- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Mathias
Canal, NFRA-Dodoma
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa, leo Aprili 21, 2018 atakuwa mgeni rasmi
kwenye sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa kuongeza uwezo wa
uhifadhi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) katika dhifa
itakayofanyika kwenye viwanja vya Ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula zilizopo Kizota, eneo la Viwanda mjini Dodoma.
Mradi huo utagharimu Dola za Kimarekani milioni 55, ambao ni
mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland ikiwa ni sehemu ya kiasi cha
Dola milioni 110 kilichotolewa kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, mikataba ya ujenzi ilianza
kutekelewa Desemba 9, 2017 ambapo Mradi huo utatekelezwa na kampuni mbili za
Kandarasi kutoka Poland ambazo ni (Feerum S.A na Unia Araj Realizacje Sp.o.o) na
msimamizi wa mradi ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Vumilia Zikankuba,
ameeleza kuwa Mradi huo utahusisha ujenzi wa vihenge vya kisasa, maghala ya
kisasa, ujenzi wa ofisi na kutekelezwa katika maeneo nane ambayo ni
Babati-Manyara, Dodoma, Makambako-Njombe, Mbozi-Songwe, Shinyanga,
Songea-Ruvuma, Sumbawanga-Rukwa na Mpanda-Katavi.
Baada ya mradi kukamilika Wakala
utakuwa umeongeza uwezo wa kuhifahi ziada ya tani za ujazo 250,000 (vihenge vya
kisasa tani 190,000 na maghala tani 60,000) jambo ambalo litakuwa chachu na
mafanikio yenye tija katika kuunga mkono juhudi za utendaji wa serikali ya
awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli.
Kupatikana kwa Mradi huo nchini ni
jitihada za Serikali ambazo zitapelekea ukuaji wa uchumi nchini na kuchangia
kuwezesha Tanzania ya viwanda ambapo kutawezesha maghala ya Wakala kuweza
kuhifadhi akiba ya Chakula ambayo itaendana na mahitaji halisi ya dharura
kulinganisha na ongezeko la watu nchini.
Hifadhi ya Chakula inayohitajika kukidhi mahitaji ya dharula kwa
miezi mitatu ni zaidi ya tani 500,000 ukilinganisha na tani 150,000 iliyokuwa
inahitajika miaka ya 2008 Wakala ulipoanzishwa.
Aidha, Zikankuba alisema kuwa technolojia itakayotumika katika
ujenzi wa vihenge vya kisasa, itawezesha Wakala kupunguza gharama za
uendeshaji; kuhifadhi chakula kwa muda mrefu zaidi; kupunguza upotevu wa zao la
mahindi baada ya kuvuna (posthaverst
loss), kuongeza soko la mahindi nchini na kuimarisha usalama wa nafaka
inayohifadhiwa kwa kudhibiti sumukuvu (Aflatoxin)
kwa mahindi yaliyohifadhiwa.
Jitihada hizi zinalenga katika kuimarisha uwezo wa Taifa katika
kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Comments
Post a Comment