- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
MILA na desturi zilizojengeka katika jamii ya Kimasai ya kutowajengea watoto wa kike na wa kiume makazi rasmi ya kudumu katika kaya zao zimedaiwa kuchangia ngono katika umri mdogo na mimba za utotoni.
Hayo yalisemwa na washiriki wa warsha ya elimu ya afya ya uzazi na elimu kwa mtoto wa kike wilayani Ngorongoro.
Warsha ya elimu ya uzazi na elimu kwa wasichana inaendeshwa na Shirika la Umoja la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kuwajumuisha washiriki zaidi ya 60 wakiwemo wanafunzi, akina mama, walimu na maofisa wa elimu na afya wilayani Ngorongoro.
Lengo la warsha hiyo ni kutoa elimu rika ya afya ya uzazi na elimu kwa mtoto wa kike ili kufanikisha malengo yao ya maisha.
Washiriki hao walisema kwa mujibu wa desturi na mila, watoto wa kike na wa kiume huwa hawana mahali rasmi na salama pa kulala mara wanapokuwa wamebalehe kwa kuwa hulazimika kuondoka kwenye boma.
Washiriki hao wamesema mara baada ya giza linapoingia, kumaliza kazi na kula chakula cha usiku, vijana huondoka nyumbani na kwenda mahali popote ambapo anaweza kupata mahali pa kulala bila wazazi kujali alikolala na wala hawaulizwi wamelala wapi na iwapo ni salama.
Mara nyingi, washiriki hao wameongeza, kwa kuwa huwezi kulala mahali pamoja kila siku kutokana na mwendelezo wa mila hiyo, vijana huishia katika ngoma za usiku zijulikanazo kama ‘esoto’ na ndiko vishawishi vya ngono vinapotokea.
Kwa kuwa akinamama ndio wanaojenga nyumba (boma) za Kimaasai, vijana wameombwa kujenga mazingira mazuri katika maboma yao kuhakikisha kuwa kunakuwa na nyumba ambayo itajengwa mbali na pale wanapolala wazazi ili kudumisha mila, lakini pia kulinda utu wa mtoto wa kike.
Mimba za utotoni katika jamii ya Kimaasai zinaongezeka kwa kasi pamoja na mambo mengine ni kutokana na tamaa ya mali, mila na desturi ya kutowapatia wasichana mahali maalum pa kulala usiku.
Comments
Post a Comment