- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Dodoma, April 12, 2018:
SIKU
moja baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa
Assad kuwasilisha taarifa yake Bungeni na kisha kuongea na waandishi wa habari,
Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha utendaji wa tofauti katika kutekeleza na
kufanyiakazi hoja za ukaguzi.
Mawaziri
wote ambao wizara zao zimeguswa na hoja mbalimbali za ukaguzi, pamoja na
kuchukua hatua za haraka na kuwasilisha majibu rasmi Bungeni, kuanzia leo
wataeleza kwa umma kupitia waandishi wa habari hatua walizozichukua za
kufanyiakazi hoja husika.
Wakizungumza
na waandishi wa habari leo mjini hapa, Dkt. Phillip Mpango, Waziri wa Fedha na
Mipango, na Selemani Jafo, Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa), wakifungua mfululizo wa mikutano hiyo, wamesisitiza kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, haitaruhusu fedha
za umma zifanyiwe israfu.
Mawaziri
hao wameipongeza Ofisi ya CAG kwa kazi nzuri kwani taarifa zake za ukaguzi zinasaidia
lengo pana la Serikali ya Awamu ya Tano la kuhakikisha kila fedha inayokusudiwa
kuwasaidia wananchi, inatumika ipasavyo ili kuyabadili maisha yao.
Akijibu
utekelezaji wa hoja ya kuwepo mafuta yaliyosamehewa kodi ya Shilingi bilioni
11.05 lakini yalitumiwa na makampuni yasiyostahili, Dkt. Mpango amesisitiza
kuwa Serikali imefuatilia na kubaini hoja hiyo ni ya kweli. “Tayari Serikali
imechukua hatua na kiasi cha Shilingi bilioni 5.53. Juhudi za kukusanya kiasi
kilichobaki cha Shilingi bilioni 5.47 zinaendelea,” alisema.
Kuhusu hoja ya ongezeko
la deni la matibabu nje ya nchi la shilingi bilioni 17.13, Waziri Mpango
alisema deni hilo lilikua kutokana
na wagonjwa wanaolazimika kusaidiwa matibabu ya muda mrefu nje ya nchi hasa
saratani, kupandikizwa figo, mishipa ya fahamu, baadhi ya mahitaji ya upasuaji
wa mifupa, moyo na baadhi ya magonjwa ya watoto.
Akifafanua hatua
zilizochukuliwa kupunguza matumizi hayo miaka ijayo, Dkt. Mpango anasema kwa
miaka ijayo mkakati wa Serikali ni kuhakikisha tiba hizo zinapatikana hapa
nchini na tayari mafanikio yamepatikana.
“Hospitali
ya Muhimbili imeshaanza kupandikiza figo; hospitali ya Jakaya Kikwete inafanya
upasuaji wa moyo; Hospitali ya Ocean Road
inakamilisha kufunga mashine za kisasa, Hospitali ya Mloganzila ina vifaa vyote
na tutaajiri wataalamu wa kutosha; Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma inakamilisha
ufungaji vifaa vya kisasa, kuajiri mabigwa na imeshafanya upasuaji wa kwanza wa
kupandikiza figo Machi, 2018,” alisema.
Kuhusu upungufu katika
usimamizi wa fedha kwa mwaka 2016/2017, ambapo CAG amebaini ubadhirifu wa Shilingi milioni 332.86 katika Ubalozi
wa Tanzania, Maputo, Msumbiji, Dkt. Mpango amesisitiza kuwa tayari mtumishi
anayehusika amerejeshwa nyumbani na atafikishwa mahakamani.
Akizungumzia hatua
mbalimbali zilizochukuliwa katika sekta zake, Waziri Jafo amewaeleza waandishi
wa habari kuwa CAG kubaini vitabu 379 vya kukusanya mapato ndio havikuwasilishwa
ni mafanikio kwani katika ukaguzi wa mwaka uliopita, idadi hiyo ilikuwa kubwa
zaidi ikiwa ni vitabu 871. Alisema mfumo mpya wa kukusanya mapato kielektroniki
utakomesha kabisa tatizo hilo.
Hata hivyo, Waziri Jafo
amesisitiza kuwa kutokana na kasoro hiyo na nyingine za udhaifu na uzembe wa
baadhi ya watendaji, Serikali haitafumbia macho hali hiyo. “Jumla ya watumishi
434 wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu na kisheria baada ya kubainika
kuwa wamezisababishia Halmashauri zao hasara au hoja za ukaguzi zisizo za
lazima.” alisema.
Alizitaja hatua hizo na
takwimu zake kuwa ni: watumishi tisa (9) wamefukuzwa kazi, watumishi 210
wamepewa barua za onyo, watumishi 15 wamefikishwa kwenye vyombo vya dola na watumishi
28 wamesimamishwa kazi.
Aidha, watumishi wengine
13 wametakiwa kufidia hasara walizozisababisha kutoka kwenye mishahara yao,
watumishi wanne (4) wameshushwa vyeo, watumishi 10 wamebadilishwa majukumu, na watumishi
64 wapo katika mchakato wa hatua za kinidhamu.
Katika mfululizo wa
mikutano hiyo kesho Dkt. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo na Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
watazungumza na waandishi wa habari saa 5:00 asubuhi kwenye ukumbi wa Idara ya
Habari Bungeni.
Imetolewa
na:
Dkt. Hassan Abbasi,
Mkurugenzi, Idara ya
Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.
Comments
Post a Comment