- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
*Asema Tanzania imechelewa sana, lazima isonge mbele
Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli,
amesema watu wanaopinga maendeleo yanayofanywa na serikali yake wana wivu na
kwamba hawana tofauti na mashetani.
akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa usimikaji wa
radar nne za kuongozea ndege jijini Dar es Salaam Jumatatu, Aprili 2, 2018,
Dkt. Magufuli alisema kwamba, watu wanaopinga jitihada za serikali wanaumia,
lakini hilo haliwezi kumfanya yeye na serikali yake wasiwaletee Watanzania
maendeleo.
"Nchi hii uwezo wake sasa ni mkubwa mno, ni wa maajabu.
Ndiyo maana watu wengine wenye wivu wivu hivi wanaumia sana. Na wenye wivu wapo
tu, hata Mungu aliumba malaika pakatokea wenye wivu mashetani yakagoma
yakatupwa huku duniani. Nayo lazima yawe na wafuasi fuasi wa aina fulani wenye
wivu wivu," alisema.
Awali, Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi,
Profesa Makame Mbarawa, alisema makataba wa mradi wa kusimika radar nne
uliingiwa tangu Agosti 22, 2017 baina ya Serikali na Kampuni ya Ufaransa ambao
utagharimu jumla ya Shs. 77.3 bilioni ambapo Mamlaka ya Usafirishaji wa Anga
(TCAA) itagharamia 45% na Serikali Kuu itagharimia 55%.
"Mradi huu umezingatia uendelevu hivyo umeweka dhamana
ya miaka 3 ili kuhakikisha mkandarasi analeta vipuri endapo hitilafu yoyote
itatokea. Pia mkandarasi atahakikisha vipuri vinapatikana kwa miaka 12 baada ya
hapo," alisema Prof. Mbarawa.
Profesa Mbarawa aliipongeza TCAA kwa matokeo mazuri ya
ukaguzi wa kimataifa wa ICAO (International Civil Aviation Organization) wa
viwango vya udhibiti wa kiusalama wa anga.
"Matokeo yameonyesha Tanzania imepanda katika viwango
vya Udhibiti wa Kiusalama wa Anga kutoka 37.8% za 2013 hadi 64.35% za 2017,"
alisema Prof. Mbarawa.
Lakini Dkt. Magufuli alisema kwamba, pamoja na jitihada
hizo, kuna watu wanaonyesha wazi kwamba hawafurahishwi na wamekuwa wakifanya
kila njia kupinga mambo yote mema yanayofanyika.
"Kwa sababu ni maajabu kwa nchi kama hii
Tanzania ambayo katika miaka mingi heshima yake ilipotea. Ulikuwa huwezi
ukayaona mawingu ya kitu kinapaa huko angani kilichoandikwa Tanzania.
"Nchi kubwa, watu milioni 55 hata ndege tulikuwa
tumekosa. Na ndege ndio heshima ya nchi. Tumeingia madarakani tukaamua lazima
tuwe na ndege. Wakasema pesa atapata wapi. Nikasema pesa ziko kwa mafisadi na
watazitema hata ikibidi kwa kutapika.
"Tukanunua ndege 6 bila kukopa. Zilipokuja hao hao
waliokuwa wanaponda ndio wa kwanza kupanda hizo ndege. Tunawasamehe sana,"
alisema Dkt. Magufuli.
Aidha, Dkt. Magufuli alisema kwamba, kwenye nchi
zilizostaarabika, huwa wanaungana hata wakiwa na itikadi tofauti.
"Tunajenga hivi vitu kwa ajili ya Watanzania wote na si
familia zetu tu," alisema. Akaongeza: "Sekta ya madini imechangia
11.5% hadi 17% baada ya sisi kubana wanyonyaji."
Rais Magufuli alisema kwamba, wapo watu duniani hata
ukiwabeba mgongoni ukawavusha mto wakifika ng'ambo watasema "limgongo lake
lilikuwa linanuka jasho".
" Tuwaombee tu, tusiyumbishwe tuko pazuri mno,"
alisema. "Wako watu waliokuwa wamezowea fedha za bure za kuwaibia maskini
hao ndio wanapiga kelele sana. Ninafahamu hata makanisani zaka zimepungua
sababu zilikuwa zinatolewa na mafisadi."
Dkt. Magufuli akaongeza: "Watendaji wangu wanafanya
kazi sana. Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wanafanya kazi ndiyo maana
tuko salama leo. Ilifikia kipindi hata kwenda Kibiti ilikuwa shida, hatukuona
mtu yeyote analaani."
Alisema wakati wa mauaji ya Kibiti hakuna aliyelaani wala
kutoa waraka, na sasa Kibiti kumekuwa salama watu wamekaa kimya.
"Ingawaje sipendi sana kulizungumzia hili kwa sababu
ninalijua wala halina msingi wala halitafanikiwa wala hakuna lolote. Kwa sababu
Serikali ipo nimekabidhiwa na wananchi kuilinda kwa nguvu zote. Na ninasema
kweli kweli; Wengine nawaangalia tu nawacheki nasema "Hiiiiiiiiii","
alisema.
Aliongeza kwamba, Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere) alishasaidia
nchi nyingine kupata uhuru, hivyo jukumu lake sasa ni kujenga uchumi wa taifa.
"Katika juhudi hizi watatokea wa kunung'unika, wa
kupiga kelele hata sitawasikiliza," alisema.
Aliongeza: "Kazi ya uongozi ni ngumu sana, unageuka
huku unakuta watu wanalalamika. Hata Wakina Musa walipata shida, unawavusha
watu unakuta wengine wameshajenga na sanamu la dhahabu."
Alitolea mfano miradi ya maendeleo kama Stiegler's Gorge,
Ndege 6, SGR ambayo haikuwepo miaka iliyopita na sasa inakwenda kwa kasi kwa
manufaa ya Watanzania.
Comments
Post a Comment