- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
HII NDIYO ‘THRILLER IN NYAMAGANA’ ILIYOSABABISHA SHABIKI WA SIMBA AJITOSE KWENYE PIPA LA POMBE YA MOTO NA KUFA MWAKA 1974
Posted by
Unknown
on
- Get link
- X
- Other Apps
Kipa wa Simba, Athumani Mambosasa, akiunyaka mpira huku
akitazamwa na Kitwana Manara 'Popat' wa Yanga (kushoto).
Kikosi cha Yanga cha mwaka 1973 kabla Dk. Victor Stanculescu
(wa pili kushoto) hajaondoka. Anayeongea na wachezaji na meneja wa timu, Shiraz
Sharrif. Wengine ni Hassan Gobbos, Kitwana Manara, Maulid Dilunga, Sunday
Manara, Elias Michael, Boi Idd 'Wickens', Selemani Said, Gibson Sembuli, Omar
Kapera, Ally Yussuf, Abdulrahman Juma (nahodha).
Na Daniel Mbega
KWA wenye kumbukumbu nzuri bila shaka kipigo
cha Nigeria cha magoli 2-1 toka kwa Italia katika raundi ya pili ya Kombe la
Dunia huko Marekani mwaka 1994 kiliwarudisha mapema miaka ya 1970 pale Yanga
ilipoichapa Simba magoli 2-1 kwenye fainali ya Ligi ya Taifa ya Soka kwenye
Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.
Nasema huenda kumbukumbu hiyo ikawa
imejitokeza kufuatia kufanana kwa kiasi kikubwa kwa matokeo hayo, hasa muda,
yaani ‘timing’, magoli hayo yalipopatikana.
Katika mchezo wa Nigeria na Italia Alhamisi
ya Julai 14, 1994, Nigeria ilikuwa ikiongoza kwa goli moja ililolipata mapema
kunako dakika ya 26 hadi dakika ya 87 Roberto Baggio alipoisawazishia Italia na
kuufanya mchezo huo uingie kwenye muda wa nyongeza.
Kisha kwenye dakika ya 11
ya muda wa nyongeza, Baggio tena alifunga goli la penati na kuiondoa Nigeria
mashindanoni. Ndivyo ilivyokuwa kwenye mchezo wa Simba na Yanga wa mwaka 1974.
Pengine watu watajiuliza kwa nini Simba na
Yanga zilipambana kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza badala ya Karume au Taifa
mjini Dar es Salaam zinakotoka timu hizo. Kwa kweli hili lilikuwa pambano lao
la kwanza la Ligi ya Taifa kufanyika nje ya Dar es Salaam.
Mashindano ya kutafuta klabu bingwa nchini
mwaka 1974 yalifanyika kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza tangu Julai 18 hadi
Agosti 10, 1974. Timu maarufu zilikuwepo pamoja na nyingine ngeni. Timu hizo
maarufu zilikuwa Yanga na Simba za Dar es Salaam, Nyota ya Mtwara, Mwadui ya Shinyanga
na Jumuiya ya Arusha. Halafu ikatokea timu mpya kabisa huko mkoani Dodoma
iliyoitwa Ntomoko. Timu nyingine za mwaka huo zilikuwa ni za kazini. Hakukuwepo
na timu kutoka Zanzibar msimu huu.
Hata hivyo, upinzani mkubwa kwenye ligi hiyo
ulikuwa kati ya Simba na Yanga, watani wa jadi wa soka nchini. Wakati huo Simba
walikuwa mabingwa baada ya kuwafunga Lake Stars ya Kigoma magoli 2-0 mwaka 1973
kama tulivyoona huko nyuma. Watu walikuwa wanajiuliza nani angeibuka bingwa
mwaka 1974 hasa ikizingatiwa kwamba, Yanga ilifungwa na Simba goli 1-0 kwenye
nusu fainali mwaka 1973.
Kwa matayarisho kabla ya mashindano hayo,
Simba walikwenda kuzuru Poland nao Yanga walikwenda Brazil, ambako walikutana
na Mfalme wa Soka Duniani, Edson Arantes do Nascimento ‘Pele’. Katika timu zote
zilizokuwemo kwenye mashindano hayo hakuna hata moja iliyokuwa na matayarisho
makubwa kama Yanga na Simba.
Simba na Yanga zilifanikiwa kuingia fainali
baada ya kuzichabanga timu nyingine kwenye michuano ya awali ya mtoano. Pambano
hilo la mwisho na la kihistoria lilifanyika Nyamagana Jumamosi Agosti 10, 1974.
