Kisiwani Mafia Tanzania, Mafuta ya
petrol na dizeli huuzwa kwa reja reja katika vibanda, huku kukiwa hakuna
sheli ya mafuta kwa ajili ya mahitaji ya matumizi ya watu wenye vyombo
vya usafiri kisiwani humo.
Mafuta hayo hupimwa kwa chupa kisha kuuzwa kwa bei ya juu kuliko maeneo ya karibu kama Dar es salaam. Wauzaji wanasema sababu kuu ya hali hiyo ni kutokua na usafiri wa kuaminika wa kuingia na kutoka kisiwani humo. Wauzaji hufunga safari kutoka Mafia hadi maeneo ya karibu kama
Dar es salaam na pwani kisha hununua mafuta katika sheli za mafuta kama
watu wengine wenye magari wanavyofanya, wao huweka kwenye mapipa na
kusafirisha kwa mashua hadi kisiwani mafia. Kwa kawaida hununua mafuta kama petrol kwa dola moja
ya marekani kwa lita moja kisha huongeza pesa kidogo kwa wanunuzi
yanapofika mafia. Mashua hizo huweza kuchukua siku kadhaa
kutokana na hali ya upepo wa bahari na wauzaji wa mafuta hayo wanasema
kuna uwezekano wa mapipa kupasuka katika mashua hizo hivyo hupata
hasara. Katika
vibanda katika eneo hilo wauzaji wengi wamekua wakiogopa kuzungumza
kutokana na kutojua hatma ya kazi yao, ingawa wamekua msaada mkubwa kwa
wamiliki wa vyombo vya usafiri. Mmoja wa wauzaji, Abdalah Mohamed
anasema kuwa gharama wanayonunua mafuta na kuuza, wanapata faida kidogo
sana kutokana na gharama ya usafirishaji huo wa mafuta. ''tunayavusha katika bahari na bahari kuna wakati
inakua inachafuka, vitu vinapinduka lakini sasa ndio kazi hiyo'' Anasema
bwana Abdallah Wategemeaji wa mafuta kuendesha kazi zao, kama
wamiliki wa taxi na bajaji, wanasema mafuta huchukua muda mrefu kufika
hivyo biashara zao huweza kuathirika. Bakari ismail ni dereva wa Tax anasema kuwa amewahi kusimamisha Bashara yake kutokana uhaba wa mafuta. ''Nimewahi
kupaki gari wa muda wa siku nne, wateja wananipigia simu nawaambia kuwa
sina mafuta hadi nilivyopata mafuta nikaendelea na biashara'' Serikali imewezaje kuruhusu mafuta kuuzwa kwa namna hii? Mkuu
wa wilaya ya Mafia, Shaibu Nnondoma anasema kuwa wameruhusu wauzaji
hawa wa mafuta katika vibanda kutokana na usafiri wa mashua hauwezi
kuleta mafuta kwa wingi, hivyo wafanya biashara hawa wamekua na umuhimu
mkubwa katika upatikanaji wa mafuta kisiwani hapa. ''Wafanyabiashara
wadogo wadogo wananua kwa bei ya kawaida na wanakuja kuuza hapa,
tumewaruhusu wauze kwa bei ya soko itakavyowaruhusu kwasababu akiuza bei
ndogo sana hawezi kupata faida na wanasaidia sana wakazi wa
hapa''amesema Nnondoma. Hata hivyo hapo awali walikua wanauza
karibu na makazi ya watu , lakini uongozi wa kisiwa hiki uliwahamishia
mbali na makazi ya watu.
Comments
Post a Comment