- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Daniel Mbega
HATIMAYE Serikali
imevunja ukimya na kutoa kauli kuhusu madai ya kutoonekana kwa matumizi ya Shs.
1.51 trilioni kwenye matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017 na
kueleza kwamba hakuna hata senti moja iliyopotea.
Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, aliliambia Bunge mjini Dodoma jana kwamba, madai
ya baadhi ya watu wasiolitakia mema Taifa na hasa Serikali ya Awamu ya Tano,
hayana msingi wowote kwa kuwa kila kitu kiko wazi.
Alisema,
kilichotokea na matumizi ya mfumo mpya wa viwango vya Kimataifa vya Uhasibu
katika sekta ya umma.
“Napenda kuliarifu
Bunge lako Tukufu na Watanzania kwa ujumla kwamba hakuna fedha taslimu ya
shilingi trilioni 1.51 iliyopotea au kutumika kwenye matumizi ambayo
hayakuidhinishwa na Bunge.
“Hivyo basi, madai
ya baadhi ya watu wasiolitakia mema Taifa letu na Serikali yetu ya Awamu ya
Tano hayana msingi wowote wenye mantiki. Haya yanadhihirishwa na aya zifuatazo
kwenye tamko hili la Serikali,” alisema.
Akifafanua zaidi, Dkt. Kijaji alisema kwamba, mfumo huo ulianza kutumika katika kipindi cha
2012/2013 hadi 2016/2017 ambacho kilikuwa cha mpito.
“Katika kipindi cha
mwaka 2012/13 hadi 2016/17, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ilikuwa
kwenye kipindi cha mpito cha miaka mitano ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa
kuandaa hesabu za Serikali kwa kutumia mfumo wa Viwango vya Kimataifa vya
Uhasibu katika Sekta ya Umma (International Public-Sector Accounting Standards
- IPSAS Accrual).
“Katika kipindi
hicho, Serikali iliendelea kukusanya taarifa mbalimbali kwa kutumia mfumo huu ili
kutuwezesha kutambua kikamilifu hesabu za mali, madeni pamoja na mapato
yanayotokana na kodi.
“IPSAS Accrual ni mfumo wa kiuhasibu
ambapo mapato yanatambuliwa baada ya muamala husika kukamilika na sio wakati
fedha taslimu inapopokelewa; na matumizi yanatambuliwa wakati muamala wa
matumizi umekamilika na sio wakati fedha inalipwa.
“Mfumo huu ni mzuri
na una faida nyingi ikiwa ni pamoja na miamala ya Mapato na Matumizi kutambuliwa
wakati husika na siyo wakati wa fedha taslimu inapopokelewa au kulipwa.
“Matokeo ya
utekelezaji wa Mpango Mkakati wa uandaaji wa hesabu kwa mfumo wa IPSAS Accrual umeiwezesha
Serikali na taasisi zake kutoa taarifa za kina na zinazoonesha uwazi na
uwajibikaji wa taasisi husika, hususan katika usimamizi wa mali na madeni ya
taasisi. Kuongezeka kwa uwazi, kumewawezesha watumiaji wa hesabu kupata taarifa
zinazowasaidia kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati.
Alisema, taarifa ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeeleza jumla ya mapato yote ya
Serikali kwa mwaka 2016/17, yalikuwa shilingi trilioni 25.3 ambapo fedha hizo
zinajumuisha mapato ya kodi, mapato yasiyo ya kodi, mikopo ya ndani na nje pamoja
na misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.
“Napenda kulitaarifu
Bunge lako Tukufu kwamba, kuanzia mwaka 2016/17, Mamlaka ya Mapato Tanzania
ilianza rasmi kuyatambua mapato kwa mfumo wa Accrual. Hivyo basi, kati ya mapato haya ya shilingi trilioni 25.3,
yalikuwemo pia mapato tarajiwa (receivables) kama mapato ya kodi yenye jumla ya
shilingi bilioni 687.3 pamoja na mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya jumla ya shilingi bilioni 203.92 (transfer
to Zanzibar),” alisema.
