- Get link
- X
- Other Apps
Featured Post
Posted by
Unknown
on
- Get link
- X
- Other Apps
Dua Said
Na
Daniel Mbega
LIGI Kuu ya Muungano iliyosadikiwa kuwa na
msisimko wa kipekee msimu huo kwa vile ilikuwa inawahusisha kikamilifu
mamilionea wote watano waliokuwa wanafadhili soka nchini Tanzania, ilianza
rasmi Jumamosi Septemba 25, mwaka huo 1993 na ilitarajiwa kupamba moto zaidi
Jumapili katika kindumbwendumbwe cha aina yake kwa kuzikutanisha Simba na
Yanga.
Siku hiyo ya Jumamosi Uwanja wa Ally Hassan
Mwinyi mjini Tabora ulianza ukurasa mpya wa kumbukumbu zake kwa mechi za Ligi
Kuu ya Muungano kuchezewa kwenye nyasi zake. Abbas Gulamali, Murtaza Dewji,
Azim Dewji, Mohammed Raza na Naushad Mohammed, wafanyabiashara wa Tanzania
wenye asili ya Asia, ambao walikuwa wamebobea katika kutumia utajiri wao
kuzifadhili timu kubwa nchini, walitarajiwa kuonyesha ubabe katika ligi hiyo na
mwenzao Salim Kanji alikuwa anakabiliwa na upinzani mkali. Hivyo, ligi hiyo
ilitazamiwa kutegemea zaidi mbinu za midani kuliko kiwango cha soka.
Naushad wa Malindi Jumamosi hiyo alikuwa
anamkabili Kanji wa Milambo huko Tabora, na huko Zanzibar, Shangani ya Raza
ilikuwa inachuana na Mlandege kwenye Uwanja wa Amaan. Septemba 26 ndiyo siku
iliyokuwa inatazamiwa kuwa ngumu zaidi, kwani timu za akina Gulamali na Dewji
wawili zilikuwa zinachuana kwa hali ya upinzani wa juu.
Baada ya kila timu kumfunga mwenzake katika
Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, Simba na Yanga katika mchezo wao huo
zilitarajiwa kuanza upya. Azim Dewji alisononeka sana mpaka akagombana na
polisi wakati Saidi Mwamba ‘Kizota’ alipofunga magoli mawili dhidi ya moja la
Edward Chumila hapo Machi 27, lakini Julai 17 ikawa zamu ya Gulamali kulia
machozi wakati Dua Said alipoifungia Simba goli pekee la ushindi.
Sasa Jumapili hiyo Azim alitarajiwa kutingwa
na Gulamali na Murtaza, mfadhili aliyeweza kuinyanyua Pan African kutoka daraja
la tatu hadi la kwanza na wakati huo sasa alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Yanga na
jukumu lake la kwanza lilikuwa kwenye ligi hiyo. Pengine ni kwa sababu hiyo
Azim alilazimika kuyafuta mapokezi ambayo awali yalipangwa kuwa makubwa wakati
timu ya Simba ilipowasili Jumamosi ikitokea Algeria ambako ilifaulu kuingia
nusu fainali ya Kombe la CAF kwa kuitoa USM El-Harrach ya huko kwa jumla ya
magoli 3-2.
Swali kubwa lilikuwa, Je, Simba ingefanya
kile kilichofanywa na Yanga Aprili 22 mwaka 1992? Ikitokea Cairo, Misri kwa
shindano la ubingwa wa Afrika dhidi ya Ismailia, Yanga iliwasili Jumamosi
mchana na kesho yake ikawalaza Simba goli 1-0.
Simba na Yanga ndizo zilizokuwa zoefu kwenye
ligi hiyo mwaka huo zikifuatiwa na Malindi, lakini zilizosalia zote zilikuwa
ngeni na mikikimikiki hiyo. Yanga, waliokuwa mabingwa wa Tanzania Bara kwa
misimu miwili mfululizo na kushikilia ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati,
mpaka wakati huo ndiyo iliyokuwa inaongoza kwa kutwaa ubingwa wa Muungano mara
nyingi zaidi, na mwaka 1992 ilivuliwa na Malindi. Mpaka wakati huo, Simba
haikuwa imetwaa ubingwa huo kwa miaka 12 mfululizo na pengine kazi kubwa
ilikuwa inamkabili mwenyekiti mpya Amir Ally ‘Bamchawi’, kufuta doa hilo kwa
klabu yake ambayo hadhi yake haikustahili kuukosa ubingwa wa taifa kwa muda
wote huo.
Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Malindi,
safari hiyo hawakutamba sana huko Zanzibar mpaka wakavuliwa taji na timu ngeni
kabisa, Shangani. Malindi walikuwa washiriki wa mara kwa mara wa ligi hiyo
tangu mwaka 1989 na huo waliokuwa wakiutetea ulikuwa ubingwa wao wa pili nchini
Tanzania. Mabingwa wapya wa Zanzibar, Shangani, pamoja na Milambo na Mlandege,
ni timu zilizokuwa zinashiriki kwa mara ya kwanza katika mashindano hayo, hivyo
uwezo wao katika ligi hiyo ungeonekana wakati wa harakati zenyewe.
Waswahili husema, ‘Usimlaumu dobi, weusi wa
kaniki nd’o rangi yake’. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa timu ya mtaa wa Jangwani,
Jijini Dar es Salaam, Young Africans (Yanga), ambayo ilimfukuza kocha wake,
Nzoysabah Tauzany raia wa Burundi, baada ya kushindwa kwa mara ya pili
mfululizo na watani wao wa jadi, Simba pia ya Dar es Salaam.
Mwanzoni, Yanga ilifungwa bao 1-0 katika
mchezo wa marudiano wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara uliofanyika kwenye
Uwanja wa Taifa Julai 17, ushindi ambao uliendelezwa pia Jumapili hiyo Septemba
26 katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Muungano, tena na mshambuliaji yule
yule, Dua Said, na kuwaacha wapenzi, mashabiki, wanachama na viongozi wa Yanga
wakiwa hawaamini kilichotokea.
Ushindi wa vijana hao wa Msimbazi dhidi ya
Yanga ulikuwa dhahiri tangu walipoweza kuhimili fujo za Waarabu huko Algeria
wakati wa mchezo wa marudiano katika Kombe la CAF. Hivyo, mashambulizi ya Yanga
hayakuwa tishio kubwa kutokana na ukweli kuwa, Simba ilikuwa tayari na hesabu
za kuwazuia kwa jinsi watakavyo.
Kama Yanga wangekuwa na mashambulizi ya
kimahesabu wangeweza kujipatia mabao kwenye mechi hiyo iliyokuwa ngumu
kutabirika wakati wa mwanzo, lakini Malota Soma ‘Ball Juggler’, ambaye alifunga
bao kwenye dakika ya nane lakini likakataliwa, alionyesha dhahiri kuwa,
wapinzani wao hao walikuwa na mwanya ambao ungeweza kutumika kuweza kujipatia
bao, na katika dakika ya 13 Simba iliweza kulipata kupitia kwa Dua Said
kutokana na shambulizi kali lililojengwa na Kassongo Athumani, Ramadhan Lenny,
Abdul Mashine na Edward Chumila.
Bao hilo la Dua halikuleta mzozo wowote
kutokana na ukweli kwamba, ni bao ambalo limezoewa na kila Mtanzania, akiwemo
mwamuzi wa mchezo huo, Mfaume Ally wa Zanzibar, kinyume na lilivyokuwa bao
la Malota.
Ngome ya Simba ilistahili sifa zote kutokana na kuweza kulinda lango kwa
kutumia akili zaidi badala ya kubutua mpira ovyo. George Masatu, Fikiri
Magosso, Kasongo Athumani na Deo Mkuki walifanya kila lifanywalo na ngome
katika kudhibiti wapinzani ambao mara nyingi walijikuta wakiingiwa na mchecheto
kiasi cha kupiga mipira nje na hata walipokuwa wakibakia na kipa Mohammed
Mwameja walishindwa kumalizia.
Kwa kufukuzwa Tauzany, Yanga sasa ilikuwa
chini ya Charles Boniface Mkwasa aliyekuwa kocha msaidizi.
YANGA: Riffat
Said, Selemani Mkati, Kenneth Mkapa, Willy Mtendawema, Issa Athuman, Method
Mogella (nahodha), Sanifu Lazaro, Stephen Mussa, Said Mwamba, Mohammed Hussein,
Edibilly Lunyamila.
SIMBA: Mohammed
Mwameja, Kasongo Athumani, Deo Mkuki, Fikiri Magoso, George Masatu, Hussein
Marsha (nahodha)/Iddi Selemani, Edward Chumila, Ramadhan Lenny, Abdul Mashine,
Malota Soma, Dua Said.
Mwamuzi katika mchezo huo alikuwa Mfaume Ally
wa Zanzibar na mgeni rasmi alikuwa Balozi wa Sweden Nchini, Thomas Palme.
NB: Makala haya ni
kutoka kwenye miswada ya vitabu vya 'VUTA-NIKUVUTE: SIMBA NA YANGA' na ‘UBINGWA
WA SOKA TANZANIA’ vya mwandishi Daniel Mbega, ambavyo viko katika hatua za
mwisho kuchapishwa. Ukirejea ni lazima eleze chanzo ambacho ni www.maendeleovijijini.blogspot.com.
Comments
Post a Comment