Featured Post

CAF YARIDHISHWA NA MAANDILIZI YA AFCON



Mlinzi wa timu ya Vijana ya Rwanda U-17, Eric Niyonsenga, akijaribu kumzuia mshambuliaji hatari wa Serengeti Boys, Kelvin John wakati wa mechi ya Kundi A la michuano ya Cecafa kuwania nafasi ya kushiriki michuano ya Afcon U-17.

NA MWANDISHI WETU
RAIS wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), Ahmad Ahmad, amesema ameridhishwa na maandalizi ya michuano ya Afrika ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (AFCON).
Mashindano ya mpira wa miguu kwa vijana wenye umri wa chini ya  miaka 17 AFCON yanatarajiwa kufanyika Mei 2019 nchini Tanzania.

Ameyasema hayo jana Jumatatu, Agosti 27, 2018 wakati akizungumza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Ahmad ameihakikishia Serikali kwamba hakuna mabadiliyo yoyote ya ratiba yatakayofanyika kuhusu uenyeji wa mashindano na kwamba CAF itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kufanikisha michuano hiyo.
Rais wa CAF yupo nchini kwa ajili ya kuongoza Mkutano Maalum wa Mabadiliko ya Katiba ya Baraza la Vyama vya Soka katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).
Mkutano huo unaofanyika jijini Dar es Salaam, umehudhuriwa na viongozi wa juu wa nchi wanachama wote 12 wa Cecafa wakiwemo marais.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Makaliwa amesema mechi zote za michuano ya Afrika ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (AFCON) zitafanyika jijini Dar es Salaam.
“Tupo katika hatua za mwisho za maandalijzi ya michuano hiyo itakayofanyika jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Taifa, Uhuru, Chamazi na uwanja wa JK Park utatumika kwa mazoezi,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alisema ni muhimu kwa nchi kushiriki katika mashindano makubwa kama hayo kwa kuwa yanasaidia kukuza vipaji kwa vijana ambao wengi wao ni wanafunzi.
Kanda ya Cecafa itawakilishwa na wenyeji Serengeti Boys na Uganda, ambao juzi Jumapili waliifunga Ethiopia mabao 3-1 kwenye mchezo wa fainali.
Katika mashindano hayo ya ukanda wa Cecafa yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania (Serengeti Boys) ilipata tuzo ya timu yenye nidhamu kwenye michuano hiyo huku Kelvin John alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa michuano hiyo.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (Caf) Ahmad Ahmad alikuwa ni miongoni mwa wageni mashuhuri waliokuwepo uwanjani kutazama mtanange huo.
Katika mchezo wao wa nusu fainali, Uganda waliwaacha midomo wazi timu ya Tanzania, maarufu kama Serengeti Boys kwa kuwachabanga magoli 3-1. Ethiopia wao waliwafunga Rwanda katika hatua hiyo kwa penati 4-2 baada ya kutoka sare ya 2-2 katika dakika 90.
Serengeti Boys, ambao walishafuzu kutokana na Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, walimaliza michuano ya kufuzu katika nafasi ya tatu baada ya kuifunga Rwanda kwa mikwaju ya penati 4-3.
Dakika 90 zilimalizika kwa vijana hao kutoshana nguvu kwa mabao 2-2.
Mafanikio ya Simba Watoto kama inavyoitwa timu ya vijana ya Uganda, yanakuja katika kipindi amabacho kaka zao, timu ya wakubwa The Cranes, imekuwa na mafanikio makubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na walishiriki michuano ya Mataifa ya Afrika mwaka 2017 baada ya kusubiri kwa miaka 39.
"Tuna furaha kwa kuwa hii ndio mara ya kwanza kwa vijana wetu kufuzu kwa mashindano haya. Kufuzu huku ni ushuhuda kuwa tunafanya kazi nzuri katika eneo kuendeleza vijana," amesema Moses Magogo, Rais wa Chama cha Soga Uganda (Fufa).
Kabla ya kuanza kwa michuano ya kufuzu, CAF iliwazuia wachezaji 11 kushiriki kutokana na kuwa na umri mkubwa baada ya kufanyiwa vipimo ya mifupa (MRI) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Hii ni mara ya kwanza kwa CAF kufanya mashindano ya kufuzu kwa michuano ya vijana chini ya miaka 17 kutokana na kanda za kijiografia.
Michuano ya vijana chini ya miaka 17 ya Bara la Afrika itafanyika kuanzia Mei 12 mpaka 26, 2019 nchini Tanzania, na timu zitakazomaliza katika nafasi nne za juu zitaiwakilisha Afrika katika fainali za Kombe la Dunia zitakazopigwa nchini Peru mnamo Oktoba 2019.

Comments