- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Na Benny Mwaipaja, Abu Dhabi
MFUKO wa
Maendeleo wa Umoja wa Falme za Kiarabu-Abu Dhabi, umeipatia Tanzania mkopo wenye
masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 15, sawa na Shs. 34 bilioni za Tanzania,
kwa ajili ya kuboresha barabara ya Uvinza hadi Malagarasi yenye urefu wa
kilometa 51, kwa kiwango cha lami.
Hafla fupi
ya uwekaji saini wa mkataba huo ilifanyika katika makao makuu ya Mfuko huo
yaliyopo Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambapo Mhandisi Mussa
Ibrahim Iyombe, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa-TAMISEMI, amesaini kwa niaba ya Serikali, na Mhe. Mohamed Saif Al Suwaidi,
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi kwa niaba ya Mfuko huo.
Akizungumza
baada ya kusaini mkataba huo, Katibu Mkuu-TAMISEMI, Mhandisi Mussa Iyombe, alisema
kuwa barabara hiyo ni muhimu kwa kuwa ni kiungo kikuu cha usafiri wa abiria na
mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Kigoma na nchi jirani za Burundi
na Congo DRC.
Alisema
kuwa uamuzi wa Serikali wa kuboresha barabara hiyo kwa kiwango cha lami
umelenga kuchochea uchumi wa nchi kwa kuwezesha usafirishaji wa mazao ya
wakulima pamoja na kupunguza gharama na kuongeza uwezo wa kufanya biashara na
nchi hizo jirani.
“Tutabakiwa
na kipande cha barabara yenye urefu wa kilometa 28 kutoka Urambo hadi Kaliua na
kilometa 42 kutoka Chagu hadi Kazilambwa, barabara ambazo Serikali inaendelea
kuzitafutia fedha ili kukamilisha barabara yote inayoelekea ukanda huo wa kati
kutokea Dar es Salaam, Manyoni (Singida), Tabora hadi Kigoma,” alisema Mhandisi
Iyombe.
Aliushukuru
Mfuko huo kwa kuendelea kuiamini Serikali na kutoa mkopo huo wenye masharti
nafuu baada ya kufanya hivyo hivi karibuni kwa kutoa mkopo mwingine wa Dola
milioni 57, uliofanikisha kuboreshwa kwa barabara ya Kidahwe hadi Uvinza yenye
urefu wa kilometa 77 kwa kiwango cha lami.
Mkurugenzi
Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi, Mhe. Mohamed Saif Al Suwaidi, kwa
upande wake, amesema kuwa Mfuko huo uko tayari kushirikiana na Serikali ya
Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Alifafanua
kuwa mradi huo ambao mkataba umesainiwa mjini Abu Dhabi, utakuwa ni wa nne
kufadhiliwa na Mfuko wake Tangu uhusiano wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na
Tanzania uanzishwe mwaka 1977, ukiwemo mradi wa kuendeleza kiwanda cha Sukari
cha Kagera, Mradi wa Maji Vijijini huko Visiwani Zanzibar na Mradi wa kuboresha
barabara ya Kidahwe hadi Uvinza kwa kiwango cha lami.
Kwa upande
wake, Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Mhe. Mbarouk
Nassor Mbarouk, alisema kuwa kusainiwa kwa mkataba huo ni kiashiria cha
kukubalika kwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John
Pombe Magufuli, katika kuwaletea wananchi wake maendeleo ya haraka na kuungwa
mkono na Jumuiya ya Kimataifa.
“Hatua hii
ni uthibitisho wa mahuasiano mazuri ya kihistoria na kidugu kati ya Tanzania na
Umoja wa Falme za Kiarabu uliodumu kwa muda mrefu tangu mwaka 1977,” alisisitiza
Mhe. Mbarouk
Mhe.
Mbarouk amebainisha kuwa kukamilika kwa barabara hiyo ya Uvinza hadi Malagarasi
kutachochea maendeleo ya kiuchumi na mapinduzi ya viwanda kwa kuunganisha
shughuli za kiuchumi kama vile kilimo na maliasili pamoja na kukuza utalii.
Comments
Post a Comment