- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga, akielezea kuwapo kwa changamoto ya kiwango cha chini cha upatikanaji wa huduma za bima za kilimo na gharama kubwa za huduma za fedha wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya Fedha na Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
SERIKALI imeitaka
Sekta ndogo ya Benki kuongeza ubunifu kwa kutoa mikopo ya muda mfupi na mrefu
ambayo itawezesha ukuaji wa sekta za viwanda na kilimo pamoja na wajasiriamali
wadogo.
Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) Prof. Florens Luoga, kwa niaba ya Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, katika Mkutano wa wadau wa Sekta ya
Fedha uliowashirikisha wabunge, washirika wa Maendeleo, wakuu wa Taasisi za
fedha na Wizara ya Fedha na Mipango.
Prof. Luoga alitoa wito huo kufuatia kuwepo kwa
changamoto katika Sekta hiyo ikiwemo ukosefu wa uwekezaji wa miradi mikubwa ya
maendeleo katika viwanda, kilimo na miundombinu pia ukosefu wa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na
wa kati.
“Kuna kiwango cha chini cha upatikanaji wa huduma
za bima za kilimo, gharama kubwa za huduma za fedha, mifumo hafifu ya
kuwalinda watumiaji wa huduma za fedha,
ukosefu wa elimu ya fedha kwa wananchi na wananchi wengi kutofikiwa na huduma
za fedha ambapo ni asilimia 8.6 tu ya nguvu kazi ya wananchi waishio vijijini
wanapata huduma za benki ikilinganishwa na asilimia 32.1 ya nguvu kazi kwa
wanaoishi mijini,” alisisitiza Prof Luoga
Gavana huyo wa Benki Kuu alisema kuwa ili kukabiliana na changamoto
hizo, Serikali ilifanya maboresho ya Sekta ya Fedha katika eneo la ubinafsishaji wa benki za
Serikali kurekebisha na kutunga sera na sheria mbalimbali hadi kufikia Desemba,
2017 ili kuweka misingi imara ya kuwezesha ukuaji, ushindani na ufanisi katika
sekta ya fedha.
“Maboresho ya Sekta ya Fedha yamesaidia ongezeko la idadi ya benki na
taasisi za fedha kufikia 54, kampuni za bima 31, kampuni zilizoorodheshwa
kwenye soko la hisa 27, taasisi za huduma ndogo za fedha takriban 450, mifuko
na program za Serikali 34, vikundi vya kifedha vya kijamii takribani 30,019
katika mikoa 18 ya Tanzania bara na uanzishwaji wa soko la bidhaa,” alieleza
Prof. Luoga.
Alisisitiza kuwa taasisi za fedha zikitimiza wajibu wake, sekta binafsi
itakuwa na uwezo wa kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa viwanda,
kuongeza uzalishaji wa bidhaa zitakazouzwa nje ya nchi na hatimaye kukuza
uchumi wa Taifa na kupunguza umasikini wa kipato wa wananchi.
Aidha, Serikali katika kupunguza umaskini na kukuza uchumi, inaandaa Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha, unalenga
kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha, kulinda watumiaji wa huduma
za fedha, upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu, uthabiti wa sekta ya fedha,
kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika sekta ya fedha, kudhibiti
utakasishaji wa fedha haramu na kuweka mazingira wezeshi ya sheria, kanuni na
taratibu katika sekta hiyo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu,
akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Doto James, alisema
kuwa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha uchumi wa nchi unaongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.
“Kuwepo kwa viwanda vingi italeta ongezeko la ajira kwa wananchi walio
wengi pamoja na kuiongezea Serikali mapato,” alieleza Dkt. Kazungu
Aidha, kwa lengo la kuwawezesha wananchi kuwekeza katika viwanda vidogo
vidogo, ni lazima wapate rasilimali fedha kutoka kwenye taasisi kama vile benki na masoko ya mitaji hivyo
watoa huduma kwenye taasisi hizo wanapaswa kuongeza ubunifu kwenye utoaji wa
huduma zinazokidhi mahitaji ya wapokeaji huduma kulingana na shughuli
wanazofanya na kwa gharama nafuu.
Alizitaka taasisi za fedha kuwekeza katika kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu
wa kutumia taasisi hizo kwa kujiwekea akiba na kupata mitaji itakayowezesha
kukuza biashara na shughuli zao za kiuchumi hivyo wadau wa sekta ya fedha
wanapaswa kujiuliza ni kwa nini mikopo ya biashara kwenda kwenye sekta binafsi
hairidhishi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na
Uratibu), Prof. Faustin Kamuzora aliwataka wadau wa sekta ya fedha kuzungumzia
mafanikio ya Sekta ya fedha kwa njia ya miamala ya Simu za mkononi kwa kuwa
Tanzania imepiga hatua kubwa Duniani katika eneo hilo na hivyo kuwa mfano kwa
mataifa mbalimbali.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji Prof. Elisante Ole Gabriel ameitaka Sekta binafsi
inayonufaika na mikopo inayotolewa na taasisi za fedha kuwekeza kwenye miradi
yenye tija na kulipa mikopo yao kwa wakati pamoja na kuongeza thamani ya bidhaa
wanazozalisha na kuongeza kiwango cha mauzo ya bidhaa hizo nje ya nchi.
Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Maria Kangoye (kushoto)
akizungumza jambo wakati wa mkutano kati ya
wadau wa sekta ya Fedha na Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) Prof. Florens Luoga (katikati), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha
na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu (kulia), na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera na Uratibu), Prof. Faustin Kamuzora (kushoto), wakati wa mkutano
wa wadau wa sekta ya Fedha na Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei,
akisikiliza kwa makini wito wa Gavana wa Benki Kuu
ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga (hayupo pichani) kuhusu
Sekta ndogo ya Benki kuongeza ubunifu kwa kutoa mikopo
ya muda mfupi na mrefu ambayo itawezesha ukuaji wa sekta za viwanda, Jijini Dodoma.
Baadhi ya wakurugenzi wa taasisi za fedha na maafisa
waandamizi wa Serikali kutoka Wizara ya Fedha na Mipango wakisikiliza maelezo ya
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu
Kazungu (hayupo pichani) alipokua akieleza wajibu wa sekta ya fedha nchini
katika kuwezesha viwanda vidogo vidogo, wakati wa mkutano wa wadau wa
sekta ya Fedha na Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu, Kazungu akisisitiza kuhusu sekta ya fedha kuwa na mikakakati yenye
tija katika kukuza uchumi wa viwanda wakati wa mkutano wa wadau wa
sekta ya Fedha na Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
Kaimu Kamishna wa Sera za Fedha wa Wizara ya Fedha na
Mipango Bw. Michael Nyagoga akielezea dhana ya Mkutano wa wadau wa sekta ya
Fedha na Wizara ya Fedha na Mipango kuwa
ni pamoja na kutatua changamoto mbalimbali za kifedha za Sekta ya Viwanda
nchini.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizaya ya Fedha
na Mipango)
Comments
Post a Comment