Featured Post

NYANZA KUWA MWENYEJI WA SIKU YA USHIRIKA DUNIANI



NA CONGES MRAMBA, MWANZA
CHAMA Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mwanza (Nyanza Co-operative Union), kitakuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya  Siku ya Ushirika Duniani.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Chama hiki ambazo Tanzanite imeambiwa jana zinasema, Menejimenti ya Nyanza sasa inafanya maandalizi kuhakikisha  maadhimisho haya yanafana; na yatashirikisha vyama vyote vya ushirika hapa nchini.
Kwa mujibu wa viongozi wa chama hicho, ambao hawakutaka kutajwa majina, maadhimisho hayo yatafanyika katika viwanja vya CCM Kirumba jijini hapa mwanzoni mwa Julai mwaka huu, ambapo mgeni rasmi anatazamiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Maadhimisho hayo yatafika kilele Julai 7 hapo kwenye viwanja vya CCM Kirumba.
“Hii hapa ni Menejimenti ya Nyanza, na hapa tunafanya maandalizi ya maadhimisho haya, na tunaishukuru serikali kutuamini ili kuwa wenyeji wa Siku ya Ushirika Duniani,” mmoja wa wajumbe wa Menejimenti hiyo ameliamia gazeti hili jana katika ofisi za chama hicho.
Kulingana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, Chama cha Nyanza ndicho kilichozaa vyama vyote vya ushirika katika Kanda ya Ziwa.
“Nyanza jamani, historia ya dunia ipo kwenye rekodi… ndiyo kilikuwa chama kikubwa cha Ushirika cha pili hapa duniani, nyuma ya kile cha Sweden. Ndiyo Victoria Federation, lakini ilikuja kuhujumiwa na watu ambao ajenda yao ilikuwa ubadhirifu na kuhujumu tu!” Mkuu huyo wa mkoa alisema.
Mkuu wa Mkoa alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kuwaambia hujuma na ufisadi uliokuwa ukifanywa dhidi ya ushirika huo, huku akisikitika chama hicho kushindwa kufanya kazi.
Wakati kikiwa katika ubora wake, kilikuwa kikimiliki vinu vya kuchambulia pamba (ginneries) na mtaji wa zaidi ya shilingi bilioni 10, huku kikinunua pamba katika mikoa ya Geita, Mwanza, Simiyu, Shinyanga na Mara.
Alisema, wakati huo kilikuwa mhimili wa ajira katika Kanda ya Ziwa, kikinunua pamba ya zaidi ya shilingi bilioni sita kwa mwaka.
Hata hivyo, Serikali ya Rais John Magufuli imeamua kukisimamisha tena chama hicho, ambapo katika msimu huu kinasimama kununua pamba mkoani humo.
Serikali ilibadilisha Menejimenti ya Chama na kuweka mpya, kisha watuhumiwa waliojiuzia mali za chama hicho kwa bei chee baadhi yao walikamatwa na kufunguliwa mashtaka.
Kaimu Meneja Mkuu wa Nyanza, Juma Mokili amesema, msimu huu wa ununuzi wa zao la pamba, wanatazamiwa kukusanya zaidi ya asilimia 50 ya malengo waliyojiwekea.

Comments