Featured Post

WASHIRIKA WA MAENDELEO WAAHIDI KUSHIRIKIANA KWA KARIBU ZAIDI NA TANZANIA KULETA MAENDELEO

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kulia) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Malawi na Somalia, Bi. Bella Bird, nje ya ukumbi wa Mikutano wa St. Gasper Mjini Dodoma, walipokutana kujadili namna pande hizo mbili zinavyoweza kuimarisha ushirikiano wa kimkakati zaidi ili kuharakisha maendeleo ya nchi.

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) imekubaliana na Washirika wa Maendeleo kurejesha uhusiano wa karibu na wenye tija ili kusaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka Mitano pamoja na Mkakati wa Kukuza Uchumi Zanziba (MKUZA III).

Hayo yamebainishwa mjini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, wakati akifungua mkutano wa Mazungumzo ya kimkakati kama ilivyobainishwa kwenye Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo.
Bw. James amesema kuwa Mwongozo huo wa miaka 7, kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2014/2025, umelenga kuipa Serikali nafasi ya kuongoza mchakato wa maendeleo na kuijengea Serikali uwezo wa kukusanya mapato yake ya ndani, kuchambua fursa muhimu za uwekezaji na kutumia masoko ya kikanda na kimataifa kupata faida.
"Tumekubaliana kwamba tutasimamia mchakato mzima wa maendeleo sisi wenyewe kama nchi, matumizi mazuri ya rasilimali, kuimarisha uwajibikaji, kukuza biashara na uwekezaji wa ndani na nje" alifafanua Bw. James.
Amesema kuwa nchi inajivunia hatua kubwa iliyofikiwa kiuchumi na kijamii ambayo Tanzania imefikia, ikiwemo kutambuliwa kimataifa kuwa kinara wa masuala ya ukuaji wa uchumi wa Taifa na uchumi jumuishi, ambapo imekuwa ikifanya vizuri kimataifa, kikanda na katika nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara.
Akizungumza katika mkutano huo uliowashirikisha Washirika wa Maendeleo kutoka nchi mbalimbali duniani, Mratibu wa Umoja wa Mataifa na kiongozi wa washirika hao Bw. Alvaro Rodriguez, ameahidi kuwa watashirikiana na Tanzania ili malengo yake ya maendeleo yaweze kufikiwa kwa kuboresha zaidi ushirikiano ambao hapo awali ulianza kulegalega.
Ameelezea kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali zote mbili-Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar katika kufanikisha malengo yake ya kukuza uchumi kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo (FYDPII) na Mkakati wa Kukuza Uchumi Zanzibar (MKUZA III).
Amesema ili mipango hiyo iweze kufanikiwa kuna umuhimu wa kuishirikisha kikamilifu Sekta Binafsi pamoja na washirika wa maendeleo kwa kuweka mazingira ya kuongeza uzalishaji, kukuza ajira kwa vijana wa kike na wa kiume na hatimaye kufanya mapinduzi ya kiuchumi.
"Vijana takribani milioni moja wanaingia katika soko la ajira kila mwaka, hivyo ni muhimu kuweka mazingira ya upatikanaji wa ajira tena zenye staha katika kipindi hiki ambacho nchi inafanya mapinduzi makubwa ya viwanda na uchumi" alisisitiza Bw. Rodriguez.
Amesema kuwa uwekezaji katika masuala ya elimu, afya, hifadhi ya jamii, kutoa fursa sawa kwa wote (wanaume na wanawake) ni muhimu kwa kuwa jamii yenye afya itashiriki vizuri katika masuala ya uzalishaji.
Ameahidi kuwa Wadau wa Maendeleo wako tayari kusaidia jitihada hizo ili kuhakikisha kuwa Tanzania inafikia malengo hayo kwa kuwezesha miundombinu ya ukusanyaji mapato yake ya ndani, usimamizi na matumizi mazuri ya fedha za umma, kuiwezesha sekta binafsi kushiriki katika miradi ya kielelezo pamoja na kusaidia kuibua sera bora na kufadhili miradi yake ya maendeleo.
Serikali na Washirika wa Maendeleo wamekubalina kukutana mara mbili kwa mwaka ambapo kikao kingine kinatarajiwa kufanyika mwezi Novemba, 2018.
  
Meza Kuu ikiongozwa na Mwenyekiti wa Mkutano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (wa tatu kulia), kushoto kwake ni Mwenyekiti Mwenza na Mratibu wa Umoja wa Mataifa na kiongozi wa washirika hao wa Maendeleo Bw. Alvaro Rodriguez, mjini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi Bi. Doroth Mwanyika (kulia) na  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango (Sera) Dkt. Khatibu Kazungu, wakifuatilia kwa makini mkutano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo uliofanyika katika ukumbi wa St. Gasper Mjini Dodoma.
Mwakilishi wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania katika mkutano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo, Bw. Dickson Lema (kushoto) akifuatilia mjadala kati ya pande hizo mbili uliolenga kuimarisha zaidi ushirikiano, uliofanyika mjini Dodoma.
Mratibu wa Umoja wa Mataifa na kiongozi wa washirika wa Maendeleo nchini Tanzania, Bw. Alvaro Rodriguez, akihutubia mkutano wa kimkakati wa maendeleo kati ya Serikali ya Tanzania na Washirika wa Maendeleo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa St. Gasper Mjini Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James akihutubia washiriki  wa mkutano wa  kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo uliofanyika mjini Dodoma ukilenga kuimarisha mahusiano kati ya pande hizo mbili ili kuiwezesha nchi kufikia malengo yake ya maendeleo.
Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. John Rubuga na Kansela Mkuu, Ushirikiano na Maendeleo wa Canada Bi. Susan Steffen, wakifuatilia kwa makini mijadala mbalimbali kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo ili kufanikisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mkakati wa Kukuza Uchumi Zanzibar (MKUZA III)), uliofanyika mjini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kulia) akisalimiana na Mkuu wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani- USAID Bw. Andy Karas, nje ya ukumbi wa Mikutano wa St. Gasper Mjini Dodoma, walipokutana kujadili namna Serikali na Washirika wa Maendeleo wanavyoweza kuimarisha ushirikiano wa kimkakati zaidi ili kuiwezesha nchi kuharakisha maendeleo yake kwa manufaa ya wananchi wake.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)


Comments