- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata Maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Edosama Hardware Limited, Edward Maduhu kuhusu bidhaa mbalimbali zinazotokana na miti ambazo zinatengenezwa na kampuni hiyo wakati alipotembelea mabada ya maonyesho kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam Mei 31, 2018. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza
Wizara, mashirika na taasisi zote za Serikali na binafsi zianze kutumia nishati
mbadala ili kuondoa kabisa matumizi ya kuni na mkaa.
“Wizara, taasisi na mashirika yote ya Serikali na binafsi
pamoja na vikundi vya uzalishaji wanaotumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili
ya kupikia au shughuli za uzalishaji waanze kutumia nishati mbadala ili
matumizi ya mkaa yaishe na ikiwezekana yatoweke kabisa,” amesema.
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Mei
31, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wananchi na viongozi wa mkoa wa Dar es
Salaam walioshiriki uzinduzi wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwenye
viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Mkaa
ni Gharama: Tumia Nishati Mbadala.”
Waziri Mkuu amesema
teknolojia bora ya uzalishaji wa mkaa mbadala ambayo ameiona kwenye maonesho
hayo, ikuzwe na kusambazwa kote nchini ili kuwawezesha wananchi walio wengi
waachane na matumizi ya mkaa wa kawaida na badala yake watumie mkaa-mbadala kwa lengo la kuhifadhi misitu
na kupunguza uharibifu wa mazingira.
Ili kufanikisha matumizi ya
teknolojia hiyo, Waziri Mkuu amesema vibali vya ujenzi wa majengo makubwa na
taasisi kama shule, vyuo, hospitali navyo pia vianze kuzingatia ufungaji wa
mifumo ya nishati ya gesi kwa ajili ya matumizi ya kupikia ili kurahisisha
upatikanaji na matumizi ya nishati mbadala katika taasisi na majengo makubwa.
“Wahandisi na wachoraji
ramani za majengo waweke njia za kupitisha kwenye michoro yao ili ujenzi wa
nyumba na majengo haya ukikamilika, watumiaji waweze kutumia teknolojia hiyo,”
amesema.
Wakati
huohuo,
Waziri Mkuu amesema Mkoa wa Dar es Salaam ni lazima ubadilike na uachane na
matumizi ya mkaa. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mkoa huo unatumia tani
500,000 za mkaa kwa mwaka.
“Viongozi wa mkoa na
wilaya ondokeni hapa na hili kama ajenda ya mkoa wa Dar es Salaam, mkaifanyie
kazi na Wizara pia ifuatilie mmetekeleza kwa kiasi gani. Jitihada zilizofanywa
na Jiji la Dar es Salaam kupitia kwa Mstahiki Meya, za kuanza kuwapa mtaji
wajasiriamali hawa wanaotengeneza teknolojia mpya ni lazima ziigwe na nyie
kwenye Manispaa zenu.”
“Meya ametoa fursa na
amewaanzishia, na ninyi sasa endeleeni. Tengenezeni bajeti kupitia Mabaraza ya
Madiwani na muwaunge mkono wajasiriamali wanaotengeneza haya majiko kwa kuwapa
teknolojia hii kwenye maeneo yenu. Wanaotengeneza mashine za mkaa mbadala,
wawezeshwe watengeneze mashine nyingi zaidi na zije kila Manispaa, ili kila
Manispaa ianze kutumia teknonolojia hiyo kupikia,” alisisitiza.
Amewaagiza Wakuu wa Wilaya
na Wakurugenzi wa Manispaa za Jiji la Dar es Salaam wafuatilie kwa karibu
usambazaji wa teknolojia hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano
na Mazingira), January Yusuf Makamba amesema hali ya mazingira hapa nchini ni
mbaya licha ya kuwa haionekani kwa haraka na watu waishio mijini.
“Hali ya mazingira nchini mwetu
ni mbaya sana na inawezekana watu wanaoishi Dar es Salaam hawaioni kwa haraka kwa
sababu mahitaji yao yote wanayapata sokoni na madukani,” alisema.
