Featured Post

UGONJWA WA SURUA ULIVYOMLETEA UPOFU SAMBAGI

Msafiri Sambagi mlemavu wa macho, akifanya mahojiano na mwandishi wa Makala haya, katika kijiji cha Mwanyengo.

Na Oliver Motto, Iringa
UKIMUONA, ni kijana mjanja, mcheshi na mwenye kujua mambo sana, anazungumza kwa kujiamini, licha ya kutoona kwake, anajituma katika shughuli za kiuchumi, huwezi kudhani kuwa haoni.
Nikiwa katika kitongoji cha Mwanyengo, katika kijiji cha Migoli ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, mara nakutana na kijana, nasema kwangu hii ilikuwa bahati ya kujifunza mengi kutoka kwake.
Msafiri ni kijana mwenye uhakika na anachozungumza kwa kuwa anajiamini sana, awali sikutambua kama ninayezungumza naye hanioni, nilifanya naye mazungumzo kadha wa kadha, lakini baadaye niliona akihangaika kuitafuta njia.
Aaah, nilishikwa na mshangao na kulazimika kuwauliza wenyeji wangu, juu ya tatizo la Msafiri sambagi, nilisikitika kuambiwa kuwa haoni hata kidogo.
Kwa kweli ya Mungu mengi, na kabla hujafa hujaumbika, niliingiwa na huzuni huku nikimsindikiza kwa macho, yeye akiendelea na safari ya kurudi nyumbani kwake.
Nilianza kumfuata kwa nyuma, nilipomshika bega alistuka, nikamuita “Msafiri” akaniitika, nikamwambia ninaomba kufanya mazungumzo naye.
Hakunionyesha ukaidi Msafiri, niliangalia eneo lenye kivuli na kumshika mkono kumuelekeza nilipotaka tukae ili kuliepuka jua kali lililokuwa likipenya katikati ya utosi hivyo kuona lingekuwa kikwazo cha mazungumzo yetu.
Mimi na Msafiri tulikaa na akaanza kunieleza kilichomsibu hadi yeye kufikia hatua hiyo ya kuwa mlemavu.
Msafiri Sambagi ana umri wa miaka 33, anasema alizaliwa katika kitongoji cha Mwanyengo mwaka 1977.
Amezaliwa akiwa hana hitilafu ya aina yoyote, nikiwa nina hamu ya kujua nini kilimpata hadi kuwa mlemavu wa macho, Msafiri anasema alipokuwa na umri wa miaka 7 alijiunga na  elimu ya msingi katika shule ya wasioona ya Bugiri iliyopo mkoani Dodoma.
Anasema elimu hiyo aliipata kutoka kwa wafadhili, kutokana na wazazi wake kutokuwa na uwezo wa kumudu gharama za ada ya shule.
Anasema hali mnamo mwaka 1994 alimaliza elimu ya msingi, na hivyo kulazimika kurejea nyumbani kwao Mwanyengo.
Anaeleza kuwa hakuweza kuendelea na masomo ya elimu ya sekondari, na hivyo kubaki nyumbani licha ya kupata ujuzi mbalimbali kutoka katika shule aliyokuwa akisoma, kufundisha masomo ya ufundi wa sanaa.
“Shule niliyokuwa nikisoma tulikuwa tunajifunza namna ya kutengeneza mazulia, kupiga kinanda, lakini tulikuwa tunacheza michezo mingi kama mpira wa miguu wenye kengere ndani, mipira ile ilikuwa inatusaidia sisi tusieona kujua mpira unakwenda uelekeo gani, na pia tulijifunza kilimo,” anasema Msafiri.
Anasema mnamo mwaka 2000 alipatwa na majonzi makubwa, baada ya kuondokewa na baba yake mzazi hatua iliyoyafanya maisha yake na familia kwa ujumla kuwa magumu zaidi.
Anasema hapo alilazimika kujituma zaidi ili kuziba pengo aliloliacha mzazi wake huyo, pasipo kujali hali aliyonayo ya kutokuona.
Maisha ambayo aliona kwa wakati huo yanamfaa ni kilimo, kwani hakukuwa na mbadala mwingine wa kufanya kutokana na kutoona.
