MAAFISA Ugani wa Kata na Vijiji
wilayani Lushoto mkoani Tanga wametakiwa kuacha tabia ya kukaa ofisini
badala yake wahakikisha wanakwenda kwa wakulima ili kuwapa elimu ya
namna ya kulima kilimo cha kisasa ambacho kitakuwa na tija kwao hali
itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa mazao yao. Kauli hiyo ilitolewa na Mbunge wa Jimbo la Lushoto (CCM) Shabani
Shekilindi alimaarufu Bosnia wakati wa ziara yake wa kuwatembelea
wananchi katika vijiji mbalimbali iliyokuwa na lengo la kuhamasisha
kujikita kwenye shughuli za uzalishaji na kusikiliza kero
zinazowakabili.
Akiwa kwenye kijiji cha Lwandai Kata ya Mlola, Mbunge huyo alisema wapo
baadhi ya maafisa ugani wamekuwa wakikaa ofisini badala ya kwenda wa
wananchi ambao wanajishughulisha na kilimo ili waweze kuwapa elimu ya
namna ya kulima kisasa jambo ambalo limekuwa likichangia kurudisha
maendeleo yao nyuma.
“Ndugu zangu maafisa ugani tambueni kuwa mnajukumu kubwa la kuhakisha
mnakwenda kwa wananchi kuwaelimisha juu ya kulima kilimo chenye tija
kwao kwani hiyo itawasaidia kuweza kupata mafanikio kuliko wanavyofanya
sasa lakini pia acheni kukaa ofisini “Alisema.
“Kwani elimu ambayo mnaweza kuitoa inaweza kuwa chachu ya wakulima
kuweza kulima mazao mazuri yatakayokuwa ya ushindani na soko la kisasa
hivyo jambo hilo ni muhimu sana “Alisema.
Alisema iwapo wakulima wataweza kufikiwa kwa wakati wataweza kuongeza
tija kwenye uzalishaji ili kuweza kujiandaa vema na ujio ya fursa
mbalimbali za miradi mikubwa inayokuja mkoani hapa ikiwemo bomba la
mafuta ghafi kutoka hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga.
“Niwaambie ndugu zangu hii ni fursa muhimu kwa mkoa wa Tanga na wakulima
ambao walikuwa wanazalisha mazao yao na kupeleka Dar es Salaam kwa
kutumia usafiri wa laki nane hadi tisa lakini sasa mtakuwa mkitumia hata
laki nne mpaka Tanga mjini kwani mradi ukianza kutakuwa na soko la
uhakika”Alisema.
Aidha pia mbunge huyo alitumia nafasi hiyo kuwataka wakulima
kubadilika kwa kuongeza uzalishaji kutokana na uwepo wa soko la uhakika
kwenye mazao yao katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya mkoa kwa lengo
la kuinua vipato vyao.
Naye kwa upande wake,Mwenyekiti wa Kijiji cha Lwandai Kata ya Mlola
wilayani humo,Juma Khamisi alimuhaidi mbunge huyo kuwa watashirikiana na
maafisa ugani waliopo kwenye maeneo yao ili kuhakikisha wananchi
wanapata elimu juu ya kulima kilimo chenye tija ili waweze kunufaika.
“Mh Mbunge tumepokea kauli yako kwa mikono miwili na sisi kama viongozi
wa kijiji hiki tutahakikisha tunashirikiana na maafisa ugani,wakulima
kwa lengo la kuongeza uzalishaji ambao utakuwa chachu ya kuweza kuwainua
kiuchumi kwa kuchochoea kasi ya maendeleo kwao “Alisema.(Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha)
Comments
Post a Comment