“Wenzetu wa mikoani na
vijijii wanaotegemea mvua na udongo wenye rutuba wanataabika kwa sababu kipato
chao kinaathirika kutokana na uharibifu wa mazingira,” alisema.
Alisema mazingira
yanafungamana na utalii, kilimo, ufugaji, nishati, maji na kwamba maendeleo ya
nchi pia yamefungamana moja kwa moja na mazingira. “Asilimia 90 ya Watanzania
wanatumia kuni na mkaa kupikia lakini asilimia 70 ya mkaa wote unaozalishwa
nchini Tanzania, unatumika jijini Dar es Salaam,” alisema.
Waziri Makamba alisema
taasisi za Serikali kama vyuo, magereza, hospitali na shule zinaongoza kwa
matumizi ya kuni na mkaa na hivyo kuchangia uharibifu mkubwa wa mazingira.
Akitoa mfano, alisema Chuo
Kikuu cha Dodoma (UDOM) kina wanafunzi wapatao 30,000 na kinalazimika kuandaa
milo mitatu kila siku.
“Chuo hiki kina migahawa
tisa, kule nyuma kumejaa magogo ya kuni. Kuna mgahawa mmoja mdogo unatumia
magunia 17 ya mkaa kwa siku, sasa huo mkubwa unatumia magunia mangapi?”
alihoji.
Maadhimisho hayo yaliyozinduliwa
leo, yataendelea hadi Juni 5, mwaka huu ambayo ni siku ya kilele. Pia wiki
nzima kutakuwa na makongamano, midahalo na mjadala wa kitaifa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla wakati alipowasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja kuzindua Maadhisho ya Wiki ya Mazingira, Mei 31, 2018. Wapili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es salaam, Kate Kamba wakati alipowasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam kuzindua Wiki ya Mazingira, Mei 31, 2018. Wapili kushoto ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla na watatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani , Mhandisi Evarest Ndikilo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Space Engineering Limited, Bw. Philip Mtui kuhusu mkaa uliotengenezwa kutokana na takataka na kufungashwa kwenye kiroba tayari kwa kuuzwa wakati alipotembelea banda la Kampuni hiyo kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018. katikati ni Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi, Evarest Ndikilo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Space Engineering Limited, Bw. Philip Mtui kuhusu mkaa uliotengenezwa kutoka na takataka na kufungashwa kwenye kiroba tayari kwa kuuzwa wakati alipotembelea banda la Kampuni hiyo kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018. Kulia kwake ni Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi, Evarest Ndikilo na kushoto ni Meneja Mauzo wa kampuni hiyo, Neema Matemba.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuuu).
Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akipata Maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Edosama Hardware Limited, Edward Maduhu kuhusu bidhaa mbalimbali zinazotokana na miti ambazo zinatengenezwa na kampuni hiyo wakati alipotembelea mabada ya maonyesho kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam Mei 31, 2018. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba na kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es salaam, Kate Kamba.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Bibi Nimwagile Mwaijumba wakati alipotembelea banda la Kituo cha Utengenezaji magari cha Nyumbu na kujionea mashine ya kutengeneza mkaa bora kwa kutumia takataka iliyobuniwa na kutengenezwa na kituo hicho. Waziri Mkuu alitembelea mabanda ya maonyesho kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018. Watatu kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba na wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Opwani Mhandisi, Evarest Ndikilo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni ya JHS , David Mwendapole wakati alipotoa maelezo kuhusu majiko makubwa yanayotumia gesi kidogo katika maonyesho ya Wiki ya Mazingira kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018. Wanne kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Wiki ya Mazingira kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam Mei 31, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya wananchi waliohudhuria katika maadhimisho ya wiki ya Mazingira wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipowahutubia kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na viongozi baada ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 30, 2018. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangala, Mwenyekiti wa CC wa Mkoa wa Dar es alaam, Kate Kamba,Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Matiku Makori na kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, MEI 31, 2018.
Comments
Post a Comment