Featured Post

FURSA ZA ELIMU KWA WALEMAVU NJIA MWAFAKA YA KUWAWEZESHA



NA MWANDISHI WETU
Miongoni mwa Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs) lengo namba nne ni kuhakikisha  unakuwepo ujumuishi  na uwiano wa elimu bora  na kuboresha fursa za kujifunza maishani kwa wote.
Hali kadhalika zimekuwepo kauli mbiu zinazoweka wazi kuwa elimu ndio ufunguo wa maisha, kuwekeza katika elimu ni kuwekeza katika ustawi wa jamii  pamoja na nyingine zinazosisitiza umuhimu wa elimu katika maendeleo.

Kwa kuzingatia hilo ni dhahiri kuwa haki ya elimu kwa wote  ni lazima ifikishwe kwa  watoto, vijana na hata watu wazima  walio na ulemavu.
Ndani ya mtazamo huo  ni kwamba walemavu wanatakiwa wawe na fursa ya kusimamia maisha yao kuliko kuwa watu wa kuangaliwa kimyakimya au kupewa uhisani.
Hili linajiweka karibu na fikra za hivi sasa kuhusu haki kwa msingi wa mtazamo wa maendeleo, ambako kunaongeza kuridhiwa na serikali na mashirika ya maendeleo ya kimataifa duniani kote.
Hali hiyo pia inamaanisha kuwa mizizi ya umasikini na kukosa nguvu,  ni jambo ambalo haliko kwenye mkondo wa biolojia bali ni katika jamii na linaweza kufanyiwa mageuzi.
Aidha, mtazamo wa haki za binadamu kwa maendeleo unatoa fursa kwa mageuzi ya kiutamaduni na kijamii. Hali kadhalika unatoa mwanya kwa watu walemavu kuwa na dhana ya mtazamo wa namna wanavyojiona kutoka kwenye dhana ya kunyanyapaliwa na kuingia kwenye mtazamo wa kuthaminiwa maisha yao.
Ufanisi katika njia hiyo ni  kupitia elimu  na ndio maana  sera za taifa za maendeleo ya elimu  zinajumuisha  mtazamo jumuishi  ambao umekuwa unajadiliwa   na serikali pamoja na jumuia ya wahisani kimataifa.
Mfano hai ni Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (Mkukuta) ambao miongoni mwa malengo ya uendeshaji wake  katika  nyanja ya elimu  ni pamoja na kuongeza uandikishaji wa watoto walio na ulemavu  shuleni.
Kwa mujibu wa Mkukuta 2005, inabainishwa kuwa uwiano wa watoto  walio na ulemavu  wanaoandikishwa  na wale  wanaohudhuria  na kumaliza elimu  unalenga kuongezeka kutoka  asilimia 0.1 ya mwaka 2000 kufikia  asilimia 20 mwaka 2010.
Hata hivyo bila kuwajibika kisheria  na kuwepo kwa bajeti lengo hilo halitafikiwa hivyo kundi hili la jamii kuwa limesokomezwa pembezoni na kutopea katika umaskini.
Shirika la Elimu Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) linasema, “Ujumuishi unaonekana  kama hatua ya kuangalia na kuwajibika kwa anuai ya mahitaji  ya wote wanaojifunza  kwa kuongeza ushirikishwaji wa kujifunza, utamaduni na jumuia na kupunguza kutengwa kwenye elimu.
“Unahusisha mabadiliko na kuboreshwa kwenye yaliyomo, mtazamo, muundo na mikakati kukiw ana dira ya pamoja  ambayo inahusisha watoto wote  walio na miaka  inayotakiwa na kuufanya kuwa ni jukumu lililo kwenye mfumo wa kawaida wa elimu kwa watoto wote...ujumuishi unamaanisha kutambua na kuondoa vikwazo...”
Kwa upande wa Tanzania ni kwamba imeshajipambanua  kuhusu haki ya watoto walio na ulemavu kwamba lazima wapate elimu kulingana na mahitaji yao kupitia Azimio la Haki ya Mtoto la mwaka 1990, na Azimio la Afrika la Haki za Mtoto la mwaka 2003 na Sera ya Elimu ya mwaka 1996.
