- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA ALOYCE NDELEIO
AJALI za barabarani, zinatisha, zinahuzunisha na zinasikitisha na
dhihirisho la hili katika kipindi cha hivi sasa kwa Tanzania, limo katika kauli
hii ya kiongozi w anchi Rais Dkt. John Pombe Magufuli Julai 2, mwaka huu.
Alisema, “Nimechoka kutuma rambirambi kila siku, inatoka ajali hii,
inakuja hii, na kwa bahati mbaya mimi ndiye pekee ninayetuma
rambirambi, Waziri wa Mambo ya Ndani hahangaiki kutuma rambirambi…wameshakufa
40, mnataka wafe wangapi…?”
Huzuni na masikitiko ya Rais hapo yalionesha wazi kukosekana kwa
uwajibikaji katika kushughulikia na kudhibiti matukio ya ajali. Katika
kuwajibisha wahusika yeyé akaanza na kumng’oa waziri mhusika na kutoa maagizo
kwa mteule mpya kushughulikia hilo.
Kupambana na suala la ajali barabarani ni suala lililoleta hisia katika
jamii na hata kimataifa hali iliyosababisha Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa kuzindua mwongo wa usalama barabarani kwa kipindi cha miaka kumi
ili kukazia hatua zinazochukuliwa dhidi ya ongezeko kubwa la ajali za
barabarani.
Azimio hilo la Umoja wa Mataifa namba A/64/L.44/Rev.1 lilipitishwa kwa
kauli moja na wajumbe wote 192 wa Baraza Kuu, likiwa linataja hatua
kadhaa zinazopaswa kuchukuliwa ili kupunguza ajali za barabarani ambazo licha
ya kuwa chanzo vya vifo na ulemavu, pia zimekuwa na athari kubwa kwa uchumi na
maendeleo kwa nchi zenye uchumi mdogo.
Alama mpya au nembo ya usalama barabarani ilizinduliwa pia katika
kutilia mkazo umuhimu wa Muongo wa Umoja wa Mataifa wa kuchukua hatua dhidi ya
ajali za barabarani.
Hatua hiyo mpya ya kupambana na ajali za barabarani ilichukuliwa ili
kuokoa maisha ya watu kutokana na kukithiri kwa ajali za barabarani ambazo
zimekuwa zinasababisha vifo vya watu milioni 1.3 kwa mwaka.
Nembo hiyo inalenga kuwa ni njia ya kuijengea jamii uelewa wa
masuala ya usalama barabarani ikiwa ni sawa na riboni za Ukimwi/ VVU au
mshipi mweupe unaovaliwa mkononi kwa ajili ya kupambana na umaskini.
Kila siku wastani wa watu 3500 duniani kote huuawa kwenye barabara, na
asilimia 90 ya ajali zote hutokea miongoni mwa nchi zinazoendelea.
Kishikizo hicho kimetengenezwa na wakala wa WPP plc ambaye yuko kwenye ubia wa
kuunga mkono Mwongo wa Hatua za Usalama Barabarani 2011 -2020.
Ajali za barabarani
Tanzania
Wakati hali ikiwa
hivyo, Tanzania katika siku za karibuni imekuwa inakabiliwa na matukio
mbalimbali ya ajali za barabarani na rejea zipo nyingi ikiwemo ajali ya basi jijini Arusha mwaka jana 2017, ambayo
ilisababisha vifo vya wanafunzi 33, mwalimu wao pamoja na dereva wa basi
hilo.
Nyingine ni ajali
zilizotisha zilitokea Julai 2011, mkoani Morogoro ambapo watu 13,
wanamuziki wa kikundi cha Five Star Modern Taarab na nyingine ni
iliyotokea Moshi, Kilimanjaro na kusababisha vifo vya watu 11 na majeruhi
26.
Pamoja na hali hiyo
kilichoonekana kimataifa ni kuwepo haja ya kuwa na Mwongo wa kuchukua hatua ili
kupunguza ajali za barabarani.
Katika dhana hiyo njia ilionekana ni kuiunganisha
dunia kuchukua hatua ambapo Mkurugenzi wa Kuzuia Madhara kwenye Shirika la Afya
Duniani Etienne Krug alisema, “Hospitali na vyumba vya kuhifadhia
maiti sehemu mbalimbali dunia zimejaa wahanga wa ajali za
barabarani. Muongo wa Kuchukua Hatua wa Umoja wa Mataifa ni fursa
ya kipekee.
“Ukiwa unatambulishwa
kwa Kishikizo cha usalama barabarani, mwongo huu utawezesha
wahusika wengi kuunganisha nguvu na kuiweka kwa vitendo programu ya kuzuia na
huduma zinazohitajika katika kuepuka hasara isiyo ya lazima.”
Mwongo wa Kuchukua
Hatua za Usalama Barabarani ulizinduliwa rasmi Mei 11, 2011 kwa matukio
mablimbali duniani. Lengo la Mwongo lililoridhiwa na serikali
100 kwenye Baraza Kuu la Umoja wa mataifa ni, “Kuimarisha na
kupunguza” vifo vya barabarani duniani ifikapo mwaka 2020.
