Featured Post

NAIBU WAZIRI BITEKO AWATAKA WAMILIKI WA LESENI KUIGA MFANO WA KIWANDA CHA KUKATA NA KUSUGUA MAWE CHA MARMO KATIKA UONGEZAJI THAMANI YA MADINI


Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akikagua  mawe yaliyo katwa, Kusagwa na kuongezewa thamani katika kiwanda cha Marmo E. Granite Mines (T) Ltd wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Mbeya, Jana 20 Februari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal, Wazo Huru Blog
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko  akiwasili katika kiwanda kinachoshughulika na kukata, Kusaga na kuuza mawe cha Marmo E. Granite Mines (T) Ltd wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Mbeya, Jana 20 Februari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko (Katikati) akisikiliza maelezo kutoka kwa Ndg Salim Jesa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Marmo E. Granite Mines (T) Ltd kuhusu usafirishaji wa mawe baada ya kuyaongezea thamani wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Mbeya, Jana 20 Februari 2018.
Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akikagua  utendaji kazi wa kiwanda cha kukata, Kusaga na kuuza mawe cha Marmo E. Granite Mines (T) Ltd wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Mbeya, Jana 20 Februari 2018.

Na Mathias Canal, Mbeya

Wamiliki wa leseni za madini ya dhababu, vito na mengineyo kote nchini wametakiwa kuiga mfano wa Ndg Salim Jesa mmiliki wakiwanda cha Marmo E. Granite Mines (T) Ltd kinachojishughulisha na kukata, Kusaga na kuuza mawe kwa kufanya mchakato mzima mpaka bidhaa kukamilika hapa hapa nchini.

Kauli hiyo kwa wamiliki wa leseni za madini nchini imetolewa leo 20 Februari 2018 na Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Doto Mashaka Biteko wakati akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Mbeya.

Alisema kuwa kiu ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ni kuona rasilimali za nchi zinaongezwa thamani zikiwa ndani ya nchi jambo ambalo linaakisi umakini wa utendaji na ulipaji kodi ya serikali pasina kukwepa ama kutorosha rasilimali madini yakiwa ghafi.

Aliseama kuwa faida ya kuongeza thamani ya madini nchini ndio muarobaini wa sekta ya madini kuongeza kiwango cha uchangiaji wa pato la Taifa hatimaye kufikia asilimia 10% kama ulivyo mpango wa wizara kuongeza kiwango cha uchangiaji wa pato la Taifa.

“Nchi nyingi ambazo zimejua siri hii kwa kiasi kikubwa zimefanikiwa lakini sisi Tanzania tulichelewa sana, na kama tungeendelea kuchelewa ingefika kipindi ambacho madini yasingekuwepo kamwe na kama Taifa tungeambulia mashimo makubwa na kusalia katika wimbi la umasikini” Alisema Mhe Biteko

Aidha, amemuhikishia mmiliki wa kiwanda hicho kuwa serikali itazungumza na taasisi zinazofanya kazi za ujenzi nchini kuunga mkono juhudi za umahiri wa kiwanda hicho kwa kununua bidhaa zinazozalishwa hususani wakati huu ambao serikali inaendelea na mchakato wake wa kuhamia Mjini Dodoma.

Sambamba na hayo pia uongozi wa kiwanda hicho umempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli kwa kuweka sera nzuri hususani kwa wawekezaji wa ndani katika sekta ya madini na juhudi zake za kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na serikali kwa ujumla wake.

Kampuni ya Marmo E. Granite Mines (T) Ltd iliyopo mkoani Mbeya ilianzishwa mradi wa kukata, kusaga na kuuza mawe Januari 2004 baada ya kukidhi masharti ya usajili wa makampuni.

Comments