- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Unknown
on
- Get link
- X
- Other Apps
Maulid
Dilunga (kushoto) enzi ya uhai wake akiwa kamisaa wa mchezo wa soka. Picha kwa
hisani ya Bin Zubeiry.
Na
Daniel Mbega
ILIKUWA jioni yenye majonzi na simanzi
kupindukia kwa wachezaji, viongozi na wapenzi wa Sunderland Jumamosi ya Juni
Mosi, 1968, kwani siyo tu siku hiyo walipata kipigo kisichovumilika cha mabao 5-0 kutoka kwa Yanga, bali pia kipigo hicho kilitia saini Yanga
kuchukua ubingwa wa soka nchini.
Kipigo hicho kilikuwa kikiuma zaidi
ikikumbukwa kuwa, katika mechi ya kwanza ya ligi hiyo mwaka huo baina yao,
mchezo ulivunjika baada ya fujo kuibuka kufuatia Yanga kujipatia goli la kwanza
kwenye dakika ya 28 kupitia kwa Kitwana ‘Popat’ Manara. Hii sasa ilikuwa ni
mechi ya marudiano ili kumpata bingwa.
Vinara wa Yanga katika mechi ya marudiano
walikuwa washambuliaji hatari wa timu hiyo, Maulid Dilunga na Salehe Zimbwe
waliofunga magoli mawili kila mmoja, na Kitwana Manara alifunga goli moja
lililokamilisha kifo cha Sunderland siku hiyo.
Katika mchezo huo wa Ligi ya Taifa
uliofanyika kwenye Uwanja wa Ilala (sasa Kumbukumbu ya Karume), Yanga
iliinyanyasa zaidi Sunderland ikielekea kuumudu mchezo katika kila idara kuliko
wapinzani wao na kuwadhibiti ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kucheza watakavyo.
Awali Sunderland walikuwa wamelalamika kutaka
mchezaji wao Emmanuel Mbele, aliyefungiwa kutocheza mpira kwa kipindi cha miezi
6 kwa kusababisha mchezo wa kwanza kuvunjika, afunguliwe. FAT ikakataa kwa
kufuata sheria, lakini Yanga, wakiwa wanajiamini, wakaiomba FAT imwachilie huru
mchezaji huyo aliyekuwa tegemeo kubwa la ushambuliaji kwa timu yake. Hivyo,
akaachiliwa, lakini bado maji yakawa mazito kwa Sunderland.
Ukiondoa rafu za hapa na pale zilizojitokeza
mara kwa mara, mchezo ulikuwa wa kuvutia ambapo timu zote zilipigana kiume
ingawa hatma ya yote Yanga walitoka kifua mbele wakiwa na ushindi mkubwa
uliowachukua Sunderland (baadaye Simba) karibu miaka 10 hadi mwaka 1977
walipokuja kulipa kisasi kwa kushinda kwa magoli 6-0, kipigo ambacho
kinaelezewa kuwa kilitokana na Yanga kuwa ndio kwanza imetoka kwenye mgogoro
mkubwa uliopelekea kufukuzwa kwa wachezaji wake wazoefu wote, hivyo kuingia
uwanjani ikiwa haijatengemaa sawa sawa kwa mikiki mikiki ya ligi.
Katika dakika ya 10 ya mchezo huo, Omari
Kimimbi wa Sunderland aliumia baada ya kugongana na golikipa wa Yanga, Elias
Michael, katika harakati za kuwania mpira. Kama utakumbuka vyema, mwaka 1974
kwenye mchezo mwingine wa ligi kati ya timu hizo mbili, golikipa Elias Michael
wa Yanga na marehemu Willy Mwaijibe wa Sunderland waligongana kiasi cha
kulazimika kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando mjini Mwanza kwa matibabu
ya haraka. Pambano hilo lilifanyika kwenye Uwanja wa Nyamagana.
Karamu ya magoli ya Yanga katika mchezo wa
Juni Mosi, 1968 ilianza kwenye dakika ya 18 pale Durban wa Sunderland
alipounawa mpira kwenye mstari wa goli alipokuwa akijaribu kuokoa huku golikipa
wao, Mbaraka Salum akiwa ‘amekwenda marikiti’. Kufuatia kitendo hicho cha
kuunawa mpira, Yanga ilipewa penati ambayo Maulid Dilunga hakufanya makosa
kuzitikisa nyavu za Sunderland kuandika goli la kwanza.
