- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Picha ya pamoja ya Maafisa (waliosimama) walioteuliwa kusimamia
rasilimali za uvuvi katika kanda maalumu kwenye Ziwa Victoria na Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina mwenye koti jeupe kushoto kwake ni
Mahamoud Mgimwa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya
Kilimo,Mifugo na Maji kulia ni Katibu Mkuu Uvuvi Rashid Tamatama na
Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Magesa Bulayi.
NA JOHN MAPEPELE, DODOMA
WAZIRI
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameunda Kanda mpya ya Ulinzi na
Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Ziwa Victoria na kuteua maafisa wapya
wataokuwa na jukumu la kudhibiti na kutokomeza uvuvi haramu na biashara
haramu ya mazao ya uvuvi katika Ziwa Victoria ifikapo Desemba 2018.
Akizungumza
jijini Dodoma mwishoni mwa wiki, Waziri Mpina amemteua Didas Mtambalike
kuwa Mkuu mpya wa Kanda mpya ya Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za
Uvuvi Ziwa Victoria huku akiunda kanda mbili za kiulinzi za Sengerema
na Ukerewe .
Pia
Serikali imeanzisha Kituo cha Ukaguzi wa Mazao ya Uvuvi mkoani Singida
na kuweka vizuizi katika maeneo yote yaliyoripotiwa kuwepo matukio ya
utoroshaji wa rasilimali za uvuvi hapa nchini.
Maafisa
wengine walioteuliwa na Waziri Mpina kuongoza kanda zingine ni pamoja
na West Mbembati ambaye ataongoza Kanda ya Kagera, Vicenti Masui Munda
Kanda ya Mwanza, Jairos Mahenge Kanda ya Mkoa wa Mara.
Wengine
ni Judith Mgaya atakayeongoza Kanda ya Kiulinzi Ukerewe na Roman Mkenda
Kanda ya Mkoa wa Geita, Wencleslaus Luhasile aliyekuwa Afisa Uvuvi wa
Wilaya ya Magu sasa ataongoza Kanda ya Kiulinzi ya Sengerema na Samson
Mboje kutoka Kituo cha Usimamizi na Ulinzi wa Rasilimali Kanda ya
Mwanza, sasa ameteuliwa kuongoza Kanda ya Simiyu/Magu.
Aidha
Waziri Mpina alisisitiza kuwa katika operesheni inayoendelea Serikali
inaandaa utaratibu wa kwenda na mahakama inayotembea ili watuhumiwa na
wahalifu wahukumiwe pale pale wakiwa na mashahidi wao.
Kuhusu
maendeleo ya wavuvi wadogo, Waziri Mpina amesema Wizara yake kwa
kushirikiana na Benki ya NMB inawafuatilia wavuvi na kuwafungulia
akaunti ambapo hadi sasa zaidi ya wavuvi 20,000 wamefikiwa.
Amesema
utafiti umebaini kuwa asilimia 98 ya wavuvi ni vibarua wa matajiri
ambapo mapato yanayotokana na uvuvi kila wanapotoka kuvua hugawanywa
nusu na tajiri wao ambaye ndiye mmliki wa chombo na nusu iliyobaki
kugawana kila mvuvi aliyekuwa katika chombo hicho hali iliyowafanya
wavuvi kote nchini kuendelea kuwa masikini na kuwanufaisha matajiri
wachache.
Vile
vile, Waziri Mpina amesema kuwa Operesheni Sangara awamu ya tatu
itaendelea na kwa maji baridi yote ikiwemo Ziwa Tanganyika, Nyasa,
Rukwa, Nyumba ya Mungu na Mtera na mito ili kuhakikisha rasilimali hiyo
inalindwa na kunufaisha taifa.
Mbali
na hatua hiyo Waziri Mpina ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini
(TAFIRI) kufanya utafiti ili kujua kiasi cha samaki waliopo katika Ziwa
Victoria baada ya kuendesha Operesheni Sangara kwa miezi sita sasa.
Kuhusu
viongozi waadilifu na wanaosimamia kikamilifu ulinzi wa rasilimali
uvuvi Waziri Mpina amesema Wizara yake itaendelea kuwatambua na
kuwapongeza wananchi na viongozi wanaofanya vizuri kwenye usimamizi wa
raslimali za uvuvi nchini.
Alisema
katika kipindi hiki Wizara yake inatambua mchango wa Mkuu wa Wilaya ya
Sengerema Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Kipole na Mkuu wa Wilaya ya Musoma,
Mkoa wa Mara, Dkt. Vicenty Anney pamoja na Afisa Mtendaji wa Kata ya
Kagya Wilaya ya Bukoba, Beatrice Lugemalila.
Naye
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji,
Dk. Christine Ishengoma alisema mawaziri waliopita katika wizara hiyo
walifanya kazi nzuri lakini ubunifu wa kipekee uliofanywa na Waziri
Mpina umeiwezesha sekta ya uvuvi kuongeza mapato kutoka sh bilioni 18.5
katika mwaka wa fedha 2016/2017 hadi kufikia sh bilioni 26.3 mwaka wa
fedha 2017/2018 fedha ambazo zitasaidia uboreshaji wa huduma za kijamii
katika maeneo yote nchini.
Mjumbe
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji, Katani Ahmad
Katani alipongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi
ya kulinda rasilamili za Taifa na kutaka juhudi hizo kuwa endelevu
kwani pamoja na kuwa na eneo kubwa la maji bado uvuvi haujaweza
kunufaisha Taifa.
Katani
ambaye pia ni Mbunge wa Tandahimba mkoani Mtwara aliishauri Serikali
kuangalia uwezekano wa kufungua maduka yake ya zana za uvuvi ili
kuwarahishia wavuvi kupata zana hizo kwa wakati na zenye ubora
unaotakiwa kwa mujibu wa sheria.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu Uvuvi-Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Rashid
Tamatama alisema suala la ulinzi wa rasilimali za uvuvi litakuwa ni moja
ya majukumu ya kila siku ya watumishi wa wizara hiyo ili kuhakikisha
Taifa linanufaika vya kutosha na rasilimali hizo.
Comments
Post a Comment