Shirika la Afya
Duniani na kamisheni za kikanda za Umoja wa Mataifa zikiratibu mwongo huo
kwa niaba ya Umoja wa Mataifa
Krug anasema, “Usafiri
salama ni lazima uonekane kuwa ni haki ya msingi ya binadamu
kama inavyokuwa kwenye mahitaji ya maji salama, hivyo
ni hitaji la msingi kwa ajili ya kusaidia mamilioni ya watu kuboresha
fursa za maisha yao na kuondoka kwenye umaskini.”
Miongoni mwa nchi
zinazoendelea watu wamekuwa wanakabiliana na mabadiliko ya kasi ya mifumo ya
usafiri katika kipindi cha miaka 20 hadi 30 na bado imebakia kuwa ni hatua
inayobadilika kwa kasi.
Idadi ya magari
duniani inakadiriwa kuongezeka kwa mara tatu ifikapo mwaka 2050 na
asilimia 80 ya ongezeko hilo linatarajiwa kuwa miongoni mwa nchi zinazoendelea.
Hali hiyo inamaanisha
kuwa kuna haja ya kuwa na lengo la kuzuia utoaji wa hewa ya Dayoksaidi
ya Kaboni kwa kiwango cha nusu ya kinachotolewa hivi
sasa na Umoja wa Ulaya.
Anafahamisha, “Wakati
kuna mabadiliko ya hali ya hewa na suala muhimu kama hili inaweza kuwa ni
muhimu kuwasaidia wapanga sera na sekta ya magari kupunguza athari
zinazotokana na ongezeko kubwa la idadi ya magari kwa kuboresha uchumi wa
mafuta na kupunguza utoaji wa gesi joto.
“Kila baada ya sekunde
30 mtoto mmoja hufariki au kujeruhiwa, zaidi ya watoto wanne kati ya kila
watoto watano wanaofariki kutokana na ajali za barabarani wanaishi
miongoni mwa nchi zenye kipato cha kati na cha chini na
inakadiriwa kuwa vifo vinavyotokana na ajali za barabarani miongoni
mwa nchi hizo zitaongezeka hadi kiwango cha zaidi ya asilimia 80 ifikapo
mwaka 2020.”
Benki ya Dunia hivi
karibuni ilikadiria kuwa nchi zinazoendelea hupoteza takribani dola bilioni 100
kila mwaka kutokana na ajali za barabarani kiasi ambacho kinalingana na
kiwango kinachotolewa kama misaada ya maendeleo.
Jambo linalofanya hata
kuiona hali hiyo kuwa ni mbaya, ni kwamba zipo nyenzo na njia za
kusitisha hali hiyo, kuokoa maisha lakini hakuna jambo ambalo
limeshafanyika.
Jambo ambalo pia
linaweza kujikita kwenye mawazo ya wanajamii ni kuona athari za kutisha
kwenye maisha ya watu wakati wapanga sera wanaichukulia hali hiyo
kinyume au kudharau tatizo. Janga la ajali za barabarani linaweza
kudhibitiwa lakini linahitaji kuangaliwa na dunia kuitupia macho.
Barabara zisizo salama
pia ni barabara ambazo haziwavutii watumiaji wengine wa barabara
wasiotumia magari, waendesha baiskeli au waenda kwa miguu katika hali hiyo ipo
haja ya kuhakikisha kuwa maskini na watu walio pembezoni ambao hawana uwezo wa
kumiliki gari kwamba na wao wanakuwa na huru na salama kwenye mifumo ya usafirishaji.
Zipo sababu kumi
zinazoweza kueleza ni kwa nini ni muhimu kuchukua hatua dhidi ya vifo
vinavyosababishwa na ajali za barabarani
Sababu ya kwanza ni
kwamba watu milioni 1.3 hufariki kila mwaka kutokana na ajali za
barabarani. Pili ajali za barabarani zinaua watu wengi kuliko
ugonjwa wa Malaria. Tatu watu milioni 50 hujeruhiwa na matokeo yake wengi
hupata ulemavu.
Nne asilimia 90
matukio ya ajali hutokea miongoni mwa nchi zinazoendelea. Tano vifo
vinavyotokana na ajali vinatarajiwa kuongezeka na kufikia milioni 1.9
ifikapo mwaka 2020.
Sita ajali za barabarani ni chanzo namba moja kinachosababisha
vifo vya vijana duniani kote na Saba ajali za barabarani zitakuwa ni
mzigo unaoielemea sekta ya afya kwa watoto walio na
umri chini ya miaka mitano.
Hata hivyo sababu ya Nane hasara inayopatikana kiuchumi kwa nchi
zinazoendelea hufikia takribani dola bilioni moja kwa mwaka. Tisa ni kwamba
majeruhi husababisha kuwepo kwa mzigo mkubwa katika mifumo ya hospitali
na afya kwa ujumla na Kumi ni kwamba ajali za barabarani zinaepukika.

Comments
Post a Comment