Featured Post

KAMISHNA MSAIDIZI WA ARDHI KANDA YA MAGHARIBI AKUTANA NA WATENDAJI WA KATA MANISPAA YA TABORA

Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Magharibi akimpatia Hati za Madai Mtendaji wa Kata ya Kaloleni Manispaa ya Tabora Monica Toba kwa ajili ya kuziwasilisha kwa wadaiwa wa kodi ya ardhi katika kata yake wakati wa kampeni ya kuhamasisha ulipaji kodi ya ardhi mkoa wa Tabora. 


Na Munir Shemweta, Tabora
Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Magharibi Idrisa Keyera amesema manispaa ya Tabora pekee inadai zaidi ya shilingi bilioni sita kwa wamiliki wa ardhi na mashamba mkoani humo kama kodi ya ardhi.
Kayera alisema hayo jana wakati akizungumza na watendaji kata wa Manispaa ya Tabora alipokutana na watendaji hao kuhamasisha ulipaji wa kodi ya ardhi na mashamba katika mkoa huo, mkutano uliofanyika ukumbi wa VETA Tabora.
Alisema, mpaka kufikia sasa katika manispaa ya Tabora zimekusanywa jumla ya shilingi bilioni 3.2 ikiwa ni pungufu ya malengo waliyojiwekea ya kukusanya shilingi bilioni nne katika mwaka huu wa fedha unaoishia juni mwaka 2018.
Alisema, kanda yake inayohusisha mikoa ya Tabora, Shinyanga, Kigoma na Katavi imeanza kuchukua hatua kwa wadaiwa sugu wa kodi za ardhi kwa kuwapatia hati za madai ambapo wahusika watatakiwa kulipa madeni yao ndani ya wiki mbili na wasipofanya hivyo wanapelekwa mahakamani na huko vifaa vyao au nyumba zitauzwa kufidia deni huku umiliki nyumba ama shamba ukifutwa.
‘’Unapopelekwa mahakamani uwezekano wa kushinda haupo na pia itakulazimu kulipa gharama za madadlali kwa kushindwa kulipa’’ alisema Kamishana Msaidizi Kayera.
Kwa mujibu wa Kayera, kikao chake na watendaji wa kata za manispaa ya Tabora ni moja ya harakati za ofisi yake ya Kanda ya magharibi kuhakikisha kodi ya serikali inapatikana sambamba na kuwashirikisha watendaji kuwatambua na kuwapelekea hati za madai wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi katika mitaa yao ili kuwabana waweze kulipa madeni yao.
Aidha, Kamishna Msaidizi wa ardhi Kanda ya Magharibi alisema, utaratibu wa kulipa kodi ya ardhi kwa sasa ni rahisi kwani unaweza kulipia kwa njia ya simu na malipo hayo yanafanywa na wananchi waliopimiwa maeneo yao ingawa serikali iko katika hatua za kuhakikisha maeneo yote ya mijini hata yale yasiyopimwa wamiliki wake wanalipa kodi ya ardhi.
Kwa upande wao watendaji wa kata za manispaa ya Tabora pamoja na kuunga mkono jitihada za uhamasishaji wa ulipaji kodi ya ardhi wametaka kupatiwa taarifa pamoja na ramani za maeneo yao kwa lengo la kutambua maeneo hasa pale yanapotokea mabadiliko ya matumizi ya ardhi katika maeneo husika jambo linalowapa wakati mgumu wakati wa kutekeleza majukumu.
Hata hivyo, wametaka halmashauri ya Manispaa ya Tabora na ofisi ya Kamishna wa Ardhi Kanda ya Magaharibi kuwawezesha wakati wa kufanya kazi ya kuwapelekea wadaiwa wa kodi ya ardhi ikiwemo kuwapa motisha hasa wale watendaji wanaoishi maeneo ya pembezoni ambapo watendaji wake wamekuwa na wakati mgumu kuwafikia wananchi kutokana na kukosa nauli na gharama nyingine.
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia ofisi zake za Kanda imekuwa na kampeni kamambe ya kuhamasisha wananchi kulipa kodi ya ardhi na mashamba kabla ya Juni 30 mwaka huu wa 2018, huku wale wadaiwa sugu wakipatiwa hati za madai ili waweze kulipa madeni yao kabla ya hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.

Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Magharibi Idrisa Kayera akizungumza na watendaji wa Kata za Manispaa ya Tabora jana wakati wa kampeni ya kuhamasisha ulipaji wa kodi ya ardhi katika kanda hiyo mkoani Tabora, kampeni inayoendeshwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kushoto ni Mwanasheria wa Kanda Ramadhani Jongo.

Watendaji wa Kata za Manispaa ya Tabora wakimsikiliza Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Kanda ya Magharibi Idrisa Kayera (hayupo pichani) wakati wa kampeni ya kuhamasisha ulipaji kodi ya ardhi katika kanda ya magharibi mkoani Tabora, kampeni inayoendeshwa ma Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi. 

Mmoja wa watendaji wa kata  za Manispaa ya Tabora akichangia maoni wakati wa kampeni ya uhamasishaji wa kulipa kodi ya ardhi kanda ya magharibi ulioendeshwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Magharibi Idrisa Kayera akiwaonesha Hati ya Madai watendaji wa Kata za Manispaa ya Tabora wakati wa kampeni ya kuhamasisha ulipaji wa kodi ya Ardhi na Mashamba katika kanda hiyo mkoani Tabora jana, kampeni inayoendeshwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Magharibi akimpatia Hati za Madai Mtendaji wa Kata ya Mbugani Manispaa ya Tabora Paul Masunga kwa ajili ya kuziwasilisha kwa wadaiwa wa kodi ya ardhi katika kata yake wakati wa kampeni ya kuhamasisha ulipaji kodi ya ardhi mkoa wa Tabora.

Mmoja wa waendesha Bajaji katika Manispaa ya Tabora akibandika Stika ya uhamasishaji wa kulipa kodi ya ardhi katika Bajaji yake wakati wa kampeni ya kuhamasisha ulipaji kodi ya ardhi katika kanda ya magharibi mkoani Tabora, kampeni iliyoendeshwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Waendesha Bodaboda katika kituo cha mabasi katika manispaa ya Tabora wakiangalia vipeperushi vinavyoeleza njia rahisi ya kulipa kodi ya ardhi kwa simu wakati wa kampeni ya kuhamasisha ulipaji kodio ya ardhi katika mkoa wa Tabora, kampeni iliyoendeshwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Picha zote na Munir Shemweta Wizara ya Ardhi.








Comments