Anasema amekuwa akihangaika kufanya kazi ya kibarua cha kulima katika mashamba ya watu, ili kupata fedha kidogo za kujikimu kimaisha yeye na mama yake mzazi ambaye anamtegemea.
Msimu wa kiangazi, wakati shughuli za kilimo zikikoma humlazimu kujihusisha na kazi ya kuchoma mkaa, kwa kuwa kuna wakati hulazimika kushinda njaa kutokana na maisha magumu yaliyopo kijijini hapo.
Anasema licha ya kufanya shughuli za kilimo laini amekuwa akikwamishwa na mpango wa serikali wa ugawaji wa pembejeo za ruzuku, kwakuwa mpango huo hauna lengo la kuwakwamua wakulima wadogo kutokana na kutumia pembejeo duni za kilimo.
“Hapa mimi ningeishauri serikali kuwa ituweeshe kutukopesha pembejeo za kisasa ili tuweze kuepukana na kilimo hiki duni cha kutumia majembe ya mkono, sasa wanapotupa mbolea na mbegu, ina maana tunaendelea kuwa na eneo lile lile dogo na hivyo kujikwamua si kazi rahisi,” anasema.
Msafiri anasema endapo serikali itamuwezesha kumpatia jembe la kukokotwa kwa na wanyama kazi kama Ng’ombe na Punda anaweza kuondokana na hali ya umasikini alionao kwa kuwa angekuwa na uwezo wa kulima eneo kubwa la shamba na hivyo kupata mavuno mengi ambayo baadhi yatamsaidia kwa chakula huku mengine akiuza na kujikwamua kiuchumi.
Anafafanua kuwa licha ya kujihusisha na shughuli za kilimo lakini amekuwa akipoteza nguvu na muda mwingi pasipo kuambulia chochote, kutokana na kutumia jembe la mkono.
Anasema na shamba lenye ukubwa wa ekari moja na nusu lakini amekuwa akipata gunia mbili pekee ambazo hazikidhi mahitaji yake kwa mwaka, na hivyo kujikuta akimaliza chakula hicho kabla ya mwaka haujaisha na hivyo kupata taabu sana katika kubuni mbinu za ukupata chakula.
Moja ya changamoto inayomkabili mlemavu huyu ni pamoja na uwepo wa Ndege, wadudu na wanyama waharibifu wa mazao, ambapo kuna  msimu wa kilimo huambulia patupu, na kujikuta mazao yake yakimalizwa na wadudu aina ya Mbilanzi (Viwavijeshi),  Kwembelele, Mijusi ambayo hutafuna mizizi ya mazao, wanyama kama Nyani, pamoja na ndege aina ya Hondohondo, Kangapori pamoja na Njiwa.
Anasema wadudu na wanyama hao wamekuwa wakichangia kudumaza uchumi wa wananchi wa kijiji hicho na hivyo kujikuta kila mwaka wakiwa ombaomba kwa serikali ili kupatiwa msaada wa chakula.
Akizungumzia sababu za yeye kutoona, Msafiri anasema wakati akiwa na umri wa miaka miwili, aliugua ugonjwa wa Surua, ambao ulimshambulia zaidi maeneo ya kichwa na hivyo kuingia katika mboni za macho.
Anasema kutokana na kuchelewa kupata matibabu kwa wakati, ugonjwa huo uliiathiri gololi za macho yake na hivyo kuishia kuwa mlemavu asiyeona maisha,anasema tatizo hilo linamfanya ashindwe kupata mke, na sababu kubwa ikiwa ni kutokuwa na hali nzuri ya kiuchumi, hivyo wanawake kutomkubali kwa kuhofia maisha magumu.
Alisema  hali ya zamani ingekuwa ni sasa,hangekuwa mlemavu kwa kiasi hicho, kwani sasa kuna wataalamu na mabingwa wa macho wenye uwezo wa kulikabiri tatizo hilo.
Msafiri anawashauri walemavu wengine kuacha kubweteka na kuwa omba omba.

Amewataka walemavu kujituma kwa kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia riziki.

Comments