Siku hiyo Uwanja wa Nyamagana ulifurika watu
isivyo kawaida. Mashabiki walitoka sehemu mbalimbali za nchi - Arusha, Moshi,
Tanga, Dodoma, Dar es Salaam, Tabora, Shinyanga, Kigoma, Morogoro, Mara na
Kagera. Hao ni licha ya wale waliotoka kwenye vitongoji vya Mwanza. Ilipofika
saa 10.30 jioni hapakuwa na nafasi ya kukaa mtu hapo uwanjani, ingawa wengine
walikuwa wanaendelea kumiminika.
Mchezo ulianza kwa nguvu ingawa Yanga
walianza pole pole kidogo wakijaribu kuusoma mchezo wa Simba. Baada ya dakika
tano tu matokeo ya nguvu hizo yalionekana. Saad Ally wa Simba aliumia baada ya
kugongana na Gibson Sembuli wa Yanga na akatolewa nje. Adamu Sabu aliyeingia
badala yake, aliwafurahisha wapenzi wa Simba, kwani aliifungia goli timu yake
katika dakika ya 16.
Yanga walijaribu sana kukomboa goli hilo
lakini walipata taabu kwani ukuta wa Simba ulikuwa imara sana. Kadiri mchezo
ulivyoendelea watu walidhani Yanga isingepata hata goli moja na kwamba, siku
hiyo ingefungwa tena, kwani hadi mapumziko matokeo yalikuwa ni yale yale ya
goli moja kwa Simba na Yanga wakiwa na gurudumu.
Katika dakika ya 87 ya mchezo, yaani dakika
tatu kabla ya mchezo kumalizika, mambo yalibadilika. Ilikuwa ni golikiki,
ambapo mlinzi wa Yanga, Ally Yussuf, alipiga mpira kuelekea golini kwa Simba.
Mpira huo ulipita juu ya vichwa vya wachezaji kadhaa wakiwemo Abdallah Kibadeni
wa Simba na Gibson Sembuli na Sunday Manara.
Mpira huo uliambaa ambaa kuelekea goli la
Simba ambako Kitwana Manara, aliyekuwa amebanwa mno na beki wa Simba ambaye
hakutaka mchezo, Omari Chogo ‘Chemba’, licha ya kuwa ameupa mgongo mpira huo
aliruka na kupiga kichwa kushoto kwake.
Moja kwa moja mpira huo uliingia kwenye
‘anga’ za nambari nane wa Yanga, Gibson Sembuli, aliyeujaza wavuni kwa shuti
kali la ugoko, lililoingilia kwenye kona ya kushoto na kumuacha kipa Athumani
Mambosasa, aliyekuwa ametoka kumkabili mchezaji huyo, akiwa hana la kufanya
zaidi ya kuutumbulia macho mpira huo ukitinga wavuni kuandika goli la
kusawazisha kwa Yanga. Hivyo, hadi mwisho wa dakika 90 za kawaida za mchezo
matokeo yalikuwa 1-1.
Goli hilo likabadilisha kabisa sura ya
mchezo. Watazamaji ambao walianza kuondoka uwanjani wakidhani Yanga wameshindwa
walikimbilia uwanjani kuangalia mchezo tena. Dakika 90 zilipokwisha ubao wa
matokeo ukasomeka Yanga 1 Simba 1 na ndipo dakika 30 zilipoongezwa ili kupata
mshindi.
Katika dakika ya saba ya muda wa nyongeza,
mlinzi Ally Yussuf wa Yanga aliipangua ngome ya Simba na kutoa pasi ya juu kwa
mchezaji wa kiungo wa Yanga, Sunday Ramadhan Manara, aliyefunga goli la pili
kwa kichwa. Goli hilo likawa la ushindi kwa Yanga baada ya Simba kushindwa
kusawazisha kwa dakika 23 zilizokuwa zimesalia.
Hili ni pambano lao la kwanza la ligi
kumalizika baada ya muda wa kawaida, yaani ndilo pambano pekee kwa wakati huo
lililokuwa limechezwa kwa dakika 120. Mapambano mengine manne huko nyuma
yalikuwa yamevunjika kabla ya muda wake na siyo zaidi ya muda wake.
Ikawa Yanga wamechukua ubingwa wa Tanzania
kwa ushindi wa magoli 2-1 na kuinyang’anya Simba iliyoutwaa mwaka 1973 kutoka
kwao. Kombe hilo lilikabidhiwa kwa nahodha wa Yanga wa wakati huo, Abdulrahman
Juma na aliyekuwa mgeni rasmi Meja Jenerali Mrisho S.H. Sarakikya mbele ya
mashabiki takriban 50,000 waliohudhuria.
