja na Alliance Air
ilishindikana. Shughuli za Alliance Air zilikoma mwaka 1999 kutokana na mzigo
mkubwa wa madeni. Wakati huo Alliance Air ilikuwa ikifanya safari zake kati ya
Dar es Salaam, Kilimanjaro na London - Heathrow kutoka Uwanja wa Ndege wa
Entebbe.
Kutokana na hilo, mipango ya
kulibinafsisha shirika la ATC likabaki chini ya serikali kama ilivyokuwa awali.
Wakati huo huo, ndege ya Boeing
737-200, 5H-ATC ilitakiwa kufanyiwa uchunguzi (C-check), ATC ikakodisha ndege
ya Boeing 737-300 XA-SWO c/n 27284 "Ngorongoro" kutoka
Transportes AƩreos Ejecutivos (TAESA) ya Brazil kwa kipindi kifupi.
Ndoa ya ATC, SAA
Mnamo Februari 2002, serikali
ikaanza mchakato wa kulibinafsisha shirika la ATC kwa kutangaza zabuni kwenye
magazeti ya ndani na kimataifa. Mashirika manne kati ya manane yakaingia kwenye
mchakato huo ambayo ni Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA), Kenya Airways, Shirika
la Ndege la Comair Afrika Kusini) na Nationwide Airlines pia la Afrika Kusini.
SAA ikashinda zabuni hiyo na
mwezi Desemba 2002 wakasaini mkataba ambapo serikali ilikuwa na asilimia 51 ya
hisa kwenye ATC.
Kwa bahati mbaya, ndege mbili za Boeing
737-2R8C(Adv) - 5H-ATC na 5H-MRK zikaondolewa kwenye huduma na
kupelekwa Afrika Kusini. SAA ilikuwa na mpango wa kununua ndege za Boeing
737-800 lakini badala yake ikanunua ndege kuu kuu za Boeing 737-200, mbili
za Fokker F-28 na mbili za De Haviland Dash 8-315.
Mnamo Januari 31, 2005, ATC
ikafuta moja kati ya safari zake za kimataifa kutoka Dar es Salaam kwenda
Nairobi, Kenya, kutokana na ushindani mkubwa kutoka Kenya Airways.
Mwaka huo huo ATC ikatangaza
kupata hasara ya Dola milioni 7.3 katika mwaka wake wa kwanza wa ubia na SAA,
hasara ambayo ilichangiwa na kushindwa kupanua safari zake kwani awali ilikuwa
imepanga kupanua safari zake kwenda Dubai, India na Ulaya lakini ikashindikana
kwa kuwa ndege pekee walizokuwa nazo ni Boeing 737-200 ambazo pia
zilikuwa kuu kuu.
Septemba 7, 2006 Serikali ikanunua
asilimia 49 kwenye ATC kwa gharama ya Dola milioni 1, hali iliyomaanisha
kuvunja mkataba na SAA.
Mkataba huo ulivunjika kutokana
na haja tofauti za wanahisa. Ndege mbili za Boeing 737-247 Adv, 5H-MVV na
5H-MVZ zilikuwa zimekodishwa kutoka Celtic Capital Air Corporation, Canada kwa
miaka miwili kwa gharama ya Dola 50,000 kwa mwezi.
Mnamo Septemba 2007 kampuni ya
Air Tanzania Company Limited (ATCL "Wings of Kilimanjaro")
ilianzishwa baada ya kuvunjwa kwa mkataba na SAA na ilikuwa na safari za Dar es
Salaam kwenda Mwanza kupitia Kilimanjaro.
Mnamo Oktoba 2007 ATCL ikakodisha
ndege ya Airbus A320 kutoka kampuni ya Wallis Trading Company kwa muda wa miaka
sita.
Ukodishaji huo ulikuwa sehemu ya
mchakato wa ubia, ambapo ATCL ilikuwa iuzwe kwa hisa kwa kampuni ya Sonangol ya
China, ambayo haikuwahi kusaini mkataba wowote rasmi wa makubaliano na serikali
ingawa ilikuwa imeahidi kuinunulia ATCL ndege tano za Airbus hadi kufikia mwaka
2012 kama sehemu ya mpango wa ubinafsishaji.
Kwa kujua kwamba walikuwa
wanaingia mkataba na Sonangol, menejimenti ya ATCL ikaharakisha kukodisha ndege
ye A320-214 kutoka Wallis Trading, kampuni ambayo ilikuwa imedai kuwa na
uhusiano na Sonangol ya China iliyoongozwa na mfanyabiashara wa Hong Kong, Sam
Pa. Ndege hiyo ilikuwa imefanya huduma Liberia ambako ndiko ilikokodishwa,
lakini kabla ilikuwa imekodishwa huko El Salvador.
Lakini wakati ATCL inaingia
mkataba wa kuikodisha Oktoba 2007 ndege hiyo ilikuwa inatakiwa kufanyiwa
ukaguzi (C-check) ndani ya miezi sita, hivyo kuingia katika hasara nyingine.
Iliporejea kutoka kwenye matengenezo Mei 2008, ndege hiyo iliruka angani kwa
miezi saba tu hadi Desemba 2008 wakati ilipoegeshwa ili ifanyiwe matengenezo
mengine ya D-ckeck na haikuwahi kuruka tena angani, hadi ilipokodishwa na ATCL
Oktoba 2011. Hiyo ilikuwa ni miaka miwili kabla ya mkataba wa ukodishaji
kumalizika lakini gharama za ukodishaji zikabakia pale pale kana kwamba ndege
ilikuwa ikifanya kazi katika muda wote wa mkataba.
Hali hii inadhihirisha namna
ufisadi ulivyokuwa ikifanyika kiasi cha kulifilisi shirika hilo.
Mwaka 2008 ATCL ilikodisha ndege
za 5H-MWH Airbus A320-214 c/n 363, 5H-MVV Boeing 737-247 Adv c/n 23520, 5H-MVZ
Boeing 737-247 Adv c/n 23607, 5H-MWF De Havilland Canada DHC-8Q-311 DASH 8 c/n
475, na 5H-MWG De Havilland Canada DHC-8Q-311 DASH 8 c/n 462.
Tangu wakati huo hali ikawa mbaya
zaidi kwa sababu Januari 2009 ndege mbili za Airbus A320 na Boeing 737
zikaondolewa katika utoaji huduma.
Kwahiyo, ujio wa Magufuli
umelifufua shirika hili ambalo lilikwishakufa kwa sababu ya 'upigaji wa dili'
na sasa heshima ya Tanzania imerejea kama Mwalimu Nyerere alivyokuwa akitamani
kuliona.
0656-331974





Comments
Post a Comment