- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII NA WIZARA YA KILIMO, MALIASILI, MIFUGO NA UVUVI YA ZANZIBAR ZAWEKA MKAKATI WA KUIMARISHA MUUNGANO
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Waziri wa Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi.
Wizara ya Maliasili na Utalii ya Tanzania Bara na Wizara ya
Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi ya Zanzibar zimeweka mkakati wa pamoja wa
kuimarisha ushirikiano wa usimamizi wa maliasili, malikale na kuendeleza utalii
kwa maslahi ya pande zote za Muungano.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na
Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi baada ya mkutano wa pamoja wa wizara hizo
uliofanyika hivi karibuni katika Chuo cha Taifa cha Utalii Jijini Dar es
Salaam.
Mkutano huo wa siku moja uliongozwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya
Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Joseph
Meza.
Akifungua Mkutano huo wa siku moja, Maj. Gen. Milanzi
alisema pamoja na Wizara hizo kutokuwa za muungano imekuepo haja kubwa ya
kukutana kwa ajili kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha sekta ya
maliasili na utalii na kukabiliana na changamoto zinazogusa sekta hiyo katika
Muungano.
"Tumejadiliana kuona ni namna gani tunaweza kushirikiana
kwenye masuala mbalimbali ya biashara ya mazao ya misitu, biashara ya
Wanyamapori inayohusiana na mikataba ya CITES na mikataba mingine ya ndani na
ya Kimataifa.
"Tumekubaliana pia kuhuisha sheria zinazokinzana katika
usimamizi wa sekta tunazozisimamia ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza
katika utekekezaji na hivyo kuathiri Muungano wetu," alisema Maj. Gen.
Milanzi.
Alisema katika mkutano huo wa siku moja wataalamu kutoka pande
zote za Muungano waliagizwa kuwasilisha mapendekezo ya namna bora ya kuendesha
biashara ya mazao ya misitu na kupendekeza utaratibu wa kufanya biashara kwa
kuzingatia Sheria na Kanuni zilizopo.
Alisema kupitia mkutano huo Wizara hizo zimeunda kamati maalum
ya kuratibu utekelezaji wa maazimio ya pamoja ya kuimarisha usimamizi bora wa
sekta hizo na utatuzi wa changamoto zilizopo kwa kuandaa mapendekezo ya
kimkakati ya muda mfupi na mrefu.
"Kamati hiyo itaongozwa na Afisa Mipango Mkuu Msaidizi
kutoka Idara ya Misitu na Maliasili Zisizorejesheka (DFNR), Saleh Kombo Khiari
na Mchumi kutoka Idara ya Sera na Mipango Wizara ya Maliasili na Utalii, Mugure
Wambura," alisema Milanzi.
Mbali na hayo alisema kutakuwepo na vikao mbalimbali vya
kuimarisha Muungano kupitia Wizara hizo katika ngazi ya wataalamu, Makatibu
Wakuu na Mawaziri ambapo kikao kingine kinatarajiwa kufanyika kabla ya tarehe
30 Machi, 2018.
Comments
Post a Comment