- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Maendeleo Vijijini
on
- Get link
- X
- Other Apps
Tume ya Taifa ya uchaguzi
imesema kuwa Wapiga kura waliopoteza vitambulisho vya kupigia kura watapata
fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi mdogo wa Madiwani wa Kata 43 unaotarajiwa
kufanyika Novemba 26, mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Bw. Ramadhani
Kailima Mjini Dodoma ikiwa ni siku ya pili ya mafunzo ya siku tatu kwa
wasimamizi na wasimamizi wasiadizi wa uchaguzi yanayoratibiwa na kuendeshwa na
NEC.
Bw. Kailima amesema wapiga kura
hao wataruhusiwa kutumia vitambulisho vya uraia vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho
vya Taifa (NIDA), Hati ya kusafiria na Leseni ya udereva.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa
kuzingatia kifungu namba 62 (a) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambacho
kinasema mpiga kura aliyeandikishwa kwenye daftari atakwenda mwenyewe kwenye
Kata aliyojiandikisha na kituo alichopangiwa” Amesema.
Ameeleza kuwa hatua hiyo ni
kumridhisha msimamizi wa kituo au msimamizi msaidizi wa uchaguzi kwamba yeye
ndiye mpiga kura halali na kuongeza kuwa kifungu hicho kinamtaka Mpiga Kura
aonyeshe kadi yake ya kupigia. Aidha, kinaeleza kwamba Tume inaweza ikaelekeza
utambulisho mwingine wowote utakao msaidia mpiga kura kuweza kupiga kura iwapo hana kadi.
Bw.Kailima amesema kuwa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia kifungu hicho, katika uchaguzi mdogo utakaofanyika
Novemba 26, 2017 imetoa maelekezo kwa Wasimamizi wa Uchaguzi kuruhusu wapiga
Kura waliojiandikisha kwenye Dafatari la kudumu la Wapiga Kura kutumia Hati ya
kusafiria, kitambulisho cha Taifa kilichotolewa na NIDA na leseni ya udereva.
Bw. Kailima amesema ruhusa hiyo
imetolewa kwa sharti moja kwamba majina na herifu yaliyopo kwenye kitambulisho
hicho yafanane na majina na herufi zilizopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura.
Ameongeza kuwa NEC itakutana na
vyama vya siasa hivi karibuni kuwajulisha juu ya maagizo hayo na kusisitiza kwamba
tofauti yoyote itakayo kuwepo kwenye majina itamnyima mpiga kura fursa ya
kupiga kura.
Bw. Kailima amesema maamuzi
hayo yamefikiwa kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa kwenye daftari la
kudumu la wapiga kura ambalo kwa mara ya mwisho liliboreshwa mwaka 2015.
“ Katika kipindi chote hichi (2015-2017)
inawezekana kwa namna moja ama nyingine, kuna baadhi ya wapiga kura wamepoteza
kadi zao za kupigia kura na kwa sababu hatujaboresha na sheria inasema watapata
hizo kadi baada ya daftari kuboreshwa, wanaweza wakakosa fursa ya kupiga kura
kwenye uchaguzi wa madiwani wa kata 43, lakini wengine kadi zao zimeharibika
kiasi kwamba haziwezi kusomeka, na wengine kadi zao zimechakaa kabisa kwa
sababu moja ama nyingine kutokana na mazingira yaliyopo,” amesema.
Wakitoa maoni yao juu ya agizo
hilo la NEC, washiriki wa mafunzo hayo wamepongeza hatua hiyo na kusema kwamba
itakuza wigo wa demokrasia nchini kwa kuwapa fursa wapiga kura halali ambao kwa
sababu zilizoko nje ya uwezo wao wamejikuta hawana kadi za kupigia kura licha
ya kwamba ni wapiga kura halali waliojiandikisha.
Bw. Abdul Kasembe ambaye ni
Afisa Uchaguzi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma amesema kuwa
amefurahishwa na uamuzi huo akieleza mambo mengi yamejitokeza kati ya mwaka
2015 mpaka sasa.
“Sisi tumefurahia agizo hili
kwa kuwa litawapa fursa wananchi ambao pengine wangeikosa fursa kwa kuwa hawana
kadi japokuwa wamejiandikisha”.
Bi. Margaret Nakayinga,
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Mkoani Tabora amesema
agizo hilo limeleta fursa kwa watu ambao pengine wangekosa fursa ya kupiga kura
kwa kupoteza kadi ya kupigia kura au kwa kuharibika kwa kadi zao. Tutakaporudi
huko tutawatangazia wananchi ili wajitokeze kwa wingi kupiga kura..”.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Mkoani Tanga, Bw. Kazimbaya Makwega
amesema kuwa agizo hilo ni muafaka na limezingatia mazingira ya Kitanzania kwa
kuwa watu wanaweza kupoteza kadi au kuharibikiwa na kadi zao na kukosa fursa ya
kupiga kura.
Comments
Post a Comment