Ilielezwa kuwa, sababu kubwa iliyoifanya
Simba isalimu amri ni ukweli kwamba, haikuwa na stamina ya kumudu kucheza
dakika 120 wakati ambapo watani wao, Yanga, walikuwa na uwezo huo na kufanikiwa
kufunga magoli safi yaliyotinga wavuni katika staili ambayo ingemshinda
golikipa yoyote kuzuia, ingawa baadhi ya wachezaji wa Simba walikaririwa
baadaye wakimlaumu kipa wao Mambosasa kwamba, aliwafungisha kwa uzembe.
Kadiri mchezo ulivyokuwa ukisonga mbele
ilijidhihirisha kuwa Yanga walistahili ushindi huo ukitilia maanani jinsi
mashambulizi yalivyoielemea Simba. Mtu aliyeivunja nguvu kabisa ngome ya Simba
alikuwa mshambuliaji hodari nambari tisa, Kitwana Manara, aliyekuwa na mazoea
ya kutegea mbele anakobaki na beki mmoja tu, na ambaye kwenye mechi hiyo
alikuwa Chogo. Haikuwa ajabu pale beki huyo alipotolewa nje baada ya mambo
kumzidia uwanjani.
Katika pambano hilo, golikipa wa Yanga, Elias
Michael aligongana na Willy Mwaijibe wa Simba katika dakika ya 70 na wote
wawili wakakimbizwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Bugando. Nafasi zao
zilichukuliwa na Muhidin Fadhil kwa upande wa Yanga na Kessy Manangu kwa upande
wa Simba.
Simba walifanya faulo 17 dhidi ya wachezaji
wa Yanga, nane zikiwa katika kipindi cha kwanza, wakati ambapo Yanga ilicheza
faulo 18, 10 zikiwa katika kipindi cha kwanza, ambacho kwacho Simba ilitawala
zaidi kiasi cha Yanga kulazimika kutumia, japo kwa kiasi kidogo, uamuzi wa
‘Aende mtu mpira ubaki, au uende mpira mtu abaki’.
Aidha, katika mchezo huo, Yanga ilitumia
zaidi mchezo wa kuotea (offside trick) na kuwafanya wachezaji wa Simba waotee
mara 15 wakati wale wa Yanga, kwa kutowekewa mtego kama huo, walijikuta
wakiotea takribani mara mbili tu.
Udhaifu wa Simba kwenye kufunga magoli
ulionekana kwenye upigaji mipira ya kona, ambapo ilipata kona sita bila hata
moja kutinga wavuni. Yanga ilipata kona mbili zote katika kipindi cha kwanza,
na kwa jinsi zilivyolikosakosa goli la Simba, huenda magoli zaidi yangetinga
kama ingepata kona zaidi.
Shabiki mmoja wa Simba huko Nzega aliamua
kujitumbukiza kwenye pipa la kirusu cha pombe kilichokuwa jikoni na kufa wakati
Yanga iliposawazisha bao. Kiingilio cha juu siku hiyo kilikuwa shilingi 30.
Timu zilipangwa hivi:-
YANGA: Elias
Michael/Muhidin Fadhil. Ally Yussuf, Selemani Saidi, Hassan Gobbos/Boi Iddi
‘Wickens’, Omari Kapera, Abdulrahman Juma (nahodha), Bona Max Mwangi, Sunday
Manara, Kitwana Manara, Gibson Sembuli na Maulid Dilunga. Kocha: Tambwe Leya
(Zaire)
SIMBA: Athumani
Mambosasa, Shaaban Baraza, Mohammed Kajole, Athumani Juma, Omari Chogo, Omari
Gumbo, Willy Mwaijibe/Kessy Manangu, Haidari Abeid ‘Muchacho’ (nahodha), Saad
Ally/Adamu Sabu, Abdallah Kibadeni, Abbas Dilunga. Kocha: Paul West Gwivaha.
Mgeni rasmi, alikuwa Meja Jenerali Mrisho
S.H. Sarakikya.
NB: Makala haya ni
kutoka kwenye miswada ya vitabu vya 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' na ‘UBINGWA
WA SOKA TANZANIA’ vya mwandishi Daniel Mbega, ambavyo viko katika hatua za
mwisho kuchapishwa. Ukirejea ni lazima eleze chanzo ambacho ni www.maendeleovijijini.blogspot.com.
Comments
Post a Comment