- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Dodoma, April 17, 2018:
Ahadi
hiyo imetolewa mjini hapa leo na Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia walipozungumza na waandishi wa habari kueleza utekelezaji
wa hoja za CAG katika sekta zao.
Akieleza
utekelezaji wa hoja mbalimbali katika sekta ya Afya, Waziri Ummy ameeleza kuwa
Wizara ya Afya, baada ya kupata taarifa ya CAG kuhusu kuongezeka kwa deni la
matibabu ya wagonjwa wanaopata rufaa nje ya nchi, imeamua kufanya uchunguzi wa
kina wa kitabibu na kihasibu kujua usahihi wa deni hili ili kuchukua hatua
madhubuti.
Aidha,
amesisitiza kuwa Wizara imekubaliana na ushauri wa CAG wa kuhakikisha Serikali
inaendelea kuboresha utoaji wa huduma za kibingwa hapa hapa nchini nchini ili
kupunguza gharama. Waziri Ummy ameeleza hatua mbalimbali zilizochukulia
kutekeleza agizo hilo ikiwemo kuanza kutolewa hapa nchini huduma za upasuaji wa
moyo, upandikizaji wa figo, uwekaji wa vifaa vya usikivu na matibabu ya
magonjwa ya mifupa na mishipa ya fahamu.
Kwa
upande wa huduma za kibingwa katika maradhi ya saratani, Waziri Ummy alisema
tatizo kubwa lililopo sasa ni huduma za kiwango cha juu cha kupima ugonjwa huo
ambazo hazipatikani sehemu nyingi za Afrika. Hata hivyo alisema katika mwaka
mmoja ujao Tanzania itamaliza tatizo hilo kwani Serikali imetenga Shilingi
bilioni 14.5 mwaka ujao wa fedha kununua mashine ya kupima saratani (PET-CT-SCAN)
.
Kuhusu
uingizwaji wa bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 1.94 kwa kutumia
vibali vya kughushi, Waziri Ummy amesema wameshachukua hatua za haraka kupitia
Bodi ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kuwabaini wote waliohusika na tayari
baadhi wameshakabidhiwa kwenye vyombo vya dola huku TFDA ikichukua hatua za
kujiunga na mfumo wa TRA ili kutambua nyaraka zisizo halali.
“Wizara
yangu itahakikisha kuwa maoni yote ya CAG yanaendelea kufanyiwa kazi kwa haraka
zaidi ili kuhakikisha hakuna senti ya wananchi katika sekta ya afya inatumika
kinyume na matarajio,” alisema Waziri Ummy.
Prof. Ndalichako: Tunakichunguza Kitengo
cha Manunuzi
Akizungumzia
maeneo kadhaa ya sekta ya elimu, Waziri Ndalichako amekubaliana na hoja
mbalimbali za CAG hasa katika eneo la ucheleweshaji wa ujenzi wa miradi
mbalimbali ya elimu ikiwemo ucheleweshaji wa mradi wa ujenzi wa shilingi
bilioni 4.6 katika Chuo cha Ualimu Ndala.
Prof.
Ndalichako amekiri kuwa kuna tatizo ndani ya Kitengo cha Manunuzi wizarani
kwake. Kufuatia hali hiyo, ameagiza uchunguzi kuhusu ufanisi wa Kitengo hicho
ambao utakamilika mwishoni mwa mwezi huu na amesisitiza kuwa hatasita kuchukua
hatua kali dhidi ya watakaobainika kuchelewesha miradi muhimu ya maendeleo.
Kwa
upande wa changamoto mbalimbali katika utoaji na ufuatiliaji wa madeni ya
mikopo ya Elimu ya Juu, Prof. Ndalichako ameeleza hatua mbalimbali ambazo
Serikali imezichukua ikiwemo kuteua Mkurugenzi Mkuu mpya wa Bodi ya Mikopo na
kuunda Bodi mpya Agosti mwaka jana; mabadiliko ambayo yameleta mageuzi katika
kupunguza muda wa wanafunzi kupata mikopo na vile vile kuongezeka makusanyo ya
madeni ya mikopo.
“CAG
alionesha kuwa miaka ya nyuma Bodi ilikuwa inakusanya kati ya Shilingi bilioni
32 na 48 za madeni ya mikopo. Lakini tangu iingie Serikali ya Awamu ya Tano na
mabadiliko yaliyofanyika, ukusanyaji umeongezeka hadi shilingi bilioni 116
mwaka 2016/17 na mwaka huu wa fedha hadi kufikia Machi, 2018 kiasi cha Shilingi
bilioni 132.20 ambazo ni sawa na asilimia 101 ya lengo la mwaka 2017/18,”
alisema na kuongeza:
“Nakiri
pia kwamba huko nyuma kulikuwa na udhaifu katika kuwatambua wadaiwa sugu. Hivi
sasa kazi inafanyika ambapo Bodi ya Mikopo imeongeza idadi ya kuwatambua
wadaiwa sugu kufikia 147,231 mwaka 2017/18 kutoka wadaiwa sugu 48 tu
waliobainishwa awali ambapo kati ya waliobainishwa jumla ya wadaiwa 42,213
wameshaanza kulipa madeni yao ya mikopo.”
Waziri
Ndalichako ametumia fursa hiyo kusisitiza kuwa Wizara yake pia imewaagiza
wataalamu na viongozi wote wa taasisi zilizo chini yake kuhakikisha kuwa
wanapitia neno kwa neno taarifa ya CAG ili kuhakikisha maeneo yote yenye
changamoto yanafanyiwa kazi.
Kesho
katika mfululizo wa mawaziri kueleza utekelezaji wa hoja za CAG itakuwa ni zamu
ya Wizara ya Nchi (Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira) na Wizara ya Maji na
Umwagiliaji.
Comments
Post a Comment