- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akifunga warsha ya wadau wa Sekta ya Fedha iliyolenga kujadili mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa viwanda leo Jijini Dodoma.
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Uamuzi wa Serikali wa kupunguza kiwango cha chini cha amana
kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na benki za biashara nchini, umechochea taasisi za fedha yakiwemo
mabenki kuanza kupunguza viwango vya riba ya mikopo hatua itakayochochea ukuaji
wa uchumi.
Hayo yalisemwa Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji wakati wa kufunga warsha ya wadau wa Sekta ya Fedha
uliowashirikisha wabunge, washirika wa Maendeleo, wakuu wa Taasisi za fedha na
Wizara ya Fedha na Mipango.
Dkt. Kijaji, alisema kuwa Serikali kupitia Benki Kuu
imeshusha riba ya mikopo kwa taasisi za fedha kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 9.0 na kupunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa
kuwekwa katika Benki hiyo na benki za biashara kutoka asilimia 10.0 hadi
asilimia 8.0 kuanzia mwezi Aprili 2017,
jambo ambalo limeleta matokeo chanya katika kuimarisha uwezo wa taasisi
kukopesha wateja wao.
Miongoni mwa Benki zilizoshusha viwango vyao vya riba za
mikopo ni CRDB ambayo imetangaza kushusha riba kutoka asilimia 22 hadi 16 na
kuongeza kiasi cha kukopa kwa wafanyakazi kutoka Sh. milioni 50 hadi Sh.
milioni 100 huku muda wa kurejesha ukiongezwa kutoka miaka mitano hadi saba.
Benki nyingine ni NMB
ambayo imeongeza muda wa marejesho ya mikopo kwa wafanyakazi, wajasiriamali
wadogo na wakubwa kutoka miezi 60 hadi 72, na
imepunguza riba ya mikopo kwa wafanyakazi kutoka asilimia 21 hadi 19 na
wajasiriamali wadogo kutoka asilimia 23 hadi 21.
Dkt. Kijaji amezipongeza benki zilizoshusha viwango vya
riba na ameitaja hatua hiyo kuwa ni
muhimu katika kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya viwanda hata kabla ya mwaka 2025
na kutoa wito kwa taasisi hizo za fedha kuitupia jicho sekta ya kilimo kutokana
na umuhimu wake katika kutimiza malengo ya kukuza viwanda.
Aidha, Dkt. Kijaji alisema kuwa Serikali imekamilisha andiko
“Blue Print” ambalo lengo lake ni
kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini ili kuleta tija kwa
wafanyabiashara na Sekta ya Fedha kwa ujumla
Alisema Serikali imeendelea kulipa malimbikizo ya madai
mbalimbali yaliyohakikiwa ya watumishi, wakandarasi na watoa huduma
wengine yaliyohakikiwa ili kuongeza
ukwasi katika jamii na kwa kwamba uhakiki uliofanyika umeokoa kiasi kikubwa cha
fedha za Serikali ambazo zingelipwa wakati madai hayakuwa sahihi.
Naibu Waziri huyo aliipongeza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa
kushiriki kwa vitengo katika utekelezaji wa Mpango huo kwa kutekeleza miradi ya
kimkakati ya kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari katika eneo la Mkulazi na
Mbigiri - Morogoro na mradi wa ujenzi wa
machinjio ya kisasa ya nyama eneo la Makunganya
mkoani humo.
Naye Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt.
Khatibu Kazungu, alieleza kuwa warsha hiyo iikuwa na manufaa makubwa na kwamba
Wizara inaandaa mkakati wa utekelezaji wa Sekta ya Fedha wa Miaka kumi ambao
utakujumuisha pia mawazo ya wadau hao.
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Prof.
Honest Ngowi, amepongeza hatua ya
Serikali ya kuwa na majadiliano na Sekta ya fedha kwa kuwa ina mchango mkubwa
katika kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Akitoa tathimini yake kuhusu utekelezaji wa Mpango huo,
Prof. Ngowi, alisema kuwa sehemu ya miradi kumi ya kipaumbele, ikiwemo ujenzi
wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa (SGR), ufufuaji wa Shirika la Ndege
na Ujenzi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi mkoani Morogoro, ni baadhi ya miradi
muhimu inayotekelezwa.
Kwa upande wao,
Mbunge wa Muheza Mhe. Adadi Rajab na Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Maria
Kangoye, wamezishauri Sekta za Fedha nchini kuiwezesha zaidi sekta ya kilimo
ili ikue haraka na kuishauri pia Wizara ya Fedha na Mipango, kufanya mikutano
ya namna hiyo na wadau kabla ya Bunge la Bajeti kuanza ii manufaa yake yaweze
kuwa makubwa zaidi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatib
Kazungu akizungumza wakati wa kufunga
warsha ya wadau wa Sekta ya Fedha
iliyolenga kujadili mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa viwanda leo
Jijini Dodoma.
PIX 0658
Mbunge wa Jango’mbe Mhe. Ally Hassan King akizungumza wakati wa
kufunga warsha ya wadau wa Sekta ya Fedha iliyolenga kujadili mchango wa
sekta hiyo katika kukuza uchumi wa viwanda leo Jijini Dodoma.
PIX 0633
Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA),
Dkt. Boghayo Saqware akizungumzia hoja
mbalimbali zilizoibuliwa na wajumbe wa
warsha ya wadau wa sekta ya fedha
iliyolenga kujadili mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa viwanda leo
Jijini Dodoma.
PIX 0521.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Dkt. Honest Ngowi
akiongoza mjadala wakati wa warsha ya
wadau wa sekta ya fedha iliyolenga kujadili mchango wa sekta hiyo katika kukuza
uchumi wa viwanda leo Jijini Dodoma.
PIX 0570.
Mmoja wa wadau wa Sekta ya Fedha akizungumzia umuhimu wa ushirikishwaji wa
sekta hiyo katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo hapa nchini ili
kuchochea maendeleo.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha
na Mipango)
Comments
Post a Comment