- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Unknown
on
- Get link
- X
- Other Apps
Kikosi cha Simba cha mwaka 1977 kilichopeleka maafa Jangwani.
Na Daniel Mbega
KATIKA mchezo wa soka kushinda ama kushindwa
ni mambo ya kawaida, lakini vipo vipigo ambavyo timu hupata kiasi cha kujiuliza
mara kumi kumi, kulikoni? Kama kuna kipigo ambacho kitabaki katika kumbukumbu
za Yanga milele na milele ni kile cha mwaka 1977 cha magoli 6-0 kutoka kwa
watani wake wa jadi, Simba, kwenye mchezo wa Ligi ya Taifa.
Kwa waliokuwepo na waliopata simulizi baadaye,
Jumanne ya Julai 19, 1977 ilikuwa siku yenye majonzi makubwa kwa mashabiki wa
Yanga na furaha kubwa kwa wale wa Simba, ambayo kwa ushindi huo, mbali na
kujihakikishia ubingwa wa Ligi ya Taifa kwa kuwa ilibakiza mechi moja tu dhidi
ya Navy (sasa KMKM) ya Zanzibar iliyokuwa ya kukamilisha ratiba, pia ilikuwa
imefanikiwa baada ya miaka tisa kulipa kisasi cha kufungwa magoli 5-0 na Yanga
mwaka 1968.
Kati ya watu waliojihisi wenye furaha
kupindukia walikuwa kocha wa Simba, Dimitier Samsarov wa Bulgaria ambaye
alikuwa na muda mchache tu tokea akabidhiwe timu na nahodha Abdallah Kibadeni
‘Mputa’ ambaye siku hiyo ‘alicheka’ na nyavu mara tatu.
Ilikuwa hadithi ya kifo cha nyani miti yote
huteleza, kwani pamoja na kukuru kakara zote za Yanga, ikiwemo kubadilisha wachezaji
wawili dhidi ya mmoja wa Simba, ambaye alibadilishwa kufuatia mwenzake kuumia
(Martin Kikwa ndiye aliyeumia na kumpisha Abbas Dilunga), mambo yalichacha na
kuvunda kwa vijana wa Jangwani waliokuwa wakipokea mashambulizi mfululizo na
kubaki wakitumia ujanja wa mtego wa kuotea (offside-trick), ambao hata
hivyo, haukusaidia kitu.
Mwaka huo Yanga ilikuwa haijatulia baada ya
mgogoro mkubwa wa mwaka 1976 uliopelekea karibu wachezaji 20 nyota kufukuzwa
kwa madai ya kutokuwa wazalendo na kusababisha Yanga kupoteza taji lake la
ubingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati mjini Mombasa, Kenya mwaka huo.
Wachezaji hao ni Gibson Sembuli, Leodgar Tenga, Sunday Manara, Boi Idd
‘Wickens’, Ally Yusuf, na wengineo ambao walikwenda kuunda timu ya Nyota Afrika
ya Morogoro kabla ya kuanzisha Pan African ya Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Simba walifanikiwa
kujipatia magoli matatu katika kipindi cha kwanza licha ya kucheza huku
wakipingana na upepo katika kipindi hicho. Sentahafu wa Yanga, Selemani Jongo,
ndiye aliyeonekana kuwa kikwazo pekee kwa Simba na hata yeye alilazimika
‘kukubali yaishe’ baada ya washambuliaji wajanja wa Simba kumshitukia, hivyo
kumuandama kama nyuki.
Katika dakika ya pili tu mashabiki, ambao
walianza kuingia uwanjani tangu saa 6.00 mchana, walishuhudia Martin Kikwa wa
Simba akitolewa nje baada ya kugongana na Boniface Makomole aliyekuwa beki wa
kulia wa Yanga na nafasi yake kuchukuliwa na Abbas Dilunga.
Baada ya kosa kosa nyingi kwenye goli la
Yanga na takribani moja tu kwenye goli la Simba pale juhudi za mshambuliaji wa
Yanga, Yanga Fadhil Bwanga zilipozimwa na golikipa wa Simba Omari Mahadhi bin
Jabir, hatimaye karamu ya magoli ilianza kwa Simba kwenye dakika ya 10. Goli
hilo la kwanza lilianzia katikati ya uwanja ambapo Aluu Ally wa Simba aliwakata
chenga beki Charles Mwanga na kiungo Sam Kampambe na kumpasia winga wa kulia,
Willy Mwaijibe, ambaye naye alitoa pasi safi kwa Jumanne Hassan ‘Masimenti’.