“...watoto walio na ulemavu  lazima wajumuishwe kwenye shule za kawaida, karibu na nyumbani hivyo kwamba wanashirikiana rasilimali ya shule na uzoefu wa pamoja na wenzao  ambao sio walemavu.”
Pamoja na hali hiyo Tanzania imelipokea  azimio jipya la Haki ya Watu walio na Ulemavu la  Machi 30, 2007. Kifungu namba 24 cha elimu kinasema, “Idara za serikali zitambue hali ya walemavu kupata elimu.
Hili linatakiwa kuwa kwenye mtazamo  kuwa haki hiyo  inatolewa bila ubaguzi na katika misingi ya fursa sawa, pia ni lazima  kuhakikisha mfumo jumuishi wa elimu unakuwepo katika ngazi zote na unakuwa  ni  wa muda mrefu na endelevu.
Katika kutambua haki hii inatakiwa kuhakikisha kuwa  watu walio na ulemavu  hawatengwi kutoka kwenye mfumo wa  jumla wa elimu  na wanaweza kufikia elimu ya msingi jumuishi,bila malipo na iliyo bora pamoja na elimu ya sekondari katika misingi ya usawa  na wengine ndani ya jumuia  ambamo  wanaishi.
Hali kadhalika malazi kwa kila anayehitaji  ni  muhimu yakatolewa  pamoja na  watu walio na ulemavu kupata msaada unaotakiwa kwenye mfumo wa elimu kwa jumla  ili uwepo ufanisi kwenye elimu yao.
Aidha hatua zenye ufanisi  kutoka kwa watu binafsi zinatolewa katika mazingira  ambayo yatawezesha kufikia  kiwango cha juu cha elimu na maendeleo ya jamii pamoja na lengo la  kufanikisha ujumuishi.
Katika mazingira ya aina hiyo  vifaa vya kusomea ni  muhimu ikiwa ni pamoja na kufanikisha kupatikana kwa  maandishi ya wasioona nukta nundu (Braille), vifaa vingine mbadala, miundo ya mawasiliano  na mbinu za kuyafikia.
Pamoja na hayo kwa walemavu wa kuzungumza na kusikia mkakati ni wa kuwawezesha  kusoma lugha za alama na kuboresha utambulisho wa lugha kwa jamii zilizo na ulemavu wa kusikia.
Hali kadhalika kuhakikisha kwamba elimu kwa watu na hususani watoto  ambao hawaoni, viziwi au wenye ulemavu wa kutosikia na kuona  inatolewa katika lugha sahihi na njia za mawasiliano kwa  kila mmoja na kwenye mazingira ya kupata maendeleo ya kielimu na kijamii.
Ili kusaidia kuhakikisha unakuwepo utambuzi wa haki hii idara zinazohusika  zitachukua hatua  ya kuajiri  walimu, wakiwemo walimu  walio na ulemavu ambao wamefuzu kwenye lugha za alama na maandishi kwa wasioona na  kutoa mafunzo kwa  wataalamu na wafanyakazi  katika ngazi zote  za elimu.
Mafunzo ya aina hiyo yatajumuisha uelewa kuhusu ulemavu na matumizi ya njia sahihi na mbadala za mawasiliano, mbinu za kielimu na zana kwa ajili ya kusaidia watu walio na ulemavu.
Hali kadhalika idara husika   kuhakikisha kuwa watu walio na ulemavu  wanaweza kuifikia na kuipata elimu ya kawaida, mafunzo ya ufundi, elimu ya watu wazima  na mafunzo endelevu  yasiyo na ubaguzi katika misingi ya usawa na wengine wasio na ulemavu.
Mnyambuliko huo unajidhihirisha kuwa  fursa ya kupata elimu kwa watu walio na ulemavu ni muhimu  ili kuwaondoa kwenye dhana dhanifu kuwa hawawezi bali  ijengeke dhana kuwa wakiwezeshwa kielimu wanaweza kubadili maisha yao.


Comments