- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
NA MWANDISHI WETU
KESI ya utakatishaji
fedha na umiliki wa utajiri kuliko kipato chake inayomkabili aliyekuwa Mhasibu
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai na
wenzake imechukua sura mpya baada ya upande wa mashtaka kuieleza Mahakama jana
kuwa mhasibu huyo alitumia miamala ya uongo kuficha umiliki wa mali zake.
Hayo yalielezwa jana
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakati watuhumiwa
hao wakisomewa maelezo ya awali, ambapo licha ya kuyakubali maelezo yao binafsi,
walikana mashtaka yote yanayowakabili.
Mbali na Gugai,
washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na
Yasini Katera.
Wakili wa Serikali,
Awamu Mbangwa, aliwasomea washtakiwa maelezo hayo ya awali (preliminary hearing
- PH) mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Wakili Mbangwa alidai
kuwa, Gugai anakabiliwa na makosa mbalimbali ikiwemo kumiliki mali
isiyoelezeka, kughushi na kutakatisha fedha ambayo anadaiwa kuyatenda kati ya
mwaka 2005 na mwaka 2006.
Alidai kuwa, Gugai
aliajiriwa na Takukuru kama mchunguzi daraja la tatu mwaka 2001 na baadaye 2009
aliteuliwa kuwa Mhasibu Mkuu wa Takukuru, kazi aliyoendelea nayo hadi Agosti
2016 alipofukuzwa kazi.
Alidai, washtakiwa
wenzake wote ni marafiki zake wa karibu na kwamba katika kipindi chote cha
ajira, Gugai hakuwa na chanzo cha mapato ambacho kingeweza kumpatia kipato
zaidi ya ajira yake.
Alidai kwamba, kwenye
mishahara ya mshtakiwa na marupurupu mengine, alijipatia kipato halali cha Shs.
852,183,160.46 kutoka kwa mwajiri wake.
Pia mikopo yote
aliyoipata katika benki ya CRDB, NBC, Benki ya Posta na Saccos ya Takukuru ilikiwa
ina thamani ya Shs. 137 milioni.
Alidai kwamba, mwaka 2009
alitakiwa kufanya matamko juu ya umiliki wa mali zake ambapo alitamka kuwa
hakuwa na vyanzo vingine vya mapato zaidi ya ajira yake na kwamba hakutamka
mali zote alizokuwa nazo.
Aidha, Mbangwa alidai
kuwa, mwaka 2014/015, Gugai alisajiri kampuni mbili za familia zenye majina ya
Guru Medical Investment Ltd na Agobest (T) Ltd, ambazo hazikuwahi kufanya kazi
yoyote wala kupata leseni ya biashara tangu ziposajiliwa.
Aliendelea kudai
kuwa, Januari 2016 baada ya kuanzishwa kwa uchunguzi mshtakiwa Gugai alisajili
kampuni ya biashara kwa jina la Cheers Wine and Spirit ambayo hadi mwishoni mwa
mwaka huo haikuwahi kuwaingizia kipato chochote.
Alisema, mwaka 2015/2016
katika uchunguzi ilionyesha kuwa, Gugai alijipatia utajiri wa juu zaidi ya
kipato chake halali wa Shs. 3,634,961,105.02 ambapo alimiliki nyumba 19 na
viwanja 37 vilivyopimwa.
Utajiri huo alishindwa
kuutolea maelezo ya jinsi alivyoupata ambapo ilisomwa kuwa, Juni 2016, Gugai
alifanya juhudi za makusudi kuficha mali hizo kwa kushirikiana na washtakiwa
hao wenziwe kwa kutengeneza mikataba ya uongo wakionyesha kuwa ameuza au
kuhamisha umiliki wa mali hizo kabla ya 2016 wakati wakijua si kweli.
Wakili Mbangwa
alidai, uchunguzi ulibaini siyo kweli kuwa mshtakiwa Gugai aliuza ama kuhamisha
umiliki wa mali hizo bali alifanya miamala ya uongo kwa lengo la kuficha
umiliki halali wa mali hizo.
Kesi hiyo itaanza
kusikilizwa Juni 28, 2018.
Katika kesi hiyo,
washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 43 yakiwemo 20 ya utakatishaji fedha
haramu, kumiliki mali zisizoendana na kipato na kughushi mikataba ya mauziano
ya viwanja katika maeneo mbalimbali.

Comments
Post a Comment