- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, George Lyego Longopa, kutoka Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete akichukua maelezo ya mgonjwa wa moyo katika hospitali ya Vwawa-Mbozi.
Na Mwandishi Wetu, Songwe
WAGONJWA 467 wenye
matatizo ya moyo wamebainishwa na kupatiwa huduma ya ushauri na matibabu kutoka
kwa madaktari bingwa waliotoa huduma kwenye kambi maalum ya siku 4 katika Hospitali
ya Vwawa-Mbozi Mkoani Songwe.
Timu ya Madaktari
Bingwa na wauguzi 5 wameeleza kuwa wagonjwa 18 kati ya hao waliowahudumia
wamepewa rufaa ya kufika hospitali za Rufaa kwa ajili ya matibabu zaidi.
Daktari Bingwa wa
Magonjwa ya Moyo, George Lyego Longopa, kutoka Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya
Jakaya Kikwete amesema wameanza matibabu siku ya Jumanne na kila Daktari
amekuwa akiona zaidi ya wagonjwa 60 kutokana na hamasa ya wagonjwa
waliojitokeza kupata matibabu ya magonjwa ya moyo.
“Tumeona
wagonjwa wengi na tumeamini kuwa Songwe tatizo la magonjwa ya moyo bado ni
kubwa, wagonjwa wengi wamekutwa na matatizo ya shinikizo la damu, moyo
kushindwa kufanya kazi vizuri pamoja na matatizo ya mishipa ya damu kuziba,”
amesema Dkt. Longopa.
Afisa Muuguzi Kutoka
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Flora Kasembe, ameeleza kuwa mtindo wa
maisha ya wananchi wa Songwe unaweza kuwa ni chanzo cha magonjwa ya moyo hasa
kutokana na uwepo vyakula vingi lakini wananchi hawali mlo kamili.
Kasembe amefafanua
kuwa, “Tumekuwa tukitoa elimu ya kuzingatia mlo kamili ili hivi vyakula vingi
vilivyopo huku visaidie kuimarisha afya na sio waishie kuuza tu bila wao
kutumia, pia wananchi wajenge mazoea ya kufanya mazoezi na endapo watabainika
na matatizo na wakaanzishiwa dawa wazitumie kwa usahihi waiache.”
Baadhi ya wagonjwa
waliohudhuria kupata matibabu ya moyo wameishukuru serikali kwa kusogeza huduma
karibu na utaratibu huo ufanyike mara kwa mara ili wananchi wengi wapate huduma
ya madaktari bingwa.
Brigita Haule ambaye
amepata matibabu ya moyo ameeleza kunufaika na huduma hiyo kwani hakuwa
akifahamu kama ana tatizo la moyo mpaka alipofika katika huduma hiyo.
“Wengi tunajiamini ni
wazima kwakuwa hatusikii kuumwa sana ila tunatembea na magonjwa mbalimbali
ambayo tunakuja kuyafahamu yakiwa katika hali mbaya, mimi pia sikufahamu kama
nina tatizo hivyo nawashauri wote tuwe na utaratibu wa kupima afya zetu,”
amefafanua Bi. Haule.
Kwa upande wake Kaimu
Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Kheri Kagya, amesema utaratibu wa kuwaalika madaktari
bingwa wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete uliangaliwa na uongozi
wa Mkoa baada ya kubaini kuwa kuna wagonjwa 210 wa moyo.
Dkt. Kagya ameongeza
kuwa wagonjwa waliojitokeza wamekuwa wengi kuliko matarajio ya awali huku
akieleza kuwa hayo ni mafanikio kwakuwa wameweza kuwabaini wagonjwa ambao
hawakutambulika hapo awali.
Afisa Muuguzi Kutoka Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kikwete Flora Kasembe akimpima shiniko la damu mwandishi wa habari
Manuel Kaminyoge katika hospitali ya Vwawa-Mbozi,
Baadhi ya wagonjwa wakisoma kipeperushi
kinachoeleza masuala ya lishe wakati wakisubiri kupata huduma ya madaktari
bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika
hospitali ya Vwawa-Mbozi.
Comments
Post a Comment