Beki Selemani Jongo wa Yanga alitoka kuucheza mpira huo lakini Jumanne
alimuwahi na kumuunganishia Abdallah Kibadeni aliyekimbia na mpira hatua chache
kabla ya kuujaza wavuni huku kipa Bernard Madale akiwa hana la kufanya.
Yanga ilikukuruka baada ya goli hilo na
kukaribia kusawazisha kwenye dakika ya 18 lakini shuti la nambari 8 wao,
Ezekiel Greyson ‘Jujuman’, lililokuwa limeshawanyamazisha mashabiki wa Simba,
lilipaa juu ya goli.
Hata hivyo, Yanga ilikuwa kama imejichongea,
kwani golikiki iliyopigwa kunako dakika ya 20 kufuatia kosa kosa hiyo ndiyo
iliyozaa goli la pili la Simba baada ya gonga za hapa na pale kumfikia Willy
Mwaijibe aliyefumua shuti la chini chini ambalo katika juhudi za kuokoa,
Selemani Saidi Sanga wa Yanga alijikuta akiusindikiza mpira wavuni. Zikiwa
zimesalia dakika chache kuwa mapumziko, kona ya Willy Mwaijibe ilimkuta
Kibadeni katika nafasi nzuri na akaujaza mpira wavuni na kuifanya Simba imalize
kipindi cha kwanza ikiongoza kwa magoli 3-0. Hiyo ilikuwa dakika ya 42.
Katika kipindi cha pili, Yanga ilijitahidi
kutafuta magoli ya kusawazisha lakini baada ya dakika 15 kupita wakiwa bado
hawajafanikiwa kuingia kwenye eneo la goli la Simba wakiishia tu nje ya eneo la
penati, kibao kiliwageukia kwa Aluu kumtangulizia pasi Jumanne aliyemzidi
maarifa Jongo na kusalimiana na kipa Madale na kupachika goli la nne, na dakika
13 baadaye Aluu Ally alimpasia tena Jumanne ambaye kwa mara nyingine alimpita
Jongo na kufunga goli la tano.
Yanga ilikosa kona kadhaa ilizopata. Katika
dakika ya 89 Abbas Dilunga alichomoka kwenye wingi ya kushoto na kumtolea
‘chumba’ Kibadeni aliyekamilisha karamu ya magoli na kuwaacha mashabiki wa
Simba wakilia kwa furaha huku wale wa Yanga wakitokwa na machozi ya simanzi.
Kwa kweli kilikuwa kipigo cha kihistoria.
Mechi hiyo iliingiza jumla ya shilingi
293,664 ambazo kwa wakati huo ndiyo yalikuwa mapato makubwa zaidi kupatikana
katika mechi ya ligi. Kabla ya hapo, pambano la timu hizo mwaka 1974 kwenye
Uwanja wa Nyamagana, Mwanza ndilo lilikuwa likiongoza kwa mapato ambapo
lilikuwa limeingiza shilingi 150,000.
Katika mechi hiyo, timu zilipangwa hivi:
SIMBA: Omari
Mahadhi bin Jabir, Shaaban Baraza, Mohammed Kajole, Aloo Mwitu, Mohammed Bakari
‘Tall’, Athumani Juma, Willy Mwaijibe, Aluu Ally, Jumanne Hassan ‘Masimenti’,
Abdallah Kibadeni (nahodha) na Martin Kikwa/Abbas Dilunga. Kocha: Dimiter
Samsarov (Bulgaria)
YANGA: Bernard
Madale, Boniface Makomole, Selemani Saidi Sanga, Charles Mwanga/Fidelis,
Selemani Jongo, Sam Kampambe, Ayub Shaban/Mrisho Caraby, Ezekiel Greyson
‘Jujuman’, Mwinda Ramadhani ‘Maajabu’ (nahodha), Yanga Fadhil Bwanga na Shaaban
Katwila.
NB: Makala haya ni
kutoka kwenye miswada ya vitabu vya 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' na ‘UBINGWA
WA SOKA TANZANIA’ vya mwandishi Daniel Mbega, ambavyo viko katika hatua za
mwisho kuchapishwa. Ukirejea ni lazima eleze chanzo ambacho ni www.maendeleovijijini.blogspot.com.
Comments
Post a Comment