Aliongeza kusema
kwamba, katika uandishi wa taarifa ya ukaguzi,
CAG alitumia taarifa za hesabu na nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na Taarifa
za Utekelezaji wa Bajeti (Budget Execution Report) ambapo hadi kufikia tarehe
30 Juni 2017, mapato yalikuwa jumla ya shilingi trilioni 25.3 na matumizi yalikuwa
shilingi trilioni 23.79.
Matumizi hayo,
alisema, hayakujumuisha shilingi bilioni 697.85 zilizotumika kulipa dhamana na
hati fungani za Serikali zilizoiva.
“Matumizi haya
yalikuwa hayajafanyiwa uhamisho (re-allocation) wakati ukaguzi unakamilika.
Hivyo basi, baada ya kufanya uhamisho jumla ya matumizi yote kwa kutumia Ridhaa
za Matumizi (Exchequer issues) yalikuwa shilingi trilioni 24.4,” alisema.
Alisema kwamba,
shilingi trilioni 1.51 zilizodaiwa kutoonekana kwenye matumizi ya Serikali
zilitokana na matumizi ya dhamana na hati fungal zilizoiva (Shs. 0.6979
trilioni, mapato tarajiwa (Receivables – Shs. 0.6873 trilioni), mapato ya kodi
yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar (Shs. 0.2039 trilioni) na fedha
iliyotolewa zaidi ya mapato (bank overdraft) ilikuwa Shs. 0.0791 trilioni.
“Hii inamaanisha
kwamba, baada ya kupunguza mapato ya Zanzibar ya shilingi bilioni 203.92 na
kupunguza mapato tarajiwa ya shilingi bilioni 687.3, mapato halisi kwa mwaka
2016/17 yalikuwa shilingi trilioni 24.41.
“Aidha, baada ya kujumlisha
matumizi ya dhamana na hati fungani zilizoiva za kiasi
cha shilingi bilioni 697.85 kwenye matumizi ya shilingi trilioni 23.79 yaliyooneshwa
katika Taarifa ya CAG, ridhaa za matumizi zilizotolewa zilikuwa shilingi
trilioni 24.49 na kuleta ziada ya matumizi ya shilingi bilioni 79.07
ikilinganishwa na mapato. Kwa mchanganuo huu, ni dhahiri kwamba kwa mwaka
2016/2017 matumizi ya Serikali yalikuwa makubwa kuliko mapato kwa shilingi
bilioni 79.09 ambazo ni Overdraft
kutoka Benki Kuu ya Tanzania.
“Utaratibu wa kutoa
fedha zaidi ya mapato (Overdraft facility) uko kwa mujibu wa kifungu cha 34 cha
Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006,” alifafanua.
Dkt. Ashatu Kijaji alifafanua kwamba, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imepata
mafanikio makubwa katika uandaaji wa Hesabu za Serikali kwa kutumia mfumo huo wa
Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika Sekta ya Umma (IPSAS Accrual).
Alisema kwamba, katika
Afrika, Tanzania ndiyo nchi pekee iliyofanikiwa kwa kiwango kikubwa kuandaa
hesabu kwa kuzingatia matakwa ya IPSAS na kufanikisha kuandaa hesabu za
Majumuisho kwa kuzingatia mfumo huo.
“Kutokana na maelezo
haya ya Serikali, napenda kulitaarifa Bunge lako Tukufu na wananchi kwa ujumla
kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, ipo makini na haiwezi kuruhusu upotevu wa aina yoyote wa fedha za
umma.
“Dhamira ya Serikali
ya Awamu ya Tano ni kuona kwamba, kila mapato yanayokusanywa yanatumika
ipasavyo na kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania,” alisema.
Comments
Post a Comment