Jitihada zote za Sunderland kusawazisha goli
hilo hazikuzaa matunda, kwani ukuta wa Yanga ulisimama imara. Alikuwa ni
Dilunga tena, ambaye siku hiyo ‘control’ yake ya mpira haikuwa na mpinzani,
aliyeandika goli la pili kufanya timu ziende mapumziko huku Yanga ikiongoza kwa
magoli 2-0.
Kwenye kipindi cha pili, Salehe Zimbwe
alifungua kitabu cha magoli kwa kupachika goli la tatu kwa Yanga kwa mpira wa
kichwa baada ya kumvisha kanzu golikipa wa Sunderland, Mbaraka Salum.
Sunderland walicharuka baada ya goli hilo, lakini Emmanuel Mbele ‘Dubwi’, Saidi
Abdallah ‘Walala’, Adamu Athumani na Hamisi Kilomoni walikosa nafasi za wazi
kabisa katika kile kilichoonekana kama ‘Sikio la kufa halisikii dawa’.
Vibao vya magoli viliendelea kusomeka 3-0
hadi zikiwa zimesaliwa dakika nne tu Sunderland waliporuhusu magoli mawili ya
haraka haraka. Kwenye dakika ya 87 Dilunga alimmegea krosi nzuri Kitwana
Ramadhani Manara aliyeachia kombora safi na kufunga goli la nne kwa Yanga kabla
Salehe Zimbwe naye hajaipangua ngome ya Sunderland na kuweka mpira kimiani
kufanya kitabu kifungwe huku Yanga ikijidai na ushindi wa magoli 5-0, ambao
hawajaukaribia tena hadi hii leo katika mechi dhidi ya watani wao wa jadi.
Kwa kuwa dakika zilikuwa chache, Yanga
walianza mchezo wa mzaha na maonyesho (show-game) ili kuvuta muda. Wachezaji wa
Sunderland walikatishwa tamaa na kuudhika sana. Katika mzaha wao, Yanga
walikuwa wanakokota mpira kutoka golini kwa wapinzani wao hadi golini kwao na kumpasia
mlinda mlango wao Elias Michael. Naye aliurudisha mpira kwa wachezaji wa ndani,
ambao walifanya dhihaka kwa wachezaji wa Sunderland huku wakicheka na kufunga
soksi au kufanya kama wanavua jezi au kaptura zao.
Wakati ambapo Emmanuel Mbele na Adamu Athumani
wa Simba walionywa kwa mchezo mbaya, Juma Bomba wa Yanga aliumia kwenye kipindi
cha pili na kupelekwa hospitali kwa matibabu huku Twaha Masimenti akiingia
kuchukua nafasi yake. Mechi ilisimamishwa kwa dakika tano wakati mashabiki
walipovamia uwanja lakini FFU walizima vurugu hizo na mchezo kuendelea.
Yanga: Elias
Michael, Kitenge Said, Hamisi Mnubi, Athumani Kilambo, Omari Kapera, Gilbert
Mahinya, Awadh Gessan/Leonard Chitete, Juma Bomba/Twaha Masimenti ‘Bryson’,
Kitwana Manara, Maulid Dilunga, Salehe Zimbwe.
Sunderland: Mbaraka
Salum, Yusuf Salum, Ally Durban, Hamisi Kilomoni, Adam Athumani, Mussa Libabu,
Omari Kimimbi, Emmanuel Mbele, Arthur Mambetta, Saidi Abdallah ‘Walala’, Ally
Wage ‘Kajo’.
Mwamuzi alikuwa Bwana Banda kutoka Zambia, na
alisaidiwa na washika vibendera Marijani Shaaban Marijani na Ramadhan Kahabuka
wa Dar es Salaam.
NB: Makala haya ni
kutoka kwenye miswada ya vitabu vya 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' na ‘UBINGWA
WA SOKA TANZANIA’ vya mwandishi Daniel Mbega, ambavyo viko katika hatua za
mwisho kuchapishwa. Ukirejea ni lazima eleze chanzo ambacho ni www.maendeleovijijini.blogspot.com.
Comments
Post a Comment