- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Unknown
on
- Get link
- X
- Other Apps
Hamis Ramadhani Kinye alidaka mechi hiyo
Na
Daniel Mbega
PENGINE msemo wa ‘Mvumilivu hula mbivu’ ndio
ulioipa nguvu Yanga, kwani baada ya vipigo vya miaka mitatu mfululizo kutoka
kwa Simba, hatimaye ilikata mzizi wa fitina na kuichapa goli 1-0 kwenye Uwanja
wa Taifa Septemba 5, 1981.
Inawezekana nao Simba walipitiwa na ule msemo
‘Ukiona Kobe kainama ujue anatunga sheria,’ ndiyo maana kila walipojaribu
kuipenya ngome ya Yanga siku hiyo ilikuwa haipenyeki na hata walipofungwa goli
hilo bado ‘waliamini’ wangesawazisha na kuongeza lingine kama ilivyokuwa
kawaida yao. Juhudi zao zote zikawa kama zile za ‘mfa maji, ambaye haishi
kutapatapa’.
Matokeo hayo yalifanya wapenzi wa soka
waliofurika kwenye uwanja huo siku hiyo kusema kwamba, ‘Bubu ameongea
uwanjani’, wakiwa na maana kwamba, vipigo vitatu bila majibu viliifanya Yanga
kuwa bubu, yaani haikutamba mbele ya Simba.
Hata hivyo, Yanga mwaka huo ilikuwa imara,
kwani awali ilikuwa imezifunga Coastal Union 2-1, Pamba ya Kigoma 4-1, Biashara
Kagera 5-1, CDA 2-0, KMKM 3-0 na baadaye kuifunga tena CDA 2-1 ingawa ilikuwa
imetoka sare ya goli 1-1 na TCC (Sigara) ya Dar es Salaam.
Simba ilizifunga Tembo ya Ruvuma 2-0,
Biashara Kagera 1-0, Pamba Mwanza 2-1, Ujamaa ya Zanzibar 4-1, CDA 2-1, lakini
mbali ya kufungwa na Yanga na kuvuliwa ubingwa, pia ilifungwa na Pan African
mara mbili. Kwanza ilifungwa goli 1-0 halafu ikafungwa magoli 2-0 katika mchezo
wa mwisho wa ligi hiyo.
Katika ligi hiyo, mchuano ulioleta upinzani
mkubwa msimu huo ulikuwa huo wa wapinzani wa jadi. Ilikuwa wazi kabisa kuwa,
Yanga ya mwaka huo haikuwa ile ya miaka iliyopita, na Simba waliona hali
ilivyokuwa ngumu kwao.
Goli lililokata mzizi wa fitina kwa Simba
lilifungwa na nahodha wa Yanga, ‘Jenerali’ Juma Mkambi katika dakika ya 42
kufuatia mpira wa kona uliopigwa na mlinzi wa kushoto wa timu hiyo, Ahmad
Amasha kutoka magharibi ya uwanja upande wa kusini. Mlinda mlango wa Simba,
Omari Mahadhi bin Jabir, aliupiga kwa ngumi na ukamfikia Mkambi, ambaye bila
ajizi aliutumbukiza wavuni kwa kichwa.
Ukiacha rafu za hapa na pale, mpira ulikuwa
safi na Yanga wangetulia, basi wangejipatia magoli mengi. Hata hivyo, kwa ushindi
huo, Yanga wakawa na matumaini ya ubingwa, kwani baada ya kuifunga CDA 2-1 sasa
ikabakia na mchezo dhidi ya Pan African, ambapo ilihitaji sare ili kuwa bingwa.
Na ndivyo ilivyokuwa katika mchezo wao wa Septemba 13, kwenye Uwanja wa Taifa,
ambapo timu hizo hazikufungana.
Mashindano ya mwaka huo, licha ya kubadilisha
ushindi kutoka kwa Simba, ambao waliuchukua kwa miaka mitano mfululizo,
yalionyesha pia kukomaa kwa Yanga. Baada ya mwaka huo timu hizo zilikuwa na
nguvu, unyonge wa Yanga ukaondoka kabisa. Kama ushindi ulipatikana kwa Simba
dhidi ya Yanga, ulikuwa kwa juhudi na maarifa kuliko unyonge wa kutokukomaa.
Tangu hapo Simba walijua kuwa Yanga siyo tena timu ya kudharau.
Jumla ya shilingi 818,845 zilipatikana, watu
31,608 walilipa kiingilio.
Timu hizo ziliwakilishwa na:
YANGA: Hamisi
Kinye, Athumani Juma ‘Chama’, Ahmad Amasha, Allan Shomari, Charles Boniface,
Shaaban Katwila/Charles Kilinda, Juma Mkambi (nahodha), Rashidi Hanzuruni,
Omari Hussein.
SIMBA: Omari
Mahadhi, Kihwelu Mussa, Mohammed Kajole, Yussuf Ismail Bana, Mohammed Bakari
‘Tall’, Nico Njohole, George Kulagwa, Mrage Kabange, Jumanne Hassan
‘Masimenti’/Adamu Sabu, Abdallah Mwinyimkuu.
NB: Makala haya ni
kutoka kwenye miswada ya vitabu vya 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' na ‘UBINGWA
WA SOKA TANZANIA’ vya mwandishi Daniel Mbega, ambavyo viko katika hatua za
mwisho kuchapishwa. Ukirejea ni lazima eleze chanzo ambacho ni www.maendeleovijijini.blogspot.com.

Comments
Post a Comment